Bei ya mafuta yapanda ghafla
New York, Marekani. Wito wa Rais Donald Trump wa kuzitaka nchi zingine kuacha kuagiza mafuta kutoka Iran umeibua wasiwasi katika soko la nishati hiyo baada ya kuanza kupanda bei.
Bei ya mafuta ilipanda jijini New York, juzi. Kipimo cha bei ya mafuta ghafi kilipanda na kufika Dola70 za Marekani kwa pipa moja kwa mara ya kwanza katika mwezi mmoja.
Bei katika vituo vya mafuta kote nchini Japan ilikuwa juu. Bei ya wastani ya rejareja ya lita moja ya mafuta ya petroli ya kawaida ni zaidi ya Yen 150 kwa wiki ya tano mfululizo.
Bei ya petroli nchini humo inaendelea kuwa juu kutokana na kupanda kwa bei za mafuta ghafi kufuatia Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran.
Marekani imeitaka Japan na mataifa mengine kuacha kuagiza mafuta ghafi kutoka Iran katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, alisema nchi hiyo inataka uagizaji huo usitishwe mpaka Novemba 4.
Alipoulizwa juu ya mgogoro huo kuhusiana na ombi hilo la Marekani, ofisa huyo alisema suala hilo ni changamoto kwa mataifa mengine.
Ofisa huyo alisema Marekani inazitaka nchi hizo kubadili sera zao kuhusu suala hilo, akisisitiza kuwa nyingine zimeonyesha nia ya kukubaliana na Taifa hilo.
Nchi zilizoombwa kuacha uagizaji huo wa mafuta ghafi kutoka Iran ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, China, India na Uturuki.
Comments
Post a Comment