Magufuli apokelewa kwa mabango ya kero za wananchi
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza viongozi kote nchini kuhakikisha wanapanga utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na kuwatembelea wanaowaongoza ili kutatua migogoro mbalimbali inayowakabili.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 30 baada ya kupokewa na mabango katika mkutano wake wa hadhara unaofanyika katika Chuo cha Ualimu Mpuguso wilayani Rungwe.
Baadhi ya wananchi walijitokeza wakiwa na mabango yanayoeleza kero mbalimbali zinazowakabili na polisi walijaribu kuwazuia wasiyaonyeshe lakini mkuu huyo wa nchi aliwataka wawaacha ili ayasome yote.
“Waacheni waonyeshe mabango yao. Haya mabango yanayotolewa ni kwa sababu ya kero ambazo hazijatatuliwa, mngekuwa mnatekeleza vizuri majukumu yenu yasingekuwapo, wananchi hawa wametaka niyaone ili nijue kero zao, nawataka viongozi wenzangu, viongozi wa CCM muwe myasome haya mabango nikiondoka mkatatue kero zao.”
“Mwananchi akatafute karatasi, wino aanze kuandika tu mnadhani kwa sababu gani, Rungwe oyeee, mabango oyeee, wananchi oyeee. Yupo mwenye bango?, nimeyaona na vyombo vyangu vimeyasoma na nitayafanyia kazi,” alisema Rais Magufuli.
Miongoni mwa watu waliotoa kero zao ni Diana Jacob ambaye alisema” “Nilimaliza darasa la saba mwaka 2017, naomba msaada wa masomo,” kufuatia ombi hilo, Rais Magufuli amesema:
“Shida kama hii ya shule si lazima Rais aje aitatue kuna Katibu tarafa na hao wazazi wako kawaambie walime hilo ndilo jibu langu, angesema ni walemavu hilo lingekuwa suala jingine, kuna masuala ya msingi na wanasema asiyefanya kazi asile na asipokula kwa maana yake afe, nataka mambo yanayohusu watu wengi kwa maana yameshindikana ngazi za chini.”
Comments
Post a Comment