Magufuli ataka Sh3 bilioni zilipe wananchi fidia Kasumulo
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza Sh3 bilioni zitengwe kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa upanuzi wa kituo kikubwa cha Kasumulo mpakani mwa Tanzania na Malawi mkoani Mbeya.
Rais Magufuli ameagiza fidia hiyo ianze kulipwa kesho Mei Mosi ili ujenzi huo uanze mara moja.
Ametoa agizo hilo leo Jumanne Aprili 30 katika viwanja vya Mwakangale wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya siku nane inayoendelea mkoani Mbeya.
Amesema lazima kituo hicho kikubwa cha Kasumulo kijengwe na tayari Serikali imeshapata fedha kutoka Benki ya Dunia huku akiagiza wahusika kusaini mkataba haraka ili kazi ianze mara moja.
Hata hivyo ameonya kuwa wapo watakaolipwa fidia na wengine wasiostahili hawatalipwa.
“Niwaeleze ukweli waliopo ndani ya mita 22.5 kila upande wa barabara wale hawastaili kulipwa fidia, tumegusa watu na mashamba yao na maeneo yao watalipwa Sh bilioni 3. Katibu mkuu muanze kuwalipa watu kesho.”
Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kushughulika na mundombinu mikubwa ambayo inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini.
Comments
Post a Comment