VIDEO-Msomi Chuo Kikuu amrithi Kinana CCM
Dar es Salaam. Hatimaye CCM imetegua kitendawili cha mrithi wa Abdulrahman Kinana baada ya Halmashauri Kuu kumpitisha mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally Kakurwa kuwa katibu mkuu.
Karibu mara mbili, mwenyekiti wa chama hicho, John Magufuli amekuwa akikataa maombi ya kujiuzulu ya Kinana, ambaye anasifika kwa kuihuisha CCM wakati ikielekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, lakini akakubali ombi la tatu.
Jana, Halmashauri Kuu, ambayo ni chombo cha pili kwa ukubwa cha CCM na ambayo ilikutana kwa siku mbili Ikulu jijini Dar es Salaam, ilimpitisha msomi huyo ambaye aliongoza kamati iliyohakiki mali za chama hicho kwa miezi mitano.
“Tumekupa dhamana hii katika kipindi kigumu,” inasema taarifa ya CCM iliyotolewa jana jioni na katibu wa itikadi wa chama hicho, Humphrey Polepole, ikimkariri Rais Magufuli.
“Tumenong’ona na makamu wa mwenyekiti na Rais wa Zanzibar kwamba kazi hii nzuri (ya kuhakiki mali za CCM) uliyoifanya Tanzania Bara ikafanyike na Tanzania Zanzibar.
“Tumekupa jukumu hili tukiwa na matumaini makubwa kwamba yote uliyoyaona kwa miezi mitano, sasa ukayafanyie kazi katika chama chote na jumuia zake kwa nafasi ya katibu kkuu wa CCM.”
Bashiru ni mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala ya UDSM na alikuwa akiongoza kurugenzi ya Mijadala na Makongamano.
Katika taarifa yake, Polepole amesema Dk Bashiru aliwashukuru wajumbe kwa heshima na imani kubwa waliyompa na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi kubwa, uadilifu na kujituma, akiwa mtii kwa katiba ya CCM na ya Nchi.
Taarifa za uteuzi wa Bashiru zilienea kwa kasi jana asubuhi wakati wafuatiliaji wakitaka kujua jina la mrithi wa Kinana hadi zilipothibitishwa na taarifa ya Polepole.
Mara baada ya taarifa hizo kuenea, wasomi mbalimbali waliofanya kazi naye, walimuelezea Dk Bashiru kuwa ni mtu anayefaa kushika wadhifa huo.
Dk Bashiru ni mzalendo
“Sina shaka na uzalendo wake,” alisema Profesa Rwekaza Mukandala, ambaye alikuwa makamu mkuu wa UDSM.
“Bashiru anafaa kwa nafasi hiyo kwa sababu ana uwezo kitaaluma na ni miongoni mwa wasomi wenye uwezo mkubwa kielimu, uwezo wa kujieleza na anatimiza majukumu yake.”
Alisema amemfahamu siku nyingi akiwa mwanafunzi wake wa shahada ya kwanza na ya pili, baadaye akafanya nanye kazi katika nyanja mbalimbali.
“Kizuri zaidi si mtu anayeyumba, huwa anasimamia maneno yake. Akisema hapana ni hapana, akisema ndiyo ni ndiyo na ni mzalendo haswa,” alisema Profesa Mukandala.
Alisema hata aliposhiriki kwenye wanafunzi waliosoma masomo ya uongozi katika chuo cha African Insitute, uliohusisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya Makerere na Nairobi, alikuwa ni kinara.
“Kwa kweli ninaufahamu uwezo wa Bashiru, sina shaka naye na ninaipongeza CCM kwa kumuona anafaa na kumpa nafasi ya uongozi,” alisema Mukundara.
“Napingana na wale wanaosema wasomi wabaki vyuoni wafundishe. Rais Magufuli amepingana na hilo kwa kuwathibitisha wanataaluma katika nafasi mbalimbali za uongozi na wanafanya vizuri.”
Profesa Shivji amfagilia
Msomi mwingine aliyekuwa tayari kumzungumzi ni mkurugenzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji ambaye alisema Dk Bashiru ni mtu pekee anayeweza kukirejesha chama kwenye misingi ya Azimio la Arusha.
“Ni jukumu la chama kufanya uchambuzi wa kina kwa nini kililitupa azimio hilo. Kwa mazingira ya sasa, hayo ndiyo mambo ya kuangaliwa,” alisema Profesa Shivji.
Mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema Bashiru alishajipambanua kama mwana CCM asilia tangu alipokuwa akifundisha chuoni hapo.
“Alijipambanua kama mwana CCM asilia, yaani ile ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo chini ya mwenyekiti wa sasa, Bashiru anaweza kabisa kuirejesha kwenye msingi hiyo,” alisema.
“Ni mtu anayejua maisha ya wanyonge na ameonyesha hivyo alipokuwa akitetea haki za ardhi kwa watu masikini katika taasisi ya Haki Ardhi.”
Hata hivyo, alisema Dk Bashiru atakutana na changamoto ndani ya chama hicho, kama uporaji wa mali za chama aliyoibua katika ripoti ya hivi karibuni.
Makatibu wa jumuiya wateuliwa
Halmashauri Kuu pia iliteua makatibu wa jumuiya za chama hicho ambao ni Raymond Mangwala anayekwenda kuwa mtendaji wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Queen Mlozi (Umoja wa Wanawake, UWT) na Erasto Sima anayekuwa katibu mkuu wa Jumuia ya Wazazi.
Pia halmashauri hiyo pia imemvua uanachama mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe, Abdallah Maulid Diwani kwa kosa la kwenda kinyume na maadili na miiko ya viongozi wa CCM.
Pia imetoa karipio kwa Fancy Nkuhi na Mariam Ussi Yahya, ambao ni wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki kwa mwenendo usioridhisha, usiolinda maslahi ya nchi na unaokinzana na misingi na miiko ya uongozi na wamewekwa chini ya uangalizi wa kimaadili kwa miezi kumi na nane.
Awali, kabla ya kutangazwa kwa uteuzi huo, watu mbalimbali walioongea na Mwananchi, wakiwemo makada wa CCM walionyesha waswasi wao wa mtu anayeweza kujaza nafasi hiyo ya Kinana.
Makada hao na wengine walimuelezea Kinana kama kiongozi wa kipekee, mwenye busara na aliyekuwa anafanya mambo kwa umahiri na hivyo hawaoni mtu wa kuvaa viatu vyake katika siku za karibuni.
“Kumkosa Kinana ni pengo kubwa. CCM na wana-CCM wamepata pigo,” alisema mbunge wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo.
Bulembo alisema Kinana alikuwa anatoa elimu kubwa, ni mkufunzi na aliyeweza kushughulikia masuala mbalimbali ya chama.
Bulembo alisema unapoona kiongozi wa juu anazungumza na watu wa chini, unaona ni mtu wa aina gani.
“CCM imepata pengo, itapata mtu wa kuziba pengo lake si siku mbili, miaka miwili au mitatu. Tuna pengo kubwa sana na hatutapata kama Kinana leo,” alisema Bulembo.
Maoni ya Bulembo yanafanana na ya mbunge wa Donge (CCM), Juma Khamis Sadifa aliyesema “Kinana ni kiongozi mwenye busara, kuondoka kwake ni pengo kubwa ndani ya CCM”.
“Kinana alikuwa kiongozi bora na si bora kiongozi. Aliweza kushughulikia mambo kwa busara. Hakuwa anapokea majungu. Kwa hiyo naweza kusema kaondoka kiongozi mzuri,” alisema Sadifa.
“Kama mtakumbuka Kinana na wenzake akina (aliyekuwa katibu wa itikadi na uenezi, Nnauye) Nape aliipa uhai CCM, yeye ndiye alidiriki kuwaita mawaziri mizigo na hawafai. Kwa hiyo alikuwa kiongozi mzuri na mahiri.”
Sadifa, kama mwenzake Bulembo alisema itakuwa ngumu kumpata mtu kama Kinana.
Taarifa za kujiuzulu kwa Kinana zilipokewa kwa hisia tofauti mwishoni mwa wiki wakati mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alipoandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema: “Pumzika rafiki wa kweli, pumzika mlezi na mzazi usiye mfano, pumzika kiongozi, pumzika komredi.”
“Mwalimu uliyebadili mtazamo wetu juu ya siasa na utumishi kwa umma. Tutakuenzi daima. Komredi. Kinana! Umepanda mbegu na itaota.’’
Ujumbe huo wa Twitter, uliambatana na picha ya Kinana, akiwa na Nape pamoja na January Makamba (waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira).
