Serikali Yashikilia Msimamo wake Kuhusu Mgodi wa North Mara
Serikali kupitia Wizara ya Madini imesema bado imeshikilia msimamo wake kuhusu muda uliotolewa kwa Mgodi wa North Mara kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa kwenye kikao cha Januari 9, 2019 kuhusu Bwawa la kuhifadhi topesumu (Tailings Storage Facility -TSF).
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila Februari 26, 2019 wakati akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake Jijini Dodoma, mara baada ya kufungua kikao cha pamoja baina ya wajumbe kutoka serikalini na wajumbe kutoka Mgodi wa North Mara waliokutana kujadili kuhusu hatua zilizofikwa na Mgodi katika kutekeleza maagizo hayo.
Amesema serikali haitoongeza muda zaidi ya ule uliotolewa katika kikao cha awali, na kusema kuwa msimamo wa serikali utabaki kuwa hivyo.
“Ndugu zangu katika kikao hiki kilenge kutoa majibu ya utekelezaji wa maagizo ya serikali kama yalivyowasilishwa kwenye kikao cha Januari 9, 2019, ni kwa kiasi gani mmetekeleza maagizo hayo,” alisema Prof. Msanjila.
Serikali kupitia kikao chake cha Januari 9, 2019 chini ya Makatibu Wakuu wa wizara saba (Madini, Makamu wa Rais Mazingira (NEMC), Ardhi, TAMISEMI, Afya, Fedha na Maji) kilitoa maagizo mbalimbali yakiwemo: Kujenga TFS mpya na Kukarabati TFS iliyopo kwa aajili ya kudhibiti mtiririko wa topesumu, maagizo ambayo mgodi ulipewa kuyatekeleza kwa muda wa miezi Nane (8) kuanzia Januari 9, 2019.
Akiongoza wakati wa mjadala wa uwasilishaji wa mada mbalimbali wa kikao hicho, chini ya Mwenyekiti wa kikao hicho Prof. Hudson Nkotaga aliwataka North Mara kueleza namna gani wametekeleza maagizo ya serikali kwa lengo la kupata mrejesho wa utekelezaji.
Kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo, Meneja Usalama, Afya na Mazingira Reuben Ngusaru, kutoka mgodi wa North Mara amesema mgodi umeanza kutekeleza maagizo hayo na bado wanaendelea kutekeleza maagizo hayo na hata kikao cha tarehe 26 Februari ikiwa ni moja mkakati wa kutekeleza maagizo hayo kwa ufanisi.
Akizungumzia kuhusu hatua zilizochukuliwa na mgodi kudhibiti uvujaji unaoendelea kwenye (TSF) mpaka kufikia siku ya kikao cha Februari 26, mambo yaliyotekelezwa ni pamoja na: Kuondoa mawe na kusafisha mtaro uliopo upande wa Kaskazini mwa TSF. Kuvukiza (evaporation) maji yaliyotokana na uchenjuaji wa mawe yanayotengeneza tindikali asili (PAF Rock) (leachate water) badala ya kuyapeleka yote kwenye TSF na Programu zote zilizokuwepo za kupunguza maji katika TSF bado zinaendelea.
Aidha, kuhusu utekelezaji uliofikiwa katika kutekeleza agizo la Serikali la kujenga TSF mpya (Construction of a new TSF) Reuben amesema mpaka kufika tarehe 26 Februari, mgodi umefanya utambuzi wa eneo linalofaa kwa ajili ya ujenzi wa TSF mpya (Site Identification) nau sanifu wa awali (Conceptual design) ambapo usanifu wa awali umefanyika na ujenzi wa TSF mpya unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani milioni 45 za tope sumu (tailings) kavu kwa kadirio la ongezeko la tani 8200 kwa siku.
Maagizo ya serikali kwa mgodi wa North Mara yalitokana na ukaguzi uliofanywa na serikali kwenye mgodi huo uliohusisha timu kutoka ofisi mbalimbali za serikali zikiwemo, NEMC, Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, na Wizara ya Afya, uliopelekea kutolewa kwa maagizo yaliyolenga kudhibiti uharibifu wa mazingira uliokuwa unafanywa na mgodi.
Comments
Post a Comment