Mtawa azikwa, Polisi yaeleza alivyojirusha ghorofani





Bukoba/Mwanza. Mwili wa mkurugenzi wa fedha na mipango wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando, Mtawa Susan Bartholomew (48) umezikwa katika makaburi ya watawa ya Kanisa Katoliki Kashozi wilayani Bukoba, huku kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jonathan Shanna akisema alikufa baada ya kujirusha ghorofani.
jana mkuu wa kitengo cha mawasiliano Jimbo Katoliki Bukoba, Padri Deodatus Kagashe alisema mwili wa mtawa huyo uliagwa juzi jijini Mwanza na siku hiyo usiku ulipelekwa Bukoba.
Padri Kagashe hakuwa tayari kuzungumzia zaidi suala hilo na kubainisha kuwa baada ya mtawa huyo kuzikwa kwa sasa anafanya taratibu za kupokea mwili wa aliyekuwa askofu wa jimbo hilo, Nestor Timanywa ambaye atazikwa leo katika makaburi ya Kanisa la Bikira Maria. Askofu mstaafu Timanywa alifariki Agosti 28 katika Hospitali ya Bugando alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani.
Akizungumzia tetesi za kwenye mitandao kuwa huenda mtawa aliuawa, Shanna aliwataka wananchi kuacha kuamini mitandao ya kijamii kuhusu kifo hicho badala yake, waiachie polisi ifanye uchunguzi.
Shanna alisema wanaendelea na uchunguzi na hivi karibuni (bila kutaja tarehe) atatoa taarifa.
Kuhusu mtawa huyo kugawa vitu na mali zake kwa ndugu, Shanna alisema hawawezi kulizungumzia kwani linaweza kuharibu uchunguzi unaoendelea.
Juzi, Shanna alisema uchunguzi wa awali unaonyesha ofisi aliyokuwa anafanyia kazi mtawa huyo kulikuwa na tuhuma za upotevu wa zaidi ya Sh300 milioni zilizosababisha watumishi wenzake wanane kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi na baadhi yao kufukuzwa kazi.
Bugando wanena
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa, watumishi walisema kifo cha mtawa huyo ni pengo kubwa kwani alikuwa mchapa kazi na mwadilifu ila upotevu wa fedha hizo uliobainika miezi miwili iliyopita umemsababishia msongo wa mawazo.
Mtumishi mmoja alisema kabla ya kujirusha, mtawa huyo alitakiwa kukabidhi ofisi kwa sababu ya upotevu wa fedha hizo na baada ya kutekeleza agizo hilo alijirusha.
“Tulisali naye misa ya asubuhi ya saa 12:00 hapa kanisani baada ya hapo alikwenda kujirusha, hivyo inawezekana ni kutokana na msongo wa mawazo,” alisema.
Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Abel Makubi hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema ameiachia polisi.

Comments

Popular Posts