Kadhalika, mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe aliandika: “Wanakuita Abdul, maana yake mtumishi, wanakuita Abdul Rahmaan, maana yake mtumishi mwenye rehema. Najua umestaafu ukatibu mkuu na si uanaCCM. Huu ndio uimara wa chama chetu kila kiongozi huondoka na kuacha alama yake. Ila mwalimu hastaafu ualimu wake.”
Kwa upande wake, January bila kumtaja, aliandika: “Hajastaafu (Kinana) bali analitumikia Taifa tena bila bughudha za nafasi ya kisasa. Asante kwa elimu kubwa.”
Profesa Gaundence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha alimwelezea Kinana kama mwanasiasa aliyefanikisha kukivusha chama hicho katika misukosuko mingi, ikiwemo kukinusuru kuondolewa madarakani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alisema Kinana alikuwa mwanasiasa aliyethubutu kuikemea Serikali na hatua yake hiyo ndiyo ilimfanya atofautiane na watendaji wengine ndani ya chama na serikalini.
“Amefanya kazi kubwa kukinusuru chama, maana katika uchaguzi uliopita chupuchupu kiondolewe madarakani,” alisema Profesa Mpangala.
Aliongeza kuwa, hata hivyo kustaafu kwake CCM si jambo la kushangaza kwa vile chama hicho kimekuwa na mfumo wa mara kwa mara wa kubadili viongozi wake na hivyo jambo linalopaswa kuzingatiwa na CCM ni kuenzi mfumo wa demokrasia ya kweli kwa Taifa.
“CCM wamekuwa na mfumo wa kidemokrasia ambao ni mzuri, lakini chama hiki tawala ambacho kinapaswa kuhakikisha demokrasia hii inasambaa nchi nzima, vyama vya siasa vipewe uhuru wa kufanya siasa na kutimiza demokrasia yao bila kubanwa wala kuingiliwa,” alisema.
Alimtaka atakayechaguliwa kurithi mikoba ya Kinana pamoja na mambo mengine kuhakikisha anasimamia vyama vya upinzani ili vipatiwe demokrasia ya kweli.
“CCM ni chama tawala, ndicho chenye Serikali hivyo lazima huyu mpya anayekuja alisimamie vyema suala hili,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema Kinana atakumbukwa kwa mengi ikiwamo hatua yake ya kuamua kuzunguka nchi nzima akiijenga upya CCM ambayo ilikuwa tayari imeporomoka.
“Katika takwimu za kuchaguliwa ukiangalia chaguzi zilizopita, CCM ilikuwa imeporomoka kwa takwimu lakini Kinana alijitosa kukihuisha upya chama.. Kuna wakati alizunguka nchi nzima akiwakosoa na kuwasema mawaziri ambao aliwaita mizigo. Haya yote ikiwamo kushiriki katika miradi mbalimbali imekisaidia chama kurudi katika mstari,” alisema.
Hata hivyo msomi huyo alieleza kuwa huenda mwanasiasa huyo ameamua kustaafu baada ya kubaini kuwa muda wa kuendelea kukitumia chama hicho sasa umefika ukingoni.
“Amebaini kuwa mchango wake ndani ya chama umetosha maana hata ukimwangalia yale makeke yake tuliyozowea hatukuyashuhudia katika awamu hii ya tano,” alisema.
Mbunda alisema Kinana anaondoka huku ripoti iliyoundwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kuchunguza mali ya chama ikiwa imebainisha mambo mengi yaliyokuwa yakifanywa kinyume na taratibu.
“Ingawa bado hatujaona ile ripoti, lakini ukisoma ile taarifa ya Ikulu iliyotolewa baada ya Dk Bashiru Ally kuwasilisha ripoti yake, utaona jinsi chama kilivyokuwa kimetawaliwa na ubadhilifu, hivyo kwa namna yoyote Kinana kama mtendaji mkuu wa chama ubadhirifu huu ulitokea wakati yeye yupo (madarakani), utaratibu mzuri ni kuwajibika tu hakuna lingine,” alisema.
Alisema yule anayeingia kuchukua nafasi yake moja ya kazi kubwa anayopaswa kuifanya ni kuendelea pale mtangulizi wake alipoishia lakini jambo kubwa zaidi ni kuweka utaratibu wa kutumia vizuri rasilimali za chama.
Kinana, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa pamoja na uwaziri wa Ulinzi alikuwa katibu mkuu wa CCM kuanzia mwaka 2012.
Comments
Post a Comment