Wawili wafariki magari yakigongana na kuwaka moto
Chalinze. Watu wawili wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa sehemu mbalimbali baada ya magari mawili ya mizigo kugongana uso kwa uso na kisha kushika moto katika kijiji cha Mwidu kata ya Mdaula halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani leo asubuhi,
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amewataja waliofariki dunia kuwa ni Ally Kiara (40) dereva wa moja ya magari hayo na mtu mwingine ni mwanaume ambaye jina lake halijaweza kupatikana mara moja.
Nyigesa ameeleza kuwa miili ya marehemu hao imepelekwa kuhifadhiwa katika hospitali teule ya rufaa mkoa wa Pwani, Tumbi kusubiri ndugu kwa utambuzi na hatua nyingine za mazishi.
Kamanda huyo pia amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Ramadhani Idd (28) na Yasini Abdallah (24) wote wafanyabiashara na wakazi wa Dar es Salaama na wamelazwa katika kituo cha afya Chalinze kwa matibabu zaidi.
"Tunaendelea kujaribu kuzima moto eneo la tukio lakini athari za awali ni kwamba magari hayo yameharibika, vifo na majeruhi kama nilivyokueleza, tunafanya uchunguzi zaidi wa chanzo cha ajali,"amesema Kamanda Nyigesa.
Comments
Post a Comment