Likizo inayomsumbua Ummy
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema atashirikiana na Tume ya Taifa ya Takwimu (NBS) kufanya tathmini kuhusu matumizi sahihi ya likizo ya uzazi kwa wanaume, kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakiitumia vibaya.
Ummy aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya 26 ya wiki ya unyonyeshaji duniani yanayoanza leo hadi Agosti 7, yenye lengo la kuendeleza na kuimarisha unyonyeshaji maziwa ya mama kama njia bora zaidi ya kujenga afya ya mtoto kimwili, kiakili na kijamii.
Alisema baada ya matokeo ya tathmini hiyo atapeleka mapendekezo ifutwe ikiwa itaonekana haina tija kwa afya ya mama na mtoto mchanga.
“Likizo ya uzazi kwa wanaume imewekwa kwa malengo maalumu lakini kwa bahati mbaya walio wengi wamekuwa wakiitumia kukaa vijiweni, kwenye mabaa kunywa pombe na wengine hawaonekani kabisa nyumbani,” alisema.
Ummy alisema anataka kufanya utafiti wa kuwahoji wanaume 1,000 au zaidi kujua ukubwa wa tatizo.
Alisema takwimu za utafiti wa hali ya kidemografia na afya uliofanyika mwaka 2015 zinaonyesha asilimia 34.4 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wana udumavu, ambao umesababishwa na ulishaji usiofuata ikiwamo taratibu za unyonyeshaji.
Pia, alisema Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya unyonyeshaji inampa haki mwanamke mfanyakazi likizo ya uzazi ya siku 84 kama amejifungua mtoto mmoja na siku 100 kwa watoto zaidi ya mmoja.
Alitoa agizo kwa kila mwajiri kuhakikisha anamruhusu mfanyakazi mwanamke aliyejifungua kumnyonyesha mtoto wakati wa saa za kazi kwa saa mbili kwa siku , kwa kipindi kisichopungua miezi sita tangu kumaliza likizo yake ya uzazi.
“Kwa sababu hii, natoa wito kwa taasisi za Serikali, binafsi, za kijamii na kidini kuhamasisha na kuwasaidia wanawake ambao wapo kwenye ajira rasmi na zisizo rasmi ili kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo,” alisema Ummy.
Naye mwakilishi mkazi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Maniza Zaman alisema zaidi ya asilimia 40 ya watoto wachanga nchini hawanufaiki na maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
Alitoa wito kwa Serikali kuangalia namna ya kuongeza fedha za ndani katika lishe ili kuwezesha unyonyeshaji.
Comments
Post a Comment