Mahakama kutoa uamuzi Julai 2 kesi ya Mbowe na wenzake
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itatoa uamuzi wa kukubali au kukataa maombi ya viongozi tisa wa Chadema yaliyotaka kusimamishwa kwa muda kwa usikilizwaji wa kesi yao ifikapo Julai 2 mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Juni 28 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kusikiliza maombi ya utetezi na mapingamizi ya maombi hayo ya upande wa mashtaka.
Mawakili wa viongozi hao, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freema Mbowe waliwasilisha maombi ya kusimamishwa kwa muda kwa usikilizaji wa kesi hiyo ya jinai ya mwaka 2018 hadi hapo mahakama itakaposikiliza maombi yao ya marejeo na kutolea uamuzi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi aliiomba mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo akisema kuwa ni batili.
Upande wa Mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa serikali wakuu, Kadushi, Faraja Nchimbi, Dk Zainabu Mango na Wankyo Simon.
Kwa niaba ya jopo hilo la mawakili wa serikali wakili Kadushi aliwasilisha hoja zao kinzani na kuiomba mahakama kuyatupilia mbali maombi ya upande wa utetezi akidai kuwa batili.
Akijibu hoja za upande wa mashtaka, Wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya alidai kuwa wanachoomba waleta maombi ni haki yao ya msingi na katika mazingira haya ni haki yao kusikilizwa.
Hata hivyo Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja hizo alisema atatoa uamuzi Julai 2, mwaka huu.
Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwamo kufanya mkusanyiko usio halali, kuhamasisha chuki, uchochezi wa uasi na kukaidi agizo la vyombo vya sheria Februari 17 mwaka huu.
Pamoja na Mbowe, viongozi wengine wa Chadema katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
Pia wamo Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Comments
Post a Comment