Upelelezi wa kesi ya kughushi saini ya Waziri January Makamba Bado Haujakamilika



Upelelezi wa kesi ya kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba inayowakabili  maofisa sita wa  Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), bado haujakamilika.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh160 milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 81/2018, iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Jenipher Masue ameeleza hayo, jana, Jumatano Januari 30, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Magori Wambura (38) ambaye ni ofisa mazingira, hakuwepo mahakamani hapo wakati shauri hilo linatajwa.

Wakili Masue alidai kuwa taarifa aliyopewa na magereza ni kwamba, Wambura alipelekwa Mahakama Kuu, kwa sababu wana kesi nyingine.

Hakimu Mmbando baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 13, mwaka huu itakapotajwa.

Washtakiwa watano wapo nje kwa dhamana baada ya kupata kibali cha dhamana kutoka Mahakama Kuu, huku mshtakiwa Wambura akiendelea kusota rumande baada ya kushindwa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.

                    KWA HABARI ZA MICHEZO PAKUA APP YETU YA MICHEZO SASA
 

Comments

Popular Posts