Kada wa CCM Arusha Mbaroni kwa Ujambazi

Kada wa CCM Arusha Mbaroni kwa Ujambazi

JESHI la polisi mkoani Arusha linamshikilia mtuhumiwa sugu wa ujambazi, Jumanne Mjuzi (J4) mkazi wa Ngarenaro jijini Arusha ambaye pia ni kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kosa la kuvunja na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo bastola moja yenye risasi tisa.

Mtuhumiwa huyo maarufu kwa kutambaa kwenye kuta za nyumba za watu anapokuwa akitekeleza uhalifu huo, alikamatwa Mei 16 mwaka huu majira ya saa 11 jioni baada ya kuvamia na kuvunja nyumba ya mkazi mmoja wa eneo la Olasiva anayejulikana kwa jina la Msafiri Msuya.


Kamanda wa Polisi Mkoani wa Arusha, Jonathan Shanna,  ameeleza vyombo vya habari kuwa jambazi huyo alifanikiwa kupora kiasi cha shilingi milioni sita, kompyuta mpakato (laptop) na bastola aina ya Browning ikiwa na risasi tisa zilizokuwa kwenye beg, i mali ya Msafiri Msuya.


“Baada ya kupata taarifa hiyo jeshi la polisi kupitia askari wenye weledi tulifanya msako mkali na ndani ya saa 48 tulifanikiwa kumtia mbaroni mhusika pamoja na vitu alivyopora,” alisema Kamanda Shanna.

Inaelezwa kuwa mtuhumiwa huyo wa ujambazi miaka ya nyuma aliwahi kukimbilia bungeni kwa nia ya kujisalimisha baada ya polisi kumsaka kutokana na matukio mbalimbali ya uhalifu aliyokuwa akifanya  jijini Arusha. Alikiri makosa na kuapa kutorejea tena kufanya vitendo hivyo huku akijiingiza katika CCM kama kivuli cha kuficha maovu yake.

Hata hivyo,  mara kadhaa amekuwa akikamatwa akihusishwa na matukio ya uporaji na kufikishwa katika vituo vya polisi na baadaye kuachiwa na kuonekana mtaani akidai kuwa amestaafu ujambazi.

Jumanne Mjuzi amekuwa kada maarufu wa CCM na alishiriki kwenye chaguzi mbalimbali za marudio kama kiongozi wa kikosi maalum cha ulinzi,  aliyekuwa akihusishwa kwa madai ya kuwakata mapanga wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusababisha baadhi yao kupata ulemavu wa kudumu.

Comments

Popular Posts