Waziri Kalemani Awanyooshea Kidole VISHOKA
Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ametoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme pamoja na vishoka.
Waziri Kalemani alitoa kauli juzi akiwa katika ziara wilayani Kwimba, Mwanza na kuzungumza kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Ngulla na Ibindo, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, kuwasha umeme na kuzungumza na wananchi.
“Mtu atakayebainika akikata nguzo, akiiba nyaya, akichezea transfoma kiasi cha kukosesha umeme wananchi, Mkuu wa Wilaya wa eneo husika atamweka korokoroni,” alisema.
Aidha, alisema kwa wale vishoka, wanaounganisha umeme kwenye nyumba za wananchi bila kuwa na taaluma hiyo, vilevile watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Ikitokea tumekukamata, hatutajali wewe ni kibarua wa mkandarasi anayetekeleza miradi yetu ya umeme sehemu yoyote, utakamatwa na kuwekwa ndani,” alisisitiza Waziri.
Waziri Kalemani aliwaasa wananchi kuendelea kuwa makini kwa kujiepusha kuwatumia vishoka kwa kazi ya kufunga nyaya za umeme katika nyumba zao.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kuutumia umeme kwa kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa ili uwe na tija kwao na taifa kwa ujumla.
Naye Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa, pamoja na kuishukuru serikali kwa kuwapelekea wananchi wa jimbo lake umeme; aliwahamasisha kujitokeza kwa wingi kulipia, ili waunganishiwe huduma hiyo.
“Umeme huu unapokuja unahitaji watumiaji na watumiaji ni ninyi. Gharama za kupeleka umeme ni kubwa. Ni vizuri muwe mnajitokeza kwa wingi kuwasilisha maombi Tanesco, ili muunganishiwe na kuanza kuutumia kuboresha maisha yenu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga aliipongeza serikali kuwapelekea wananchi umeme na kuomba vijiji vichache ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo vipelekewe, ili nao wautumie katika shughuli za kujiongezea kipato na kuboresha hali zao za maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya TANESCO, Wilaya ya Kwimba ina jumla ya vijiji 119 ambapo mpaka kufikia Julai 2020, vijiji 78 vitakuwa vimepatiwa umeme, sawa na asilimia 66 ya vijiji vyote vya wilaya hiyo.
Comments
Post a Comment