Zitto afunguka kutakiwa kuripoti polisi ndani ya siku mbili
Dar s Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema ataripoti kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ikiwa atapewa wito wa kisheria.
Ametoa kauli hiyo leo mchana Jumanne Julai 31, 2018 ikiwa ni saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kumtaka kiongozi huyo wa ACT kujisalimisha polisi kwa maelezo kuwa ametoa kauli za uchochezi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo, Lugola amesema Zitto ametoa kauli za uchochezi na kuwatukana viongozi wa Serikali wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Kilwa Kusini.
Katika mkutano huo Zitto alialikwa na mbunge wa jimbo hilo, Seleman Bungara maarufu Bwege.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter Zitto amesema, “waziri hana hayo mamlaka. Kama polisi wananitaka watoe wito wa kisheria nitakwenda.”
“Naendelea na kampeni za ubunge wa Buyungu ambapo tunamuunga mgombea wa Chadema na madiwani wa ACT- Wazalendo kwenye kata kadhaa. Nashauri waziri ampate kwanza yule mbwa wa polisi bandari."
Comments
Post a Comment