Waziri Mkuu Ataka Wachimbaji Wadogo Waende Benki Wakakope Mitaji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo wa madini waende Benki wakakope mitaji kwa sababu wana uhakika wa kudhaminiwa na Benki Kuu.
“Msihofu kukopa, kukopa ni jambo la kawaida sana. Nenda mkakope ili mpate mitaji ya kununua mitambo ya kuchenjua dhahabu na madini mengine,” amesema.
Ametoa wito jana (Jumapili, Septemba 30, 2018) wakati akifunga maonesho ya mkoa wa Geita ya dhahabu, madini, teknolojia ya madni na uwekezaji yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kalangalala, mjini Geita. Maonesho hayo yalianza Septemba 24, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema, wakati akikagua mabanda ya maonesho kwenye viwanja hivyo, ameelezwa kwamba gharama ya mtambo unaohitajika kwa wachimbaji wa kati inafikia sh. milioni 10. “Naomba niwaeleze wanaGeita kwamba mnakopesheka, nendeni mkaombe mikopo ili mnunue mitambo ya kuchenjua dhahabu,” amesisitiza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaeleza wana-Geita kwamba siri kubwa ya kufanikiwa kupata mikopo ni kwa wao kuunganisha nguvu kwa kujiunga kwenye vikundi ili wawe na malighafi ya kutosha mitambo hiyo.
“Wakuu wa wilaya za Mkoa huu simamieni zoezi hili kwa sababu wilaya zenu zote zinachimba madini. Simamieni uundaji wa vikundi na mwende mkawasemee benki pale wanapokwama.”
Akielezea kuhusu makusanyo ya fedha kutokana na mauzo ya dhahabu kwenye mkoa huo, Waziri Mkuu amesema tangu Aprili mwaka huu, mapato yanayotokana na madini yameongezeka kutoka sh. milioni 400 na kufikia sh. milioni 850 Agosti, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wazazi wawapeleke watoto wao kwenye vyuo vya ufundi vya VETA ili wakajifunze taaluma ya uchongaji wa madini na vito kama eneo jipya la ajira nchini.
“Nimemuona binti mmojakwenye banda la VETA akielezea vizuri kuhusu uchongaji wa madini na vito. Nikabaini kumbe jambo hili linaweza kufanyika hapa nchini kwetu. Ninawasihi Wazazi pelekeni watoto wenu kwenye vyuo vya VETA vya Mwanza, Geita na Moshi ambako kozi hii inafundishwa,” amesisitiza.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria maonesho hayo, Waziri wa Madini, Bibi Angella Kairuki alisema sekta ya madini ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 4.8 tu, licha ya kuwa sekta hiyo iliongoza kwa kuingiza fedha za kigeni kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya nchi katika mwaka 2016/2017.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Alisema zaidi ya asilimia 90 ya thamani ya madini yanayouzwa nje ya nchi ni dhahabu na kwamba mkoa wa Geita unaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu ambapo katika mwaka 2017, asilimia 41.2 ya dhahabu iliyouzwa ilitoka kwenye mkoa huo.
“Kwa upande wa wachimbaji wadogo wanaozalisha dhahabu, mkoa wa Geita unaongoza ambapo tani 1.175 za dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 89 zilizalishwa, na kati ya hizo, asilimia 49 ilizalishwa na wachimbaji wadogo,” alisema.
Alisema takwimu hizo zilipatikana kabla Serikali haijachukua hatua ya kuzuia usafirishaji wa carbon yenye dhahabu kuvuka mipaka ya mkoa, hali iliyokuwa inachangia utoroshaji, ukwepaji wa kodi na jamii husika kushindwa kunufaika na madini yayiyopo kwenye maeneo yao.
Maonesho hayo yamekutanisha makampuni 250 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na yataendelea hadi Jumatano jioni, Oktoba 3, 2018 kutokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel kwa Waziri Mkuu ili wananchi wa mkoa wake wapate fursa zaidi ya kujifunza masuala ya madini, uwekezaji na matumizi ya teknolojia sahihi zinazozingatia utunzaji wa mazingira.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini, inasema: “Teknolojia bora ya uzalishaji dhahabu kwa maendeleo ya kijamii na uchumi wa viwanda”.
Comments
Post a Comment