Serikali yashikilia msimamo wake ushuru wa korosho

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha bungeni  muswada ya sheria ya fedha wa mwaka 2018, jijini Dodoma leo. 
Dodoma. Serikali imeendelea kung'ang'ania msimamo wake wa kufuta kifungu cha 17A cha Sheria ya Sekta ya Korosho ili kuruhusu ushuru unaotokana na mauzo ya korosho ghafi  nje ya nchi kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akizungumza leo Alhamisi Juni 28, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha  muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2018, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema lengo ni kuyafanya makusanyo hayo kuwa sehemu ya mapato ya Mfuko Mkuu wa Serikali badala ya utaratibu wa sasa.
Amesema utaratibu wa sasa asilimia 65 ya mapato hayo ni sehemu ya mapato ya Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho pamoja na gharama za uendeshaji wa bodi ya korosho.
Amesema gharama hizo zitagharamiwa kupitia bajeti ya Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo kama inavyofanyika hivi sasa kwa mazao mengine ikiwemo pamba, kahawa na pareto .
“Lengo la hatua hii ya Serikali ni kuhakikisha kwamba mapato  yanayotokana na ushuru kwenye mazao mbalimbali yanasimamiwa ipasavyo na kutumika kwa ajili ya shughuli zilikusudiwa,”amesema.
Kwa miezi kadhaa suala la asilimia 65 ya ushuru huo limekuwa likijadiliwa bungeni ambapo baadhi ya wabunge wamepinga hatua hiyo ya Serikali kwasababu inaenda kurudisha nyuma uzalishaji wa zao hilo.



Comments

Popular Posts