MAUAJI YA MWANAFUNZI SCOLASTICA: Mahakama yahamia eneo analodaiwa kuuawa
Washitakiwa wa kesi hiyo ni mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha; mmiliki wa shule, Edward Shayo na mwalimu wa zamu, Laban Nabiswa ambao wamekana shitaka hilo.
Mahakama ilihamia eneo hilo ili kuwawezesha shahidi wa 18, Jackson Kileo na shahidi wa 19, Inspekta Waziri Tenga ili wakaonyeshe baadhi ya maeneo ya tukio hilo yaliyomo katika ushahidi wao.
Akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu Joseph Pande, Inspekta Tenga alionyesha sehemu ambayo inadaiwa Chacha alimuonyesha sehemu wanayovuka na eneo ambalo mshitakiwa alijificha.
Pia, aliionyesha mahakama eneo ambalo mshtakiwa Chacha alimulika tochi na baadaye kumkimbiza mtu aliyeruka ukuta hadi eneo ambalo mwanafunzi huyo anadaiwa kuanguka.
Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana, shahidi wa 18 Jackson Kileo aliiongoza mahakama hadi eneo la mto Ghona ambalo alisema ndipo aliuona mwili huo, Novemba 10.
Juzi alasiri, shahidi huyo wa 19 Inspekta Tenga aliyesimamia upelelezi wa shauri hilo, alieleza hatua kwa hatua tangu walipoanza uchunguzi hadi washitakiwa walivyokamatwa.
Taarifa za awali kwa mujibu wa shahidi huyo, zilionyesha kutoonekana kwa Humphrey tangu usiku wa Novemba 6, 2017 na taarifa za kutoonekana zilitolewa taarifa polisi na mshitakiwa Laban Nabiswa.
Shahidi huyo alieleza taarifa ya kutoonekana kwa mwanafunzi huyo iliripotiwa polisi Himo Novemba 10, 2017 ikipishana kwa muda wa nusu saa tu na taarifa ya mwili wa mtu kuonekana mtoni.
Alidai kuwa Novemba 14, 2017 walifika shuleni Scolastica ambapo Chacha na Laban waliwaonyesha eneo ambalo walidai wanafunzi hulitumia kutorokea kutoka shule. Shahidi huyo alidai siku hiyo Chacha aliwaeleza kuwa usiku wa Novemba 6, 2017 alimkimbiza kibaka aliyeruka kutoka ndani ya ukuta wa shule, wakati huo yeye akiwa amejificha eneo hilo.
Kwa mujibu wa Inspekta Tenga, mshitakiwa aliwaeleza alipopiga tochi alimwona mtu amevaa bukta, fulana na soksi akikimbilia maeneo ya kijijini akiruka kutoka uzio wa ukuta wa shule hiyo.
Baada ya kumaliza kuzungumza na uongozi wa shule na washitakiwa Chacha na Laban, walirudi mjini Moshi, lakini katika siku iliyofuata walirudi Himo na kwenda hadi eneo ambalo mwili uliokotwa.
Shahidi huyo kuwa kwa kuwa kulikuwa na taarifa za kukinzana kuhusu tukio hilo, walifuatilia kuangalia namna ya kujiridhisha na mwili uliozikwa na ulipofukuliwa Novemba 17, 2017 ulibainika ni wa Humphrey.
Wakati upelelezi ukiendelea, shahidi huyo alisema waliiandikia barua kampuni ya Vodacom ili wawapatie kumbukumbu za mawasiliano ya simu za washitakiwa kati ya Novemba 6 na 20, 2017.
Aprili 2018 walipewa majibu hayo na baada ya kupokea, alizifanyia simu hizo uchambuzi ili kuona kilichopo kwenye maelezo hayo ya kukiri kosa ya Chacha kama vinaenda pamoja.
Alifafanua Chacha katika maelezo yake ya ungamo alieleza Novemba 6, 2017 saa 2:30 alimkimbiza mtu aliyeruka kutokea ndani ya shule na mbele kidogo alidondoka na kupasuka kichwa.
Inspekta Tenga alieleza Chacha katika maelezo hayo alisema baada ya kudondoka na kupasuka kichwa na kuvuja damu na aliendelea kumpiga kwa bapa la upanga hadi akatulia.
Baadaye alifanya mawasiliano na Laban na baadaye mmiliki wa shule ambaye ni mshitakiwa wa pili ambaye anadaiwa kutoa maelekezo mwili wa mtu huyo utupwe katika mto Ghona.
Inspekta Tenga alidai uchambuzi alioufanya kwenye taarifa ya Vodacom, alibaini kulikuwa na mawasiliano ya simu katika muda alioutaja Chacha kutokana na tarehe na mnara mmoja uliotumika.
Alieleza Chacha akitumia simu yake aliyoisajili kwa jina la Bhoke, siku hiyo saa 3:07 simu yake ilipiga kwenda namba ya Shayo na waliongea kwa sekunde 8, mnara ulisomeka Makuyuni.
Shahidi huyo alieleza siku hiyohiyo saa 3:05 simu hiyo ilipiga kwenda kwa Laban ikitumia mnara wa Makuyuni kwamba saa 3:09 usiku namba hiyo ilizungumza kwa sekunde 52.
Taarifa hiyo ya Vodacom kwa mujibu wa Tenga, ilionyesha kuwa siku hiyo hiyo ya tukio saa 4:41, mshikiwa Chacha alimpigia simu mshitakiwa Shayo na walizungumza kwa sekunde 36.
Comments
Post a Comment