Rais Magufuli Kuanza Ziara Ya Kikazi Mkoani Mtwara.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Dkt.John Pombe Magufuli, anatarajia kufanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kuanzia 02 April hadi April 04, Mwaka huu wa 2019 .

Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi 30 Machi 2019, mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema katika ziara hiyo Rais Magufuli atazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara na lingine la ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata (Km 50),pia ataweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin kilichopo Msijute na ataweka pia jiwe la msingi katika chuo cha ualimu cha Kitangali.

Mh.Byakanwa amesema licha ya kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali, Rais Magufuli atazindua kituo cha afya cha Mbonde wilayani Masasi na barabara ya Mangaka-Mtambaswala na pia Mangaka -Nakapanya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

"Miradi inayozinduliwa ni mikubwa ambayo itasaidia kuchochea kukua kwa uchumi wa Mtwara na kwa uchumi wa Mtwara na nchi kwa ujumla na pia ni miradi ambayo kwa Mtwara ina tija kubwa sana, hivyo amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika maeneo yote yenye miradi ya maendeleo itakayozinduliwa ili kumsikiliza Mh.Rais" amesema   Mkuu wa mkoa huyo wa Mtwara.

Hii ni ziara ya pili kwa Rais Magufuli kutembelea Mkoa wa Mtwara tangu alipoapishwa kuwa Rais mwaka 2015, ambapo safari hii anatarajia kuzunguka katika wilaya zote za Mkoa huu. 

Comments

Popular Posts