CAG mstaafu awashauri wasioridhishwa na CAG Assad



Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amewashauri watu ambao hawajaridhishwa na Ripoti ya CAG, Profesa Mussa Assad kufuata utaratibu uliowekwa kikatiba na kisheria wa kuipinga ripoti hiyo.

Utouh amesema kuwa Katiba inaelekeza mtu anayepinga ripoti ya CAG kuwasilisha malalamiko yake Mahakama Kuu.

 “Mahakama Kuu ndio itachunguza kuona kama ukaguzi wa CAG pamoja na ukamilifu wake umefanywa kwa utaratibu unaokamilika,” Mwananchi linamkariri Utoh.


Kauli hiyo imekuja wakati ambapo kumetokea mgongano wa kimtazamo kuhusu ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni, ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alilieleza Bunge kuwa ripoti ya CAG haikusema ukweli kuhusu kutonunuliwa kwa sare za jeshi la polisi.

Hatua hiyo ilizua mijadala hasa baada ya Waziri Lugola kueleza kuwa sare zinazodaiwa kuwa hazipo amezishuhudia kwenye ‘magodauni’ ya jeshi hilo hivyo alisema CAG ni muongo.

CAG katika ripoti yake ya Mwaka Wa Fedha 2017/18, alisema hakukuwa na ushahidi wa manunuzi ya sare za jeshi hilo zilizogharimu Sh 16.6 bilioni. Alisema malipo ya fedha hizo yalifanyika lakini hakuna ushahidi wa kihasibu uliowasilishwa wakati wa ukaguzi.

Lugola aliweka kiapo akipinga maelezo hayo ya CAG, na aliahidi kuvua nguo endapo itathibitika kuwa alichokisema yeye sio cha kweli. 

Comments

Popular Posts