Mbio za Urais Zanzibar Zaibua Halmashauri Kuu Ya CCM.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) kimetoa kalipio la mwisho kwa wanachama wa chama hicho wanaokiuka katiba,kanuni ya uchaguzi na ya uongozi na maadili kwa kuanza kufanya kampeni za kificho na za wazi za urais wa Zanzibar.
Kalipio hilo la kwanza kwa NEC lilitolewa jana katika kikao chake kilichoketi jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humphrey Polepole ilisisitiza kuwa; “Kufanya hivyo ni kwenda kinyume na utamaduni na desturi njema za chama ambazo kwa pamoja zinatuongoza kuwapata viongozi wa CCM na serikali zake,”.
Onyo hilo limetolewa ikiwa imebaki miaka miwili kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo rais aliyepo madarakani kwa sasa Dkt Ally Mohammed Shein atakuwa amemaliza muda wake baada ya kuongoza Kisiwa hicho kipindi cha miaka kumi na kwa mujibu wa Katiba hataruhusiwa kugombea.
Kwa mantiki hiyo ni jambo la kawaida kwa wanasiasa kuanza kujipanga au kupanga safu zao na mara nyingi uchaguzi kama huo huambatana na vikumbo vingi vya kisiasa kwa kila kambi kuhakikisha wanayemuunga mkono anasimamishwa kugombea urais.
Hii si mara ya kwanza kwa CCM kutoa onyo kwa watu ambao wameanza harakati za kuusaka urais Zanzibar.
Agosti 18 mwaka huu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt Bashiru Ally akiwa visiwani humo alitumia neno ‘wakome’ kuwaonya wana- CCM walioanza kampeni za wazi na kificho kuusaka ukuu huo wa dola.
Dkt Bashiru alisema amesikia wapo watu ambao wengine wana vyeo na wengine hawana wana ndoto ya kushika madaraka ya urais Zanzibar na kuwataarifu kuwa nafasi hiyo bado haijatangazwa kama ipo wazi.
“Nafasi ya urais Zanzibar haijatangazwa kuwa ipo wazi bado ina mwenyewe na kutakuwa na utaratibu wa kuijaza,utaratibu huo utasimamiwa na chama sio makundi hayo mnayoyapitisha pitisha mara kwenye hoteli mara kwenye ofisi za serikali komeni tabia hiyo acheni,” alisema Dkt Bashiru.
Dkt Bashiru alisema CCM sio chama cha kusaka vyeo bali ni chama cha Mapinduzi na kwamba wataendelea kuwafuatilia wasaka vyeo kwa kuwa wengine wanawajua na siku zao zinahesabiwa.
Dkt Bashiru aliwataka watu hao wamuache Dkt Shein amalize kipindi chake kwa heshima na wakati ukifika chama hicho kitasema na kuweka utaratibu wa kumpata mtu atakayejaza nafasi hiyo.
Mbali na Dkt Bashiru kiongozi mwingine aliyetoa onyo hilo ni Rais Dkt Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea mashina ya chama hicho katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Dkt Shein aliwaonya baadhi ya watu wanaofanya kampeni za kusaka urais wa Zanzibar kabla ya muda wa kufanya hivyo kufika na kusisitiza kuwa yeye bado ni Rais wa Zanzibar.
Dkt Shein alisema kuna baadhi ya viongozi wa chama na serikali tayari wameanza kupanga timu za urais badala ya kushughulika na mambo ya msingi ya kufanya shughuli za chama zitakazofanikisha kuiweka serikali madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nafasi ya urais ndani ya CCM haipatikani kwa kampeni na makundi yasiyo halali bali kwa utaratibu maalumu kupitia vikao vya kikatiba ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba na miongozo na kanuni mbali mbali za CCM,” alisema Dkt Shein.
Dkt Shein pia aliwatahadharisha kuwa watu hao wasipoacha tabia hiyo na kuvumilia hadi 2020, atawachukulia hatua kali za kinidhamu zikiwemo kufikishwa katika vikao vya usalama na maadili vya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ili wahojiwe na kuchunguzwa dhidi ya mwenendo wao usiokuwa na manufaa kwa CCM.
Bado haijajulikana kama katika kikao cha jana Dkt Shein alifikisha malalamiko hayo rasmi au la baada ya kuahidi kufanya hivyo.
Pamoja na hayo onyo hilo la mwisho la CCM tayari limeleta hisia tofauti tofauti ndani na nje ya chama hicho kwani wapo ambao wanaona kwamba endapo wahusika hawatasikia, huenda baadhi ya viongozi na watu walioteuliwa kushika madaraka fulani fulani wakaondolewa kutokana na ama wenyewe au makundi yao kuwa miongoni mwa yale yanayotajwa kuanza harakati za kuusaka urais wa Zanzibar.
Mbali masuala ya urais wa Zanzibar, kikao cha NEC pia kimemteua Ramadhani Hamza Chande kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi wa jimbo la Jang’ombe.
Uchaguzi wa jimbo hilo ambao utasimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) unatarajiwa kufanyika Oktoba 27 baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Abdalla Maulid Diwani kuvuliwa uanachama wa CCM na kupoteza sifa ya kushika nafasi hiyo.
Install Application ya CCM NEWS Uweze Pata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi
Comments
Post a Comment