Wabunge waungana kuhoji umeme vijijini
Dodoma. Wabunge wameungana kuitaka Serikali kueleza kwa nini utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme umekuwa ukiruka vijiji au vitongoji.
Pia wamehoji kukwama kwa mradi wa gesi iliyosindikwa (LNG) mkoani Lindi lakini wakatofautiana katika mradi wa umeme wa Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge.
Hayo yalijiri jana bungeni jijini Dodoma wakati wabunge wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2019/20 ya Sh2.14 trilioni ambayo kati ya fedha hizo, asilimia 98.8 zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Wakichangia, wabunge wa CCM licha ya kusifia juhudi za Serikali kupeleka umeme vijijini, walikosoa baadhi ya vijiji au vitongoji kurukwa huku mradi wa Stiegler’s Gorge ukiwagawa; wapinzani wakiukosoa na wa chama tawala wakiukingia kifua.
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliipongeza Serikali kwa, “kuhuisha mradi wa LNG ambao ni mkubwa kuliko miradi yote nchini kama wa reli, ATCL, Stiegler’s Gorge ukichukua kwa pamoja mradi huu bado ni mkubwa na uamuzi huu ni mzuri na mkubwa sana.
“Pamoja na kwamba ni mkubwa lakini ni ushahidi wa sekta binafsi katika kuendeleza mradi huu kwani karibu dola bilioni 30 zitaletwa na sekta binafsi na naipongeza Serikali. Malizeni mazungumzo ya huu mradi na Serikali iwawezeshe wazawa,” alisema waziri huyo wa zamani wa habari, utamaduni, sanaa na michezo
Alitaka Serikali ikamilishe mazungumzo aliyosema yamechukua muda mrefu akisisitiza ushiriki wa wazawa na kuwezeshwa ili washiriki kwenye sekta ya nishati na ya uwekezaji. “Tuwachukue wazawa na kuwawezesha.”
Mbunge wa Lupembe (CCM), Joram Hongoli alisema, “kasi ya usambazaji katika maeneo mengi hairidhishi na mkandarasi aliyepo jimboni kwangu alianza mwaka jana lakini mpaka sasa amepeleka vijiji viwili na katika vijiji hivyo amepeleka katika vitongoji viwili tu.”
Kuhusu LNG alisema, “LNG mimi napongeza lakini napata mashaka makubwa sana na jambo hili. Limekuwapo tangu mwaka 2010 na tuliambiwa uchumi wa Kusini ungepanda kama LNG ingeanza kufanya kazi lakini mazungumzo hayafiki mwisho.”
Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi alisema, “huu mradi (Stiegler’s Gorge) tusiuzungumzie sana na Serikali imekwisha kubaliana na mradi huu, imedhamiria, imesema haiyumbishwi na kihistoria Serikali ya Rais John Magufuli inatekeleza miradi yote.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema licha ya Serikali kusema mradi huo ukikamilika gharama zake zitakuwa Sh6 trilioni lakini kwa mwenendo ulivyo zinaweza kuzidi. Alisema awamu hii inaweza kuweka rekodi ya kuanzisha miradi mingi lakini ikawa haina tija kwa Taifa kwani itachukua muda mrefu kuanza kufanya kazi.
Majibu ya Serikali
Akijibu hoja kuhusu LNG, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema Serikali inapitia mikataba 11 ya uchimbaji na utafiti wa gesi na mazungumzo ya tatu na ya mwisho yatafanyika kati ya Juni 6 na 25. Alisema katika mapitio ya kwanza, suala lililopewa nafasi zaidi ni ule mpango wa muundo wa kiuchumi na kifedha.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akijibu hoja ya umeme kuruka vijiji alisema, “tumewasikia, tunahitaji kufanya kazi ili kuunganisha vijiji vyote na mradi huu wa Rea Awamu ya Tatu, tunatambua makandarasi ambao wanafanya vizuri na wale ambao hawafanyi vizuri.”
Alisema licha awamu hiyo kumalizika Juni mwakani, aliwaeleza wabunge kwamba hadi Desemba mwaka huu watakuwa wamekamilisha masuala ya msingi.
Pia, aligusia suala la LNG akisema, “ni kweli mazungumzo yamechelewa, yalikwama kutokana na wabia kutofautiana, sasa yanakwenda vizuri na tunatarajia yatakamilika Septemba 2019.”
Kuhusu Stiegler’s Gorge, Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji alisema kutokana na umuhimu wa mradi huo, waziri wa fedha alihamisha Sh23 bilioni fedha kutoka Hazina.
Alisema mpaka sasa Serikali imelipa Sh723.59 bilioni licha ya Bunge kupitisha Sh700 bilioni na kutokana na umuhimu wa mradi huo imeongeza Sh23 bilioni.
“Mamlaka ya kufanya uhamisho wa kutoka fungu moja kwenda jingine ni ya waziri wa fedha na kunapokuwa na jukumu kubwa la muhimu anafanya hamisho na hii Sh23 bilioni amehamisha fungu 21 Hazina kwenda fungu 28 ili mradi huu uweze kutekelezwa na taifa lianze kupata faida.”
Comments
Post a Comment