Pengo la Ndesamburo laitesa Chadema Kilimanjaro
‘Pengo halitazibika’ ni neno sahihi lililotafutwa na wahenga la kuwakumbuka wale watendao mema wakati wa uhai wao. Neno hili pia linafaa kumzungumzia Philemon Ndesamburo au ‘Ndesa Pesa’ aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro.
Mwaka umepita tangu mwasisi huyo wa Chadema afariki dunia na ni dhahiri pengo lake limeendelea kuonekana mkoani hapa hasa kutokana na hulka yake katika ulingo wa siasa, wengine bado wanaamini ni vigumu kupata mbadala wake. Ndesamburo afariki dunia Mei 31, 2017.
Ndesamburo, ambaye wengi walizoea kumwita Ndesa Pesa, kutokana na umahiri wake wa kujitolea kusaidia watu, pia aliwahi kuwa mbunge wa Moshi Mjini, kwa vipindi vitatu mwaka 2000 hadi 2015.
Akizungumza namna wanavyomkosa Ndesamburo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema anasema enzi za uhai wake alikuwa mtu wa tofauti kwenye jamii katika siasa na hata kiuchumi na kwamba kumkosa kwa mwaka mmoja wamevikosa vitu vinne wanavyo vililia hadi sasa.
Lema anasema moja ya vitu ambavyo wamevikosa ni kwamba hawana kiongozi anayekaa mbele kuwaonyesha watu waende wapi kama alivyokuwa akifanya Ndesamburo enzi za uhai wake.
Anasema kwa sasa hawana mwongozaji, kiongozi anayekaa mbele kupambana na kichaka ili wafuasi wake kupita salama. “Hatuna viongozi wanaotangulia mbele ya wafuasi wake, lakini Ndesamburo alikuwa akitangulia.”
Anasema jambo la pili ambalo wamelikosa ni usuluhishi, kwa kuwa Ndesamburo alikuwa msuluhishi na hakuruhusu watu wagombane naye. Alijitahidi kutatua na kuondoa migogoro. “Hakika alikuwa na mbinu nyingi za usuluhishi.”
Anasema madiwani wa manispaa ya Moshi na maeneo mengine ya mkoa wa Kilimanjaro na hata viongozi wa mikoa mingine na kitaifa, siku zote walijua wanaye baba atakaye waita awasuluhishe jambo ambalo sasa wamelikosa.
Lema anasema, Ndesamburo enzi za uhai wake, aliwanyanyua watu kwa kuwa alikuwa akipanga kazi anaweka nguvu ya kiuchumi ili kuwawezesha kunyanyuka kimaisha. “Wapo watu wengi wenye fedha lakini ni wangapi wenye uthubutu kutumia fedha zao kufanya kazi za kisiasa na kijamii kama Ndesamburo.”
Changamoto
Akizungumzia changamoto ambazo zinawakabili katika chama toka Ndesamburo aondoke, Lema anasema zipo changamoto ambazo hazimuhusu yeye lakini pia zipo ambazo zinamuhusu.
Anaeleza kuwa moja ya changamoto ambazo wamekutana nayo ni kukosa nguvu ya kifedha kwa kuwa enzi za Ndesamburo, walizoeshwa kupewa fedha za kujikimu katika safari pamoja na vifaa vya kazi.
“Hatuwezi kukwepa ukweli nguvu ya kifedha ya kufanya kazi kwani katika mkoa wetu wa Kilimanjaro tulizoeshwa na kudekezwa kwani mzee alikuwa na uwezo mkubwa na baada ya kupanga kazi alituwezesha kwa kutupa fedha, chakula na vifaa kama magari na mafuta, lakini kwa sasa hatuna mtu wa kufanya hivyo, hii ni changamoto kubwa kwa sasa,” anasema Lema.
Anasema Chadema inaendeshwa kwa watu kujitolea, kutokana na kwamba ruzuku inayotolewa na serikali ni ndogo na haitoshelezi kukidhi mahitaji ya chama.
