Vijana waondolewa kambi ya wazee Nunge, walipwa Sh100,000


Dar es Salaam. Vijana 34 wanaotakiwa kuondoka katika kambi ya wazee na wasiojiweza ya Nunge Kigamboni wameanza kulipwa Sh100,000 kila mmoja kwa ajili ya kujikimu kimaisha.
Vijana hao walitakiwa kuondoka katika kambi hiyo na mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri kwa lengo la kuwapisha wazee, kutakiwa kwenda kuanza maisha mengine uraiani.
Vijana hao yatima walilelewa kambi ya makao makuu ya Taifa ya watoto Kurasini tangu wakiwa na umri chini ya miaka mitano hadi walipofikia umri wa miaka 18, kuhamishiwa katika kambi hiyo ya wazee.
Akizungumza leo Ijumaa Agosti 31, 2018 kamishna msaidizi  wa ustawi wa jamii wa Wizara ya Afya, Rabikira Mushi amesema wameanza kuwalipa vijana hao fedha hizo za kujikimu waweze kwenda kupanga uraiani.
Mushi amesema kati ya vijana hao, 20 watapatiwa mafunzo ya mgambo kwa miezi mitatu na baadaye watatafutiwa kazi katika kampuni ya ulinzi ya Suma JKT ambapo Serikali itagharamia Sh 13 milioni kwa ajili ya mafunzo na sare zao.

Comments

Popular Posts