WANANCHI WAMETAKIWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA NA KUZINGATIA LISHE BORA.
Watanzania kote nchini wametakiwa kufuata kanuni na taratibu bora za maisha ikiwemo kubadili mfumo wa maisha ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na udumavu kwa watoto wachanga.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika Wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida wakati alipotembelea kituo cha afya na kuongea na wananchi.
“Serikali chini ya uongozi wa Rais Magufuli inataka kila mtanzania awe na afya bora, ndo maana tunajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kutunza afya zenu ikiwemo kufanya mazoezi na kuepuka vyakula ambavyo si salama kwa afya zetu pamoja na kubadili mfumo mzima wa maisha”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha,Naibu waziri huyo ameendelea kusisitiza kwa upande wa akina mama walio na watoto wadogo chini ya miaka miwili kuendelea kuwanyonyesha na kuwapa vyakula vyenye lishe bora watoto wao ikiwa ni sehemu ya kumsaidia mtoto kukua kiakili na kuwa na afya bora huku akisisitiza siku 1000 za mwanzo kwa mtoto ndizo siku muhimu katika kumuwezesha kuwa na afya bora na kukua vizuri.
“Siku 1000 za mwanzo tunaanza kuzihesabu toka mimba inapotungwa, anapozaliwa na kufikisha miaka miwili, hiki ni kipindi muhimu sana cha mama kumnyonyesha mtoto ikiwa ni pamoja na kumpa vyakula vyenye lishe ili mtoto aweze kuwa na afya bora na ubongo unaofanya kazi sawa sawa”. Alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile amekipongeza kituo cha afya cha Kinyambuli kwa kuzitendea haki fedha zilizotolewa na Serikali Shilingi milioni 400 ili kusaidia kupanua kituo hicho kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi.
“Nawapongeza sana wananchi wa Kinyambuli kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo hiki, ninachokiona hapa kipo mara 300 nchi nzima, kwa kweli mnastahili pongezi na fedha za serikali tulizoleta milioni 400 mmezitendea haki”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Hata hivyo Dkt.Ndugulile amesema serikali bado ina nia kubwa ya kuboresha hali ya utoaji huduma za afya nchini, huku ujenzi wa Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama ukitarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Dkt. Ndugulile amesema mkoa wa Singida umetengewa bajeti ya Bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama pamoja na Singida DC.
Kwa upande wake diwani wa Kinyambuli, Rubeni Charles ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo kikubwa cha afya.
“Kwakweli naishukuru sana serikali kwa kutukumbuka, wananchi wa kijiji hiki walikua wanapata shida sana kupata huduma za afya hasa wakinamama wajawazito ambao tulipoteza wengi kutokana na kukosa huduma hii muhimu”. Alisema Rubeni.
Comments
Post a Comment