“Kujitolea na kujituma kwa Ndesamburo, kulikifanya chama kiwe imara, kwani Chadema mnayoiona ikiisumbua CCM na serikali, inaendeshwa kwa watu kujitolea na kutoa fedha zao mifukoni”
Kaimu mwenyekiti anena
Akizungumza mwaka mmoja bila Ndesamburo, kaimu mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Selasini anasema Ndesamburo mbali na uongozi pia alikuwa mfadhili wa chama.
“Alitumia rasilimali zake nyingi na utajiri wake kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya chama, hadi sasa hivi hajatokea mtu wa aina yake,” anasema Selasini.
Anasema mbali na kukisaidia chama na jamii pia aliwasaidia baadhi ya wabunge kuwawezesha kufikia walipo, lakini sasa hakuna mtu anayeweza kuwasaidia hata wanapokwama kiuchumi na kwenye miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
“Ndesamburo alikuwa mfano wa kuigwa kwa uvumilivu wa kisiasa, alitunyanyua wengi kisiasa, nikiri tu kwamba tumepoteza na hatujampata wa aina yake na hata tukijitahidi kuiga yale yaliyokuwa akiyafanya, hatuwezi kuyafanya moja kwa moja kwani kazi nyingi za chama yeye alizifanya kwa fedha zake, na si dhani kama kwenye mkoa huu yupo wa aina hiyo,” anasema.
Wadau wamzungumza
Akizungumzia mwaka mmoja bila Ndesamburo, Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro, Awadhi Lema anasema wamempoteza kiongozi maana alikuwa mmoja wa watu ambao walishirikiana kwa karibu na wananchi na hakuwa na makeke kama walivyo viongozi wengine.
Lema ambaye aliwahi kugombea udiwani katika Kata ya Pasua mwaka 2000, anasema, Ndesamburo hakuwa na majivuno kama walivyo baadhi ya viongozi na wakati wote alifikika bila kujali aina ya mtu ambaye anamuhitaji kwa wakati huo.
“Alikuwa hachagui mtu wa kusema naye au kushauriana naye, hakika alikuwa tofauti na wabunge wengine, kwani hakuweka gape (hakuwa na mbali na watu) baina yake na wananchi,” anasema Lema.
Lema anasema Ndesamburo alifanya kazi kubwa ya kujenga Chadema Kilimanjaro, hivyo kuondoka kwake pia kumekiathiri chama na kwamba kukosekana kwake kunaweza kusababisha wakati mgumu katika chaguzi zijazo.
“Ni vyema sasa watu wapendane na kila mtu ajione yuko sawa na mwenzake kwani wakishatokea watu na kujiona kuwa wao ndio muhimu kuliko wengine katika chama watavuruga chama.”
Akizungumza katibu wa Bakwata Wilaya ya Moshi Vijijini, Nuhu Mnango anasema Ndesamburo enzi za uhai wake alikuwa akisaidia makundi na taasisi mbalimbali bila kujali itikadi za kisiasa na dini.
Mnango ambaye anakaimu katibu wa Bakwata Moshi Mjini, anasema, Ndesamburo alisaidia kupatikana kwa pikipiki kwa ajili ya maimamu wa Moshi mjini, ikiwa ni pamoja na kununua baadhi ya vifaa kwenye baadhi ya misikiti.
Anaeleza kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Ndesamburo afariki dunia wameona pengo kubwa kwa kuwa yapo mambo ambayo walikuwa wamejadiliana naye enzi za uhai wake na yeye kuahidi kuwasaidia lakini wamevikosa.
“Kwa kipindi hiki ambacho Ndesamburo hatunaye sisi tunaona pengo kwa kuwa tunajaribu kufikiri mambo ambayo aliahidi kutusaidia ikiwemo pikipiki kwa maimamu ambao hawana na samani katika ofisi ya Bakwata Mkoa, lakini tumevikosa na hatuna mwingine wa kutusaidia na kushirikiana naye kama ilivyokuwa kwa Ndesamburo,” anasema Mnango.
Comments
Post a Comment