Marekani yapandishwa kizimbani



Serikali ya mamlaka ya Palestina imedaiwa kuwasilisha faili la malalamiko dhidi ya Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), ikitaka kuangaliwa upya hatua ya Washington ya kuhamishia ubalozi wake nchini Israel katika mji mtukufu wa Jerusalem, kutoka Tel Aviv.
Katika taarifa iliyotolewa juzi, ICJ imethibitisha kwamba kupokea faili hilo la Palestina, inayotaka Marekani ishurutishwe kufunga ubalozi wake nchini Israel ulioko Jerusalem inayokaliwa kwa mabavu.
Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema, Wapalestina kupitia Mamlaka ya Ndani ya nchi hiyo, PA wametumia hoja kwamba, Hati ya mkataba wa Vienna ya Mwaka 1961 kuhusu Uhusiano wa Kidiplomasia imeweka wazi kuwa nchi ina haki ya kuweka ubalozi wake ndani ya mipaka ya nchi mwenyeji na kwa msingi huo, uwepo wa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem ni kukanyaga haki ya kujitawala na mipaka ya Palestina.
Itakumbukwa kuwa Disemba 6 mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake inautambua Jerusalem kuwa ni mji mkuu wa Israel na kisha kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv.
Uamuzi huo umeendelea kupingwa na jumuiya ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.
Kadhalika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio likitangaza kuwa haliitambui Jerusalem kuwa ni mji mkuu wa Israel.

        Install Application ya CCM NEWS Uweze Pata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi

Comments

Popular Posts