Simulizi muumini aliyeunguzwa moto akitolewa pepo kanisani
Serengeti. Wakati mchungaji anayedaiwa kumchoma moto muumini kwa lengo la kumuondolea mapepo akishikiliwa na polisi, baadhi ya waumini walioshuhudia tukio hilo wameeleza walivyomuokoa mwenzao.
Anna Butake, mchungaji wa kanisa la Calvary Assembly Of God(CAG) lililopo kijiji cha Musati wilayani Serengeti ndiye anayedaiwa kumchoma moto muumini huyo, Philipo Elias.
Elias (22), mkazi wa Kakonko mkoani Kigoma kwa sasa anafanya kazi ya kuchunga mifugo katika kijiji cha Musati. Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali Teule ya Nyerere mjini hapa kwa ajili ya matibabu.
Mchungaji Anna anadaiwa kumchoma moto wakati anachoma nguo za muumini huyo zilizodaiwa kuwa na mapepo na mizimu, tukio lilitokea Aprili 28, mchana wakati wa ibada ya kuombea wenye mapepo na kuteketeza zana za uchawi.
Sophia Bogomba (44), mwalimu wa watoto kanisani hapo, alisema Elias alikuwa na nguo ya ndani na fulana ambazo zina zindiko na zilimwagiwa mafuta ya taa kwa ajili ya kuteketezwa. “Aliambiwa awashe moto, aliwasha njiti tano zote zikazimika, lakini ya sita ikawaka kidogo na baada ya muda moto ukalipuka na yeye akaanza kuungua,” alisema.
Sophia alisema waumini waliogopa mlipuko uliotokea na kuungua kwa kijana huyo, hata hivyo walifanikiwa kumuokoa kwa kumumwagia mchanga wa ujenzi uliopo nje ya kanisa.
Mwenyekiti wa wanawake wa kanisa, Modesta Jeremia (58), aliliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa kijana huyo kabla ya kuteketezwa kwa nguo zake alitoa ushuhuda kuwa ana mizimu.
Alisema mchungaji alimhakikishia kuwa zitaungua na kumwambia aziweke chini ili achome, na baada ya kuwasha kiberiti moto ulilipuka na shati lake likaanza kuungua.
Modesta alisema walipambana kumuokoa kijana huyo lakini hakutaka kuvua shati ambalo lilikuwa linaungua.
Katika mahojiano na Mwananchi, Elias alisema alikwenda kanisani kuombewa ili apone maumivu ya kichwa, lakini aliambulia kuchomwa moto.
Hata hivyo, mchungaji Anna alisema kuwa yeye alichoma nguo alizokuwa amepeleka majeruhi huyo baada ya kubainika kuwa zina maagano na mapepo, lakini alishangaa hazikuungua badala yake aliungua Elias.
Alisema kijana huyo alikuwa na nguvu za giza.
Mkinzano wa kauli
Wakati mchungaji Anna akidai kuwa alimshikisha nguo muumini huyo wakati wa kuzichoma ili kuachana na maagano yake, baadhi ya maelezo ya waamini waliokuwepo wakati wa tukio yanakinzana naye.
Zakaria Mugendi, mmoja wa waumini wanaomsaidia kutoa huduma katika kanisa hilo alisema Elias alijiunguza mwenyewe.
“Baada ya kuchoma nguo mbili chupi na tisheti ambazo alidai zina maagano ya kichawi, alizibeba na kuweka kifuani kisha akakimbia wakati huo moto ukaanza kumuunguza,”alisema.
Alisema kuwa walilazimika kumfukuza na kumnyang’anya nguo hizo wakati zinawaka na nguo alizokuwa amevaa zikawa zimeshika moto.
Mugendi alisema walimrudisha kijana huyo kanisani na kuomba aende nyumbani kwao.
Hata hivyo, kwa kugugumia, Elias alisema yeye siyo mchawi kama wanavyodai na hakuwasha moto, bali aliambiwa afumbe macho aombewe na akashtukia kuwa alianza kuungua kwa madai kuwa nguo zake zina mapepo.
Polisi wamng’ang’ania
Kamanda wa Polisi wilayani Serengeti, Mathew Mgema alisema wanamshikilia mchungaji Anna tangu Aprili 28 na kwamba, wanategemea kumfikisha mahakamani. Chini ya mchungaji Anna, kanisa hilo limeongezeka tangu 2010 lilipoanzishwa limekuwa likiongeza waumini kila uchao.
Akizungumzia hali ya majeruhi huyo, muuguzi wa zamu katika wodi ya wanaume Hospitali Teule ya Nyerere, John Nyang’ombe alisema inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.
Comments
Post a Comment