TBL yatupiwa tuhuma nzito, yaburuzwa kortini
Dar es Salaam. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inadaiwa kuvunja mfuko wa hisa wa wafanyakazi wake kinyemela na kufuja mabilioni ya fedha ikiwamo kuwagawia watu wanaodaiwa kuwa si wanufaika huku baadhi ya wanufaika halali wakitengwa.
Tuhuma hizo zimetolewa mahakamani na makundi mawili ya wafanyakazi wa zamani wa TBL wanaodai ni miongoni mwa wanufaika wa mfuko huo ulioanzishwa mwaka 1998 dhidi ya kampuni hiyo na wadhamini wa mfuko huo.
Kesi hiyo namba 256 ya mwaka 2017 imefunguliwa na watu watano; Oscar Shelukindo na wenzake wanne dhidi ya TBL na wadhamini wa mfuko wa umiliki hisa wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, hisa zilizotengwa kwa ajili ya wafanyakazi hao kwenye mfuko huo zilikuwa ni 5,898,596 sawa na asilimia mbili ya hisa za TBL ambazo hadi 2017 thamani yake kiwango cha chini ilikuwa Sh83 bilioni.
Mbali na Shelukindo na wenzake, watu wengine saba wakiongozwa na Daniel Shalua nao kupitia maombi namba 96 ya mwaka 2018 wanaomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo.
Makundi hayo yote mawili yamekwenda mahakamani baada ya taarifa za menejimenti ya TBL kutangaza kuuvunja mfuko huo na kugawa fedha zilizokuwamo huku walalamikaji wakidai kutengwa.
Wote wanadai kuwa, licha ya kwamba kwa sasa si wafanyakazi wa TBL lakini kwa mujibu wa mkataba na kanuni za uanzishwaji wa mfuko huo bado ni washiriki na wanufaika hivyo wana haki za kunufaika na mazao ya mfuko huo.
TBL iliwasilisha maombi namba 68 ya mwaka 2018 mahakamani hapo ikiomba suala hilo liende kwenye usuluhisi.
Hata hivyo kundi la kina Shalua linapinga maombi hayo, wakidai kuwa kuna vitendo vya jinai vilivyofanywa na wadaiwa katika mfuko huo .
Comments
Post a Comment