Majina ya Wanaodaiwa Na Suma JKT Yaanikwa, Wamo Mawaziri, Wabunge na Makada CCM


Shirika  la Uzalishaji Mali la Suma JKT, limetangaza orodha ya majina ya wadaiwa wake sugu wa matrekta ambamo wako pia mawaziri wa sasa, mawaziri wastaafu, wabunge na wakuu wa mikoa.

Baadhi ya majina ya mawaziri wa sasa yaliopo kwenye orodha hiyo ni Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Luhaga Mpina na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Kangi Lugola.

Pia kwenye orodha hiyo yumo Naibu Waziri wa Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Abdalah Ulega, ambaye ni Mbunge wa Mkuranga.

Mawaziri wastaafu waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Dk. Juma Ngasongwa ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na waziri wa wizara mbalimbali kwenye serikali zilizopita.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato mkoani Geita naye ametajwa kwenye orodha hiyo.

Mwingine aliyetajwa kwenye orodha hiyo yenye jumla ya majina 1,392 ni aliyekuwa Waziri wa Fedha kwenye utawala wa awamu ya nne, Mustapha Mkulo.

Wakuu wa mikoa wa sasa waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na Mkuu wa Mkoa wa Sindiga, Dk. Rehema Nchimbi.

Wabunge waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Husna Mwilima wa Kigoma Kusini (CCM), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Maselle (CCM) na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM).

Wabunge wengine waliotajwa ni Ignas Malocha wa Jimbo la Kwela (CCM), Mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwammoto, Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Mary Chatanda na aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini (CCM), marehemu Laurence Gama.

Kwenye orodha hiyo pia wamo wabunge waliopita akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Benson Mpesya (2000-2010).

Wabunge wengine waliopita waliotajwa ni aliyekuwa Mbunge wa Manyoni Magharibi (CCM), Paul Lwanji, aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki (CCM), Kate Kamba, aliyekuwa Mbunge wa Mbarali (CCM), Modestus Kilufi na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Manju Msambya.

Mwingine aliyetajwa ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM na mwanachama wa Chadema sasa, John Guninita.

Kwenye orodha hiyo pia ametajwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, marehemu Said Mwambungu.

Katika tangazo la SumaJKT lililotoka jana kwenye moja ya magazeti ya kila siku, wadaiwa walioshindwa kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kulipa madeni wanayodaiwa kwa wakati, walitangaziwa hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Wakati akizindua Kituo cha Uwekezaji cha Jeshi la Wananchi (JWTZ) kupitia Suma JKT kilichopo Mgulani, jijini Dar es Salaam Mei 17, Rais John Magufuli alitoa mwezi mmoja kwa wadaiwa hao kulipa madeni yao kabla ya msako wa kuwatafuta haujaanza.

Baadaye, Suma JKT iliwatangazia wote wanaodaiwa kupitia tangazo lao la hivi karibuni kwa kuwataka wadaiwa kulipa kabla ya Juni 15, muda ambao tayari umeshaisha.

Tangazo lingine lililotolewa na Makao Makuu ya SumaJKT la Jumanne wiki hii likiwa na kichwa cha habari 'Lipeni madeni kwa wakati' lilisema wale walioshindwa kutekeleza agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.

Pia tangazo hilo liliwaeleza wale waliopatiwa huduma ya ulinzi na Suma JKT Guard na kushindwa kulipa kuwa huduma hizo zitasitishwa na watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kukamata mali zao kufidia deni wanalodaiwa


Comments

Popular Posts