Trump, Abe kukutana tena kujadili mkutano wa kilele



Tokyo, Japan. Waziri Mkuu Shinzo Abe na Rais wa Marekani Donald Trump wamekubaliana kukutana kabla ya mkutano wa viongozi wakuu wa Marekani na Korea Kaskazini uliopangwa kufanyika Juni 12 nchini Singapore.
Abe amesema alizungumza na Trump kwa njia ya simu kwa takriban dakika 30 Jumatatu jioni na kukubaliana kuwa na kikao hicho.
Katika mazungumzo na waandishi wa habari, Abe alisema kwamba aliambiwa kwa kifupi kile kinachoendelea kuhusiana na mazungumzo yanayotarajiwa kati ya Trump na kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
 Mtumishi mkuu
Habari kutoka Pyongyang zinasema ofisa wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini Jumatatu aliwasili Singapore ambako alitarajiwa kukutana na maofisa wa Marekani kujadili mipango ya mkutano huo wa kilele.
Kim Chang Son, aliyetajwa na shirika la habari la Korea Kusini kama "mtumishi mkuu" wa kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong Un aliwasili katika mji wa Singapore kupitia Beijing Jumatatu. Baadaye, ndege iliyobeba msafara wa maofisa wa Serikali ya Marekani iliwasili Singapore.
 Jasusi wa Korea Kaskazini
Taarifa nyingine kutoka Pyongyang zinasema mkuu wa zamani wa shirika la ujasusi la Korea Kaskazini aliondoka Jumanne kwenda Marekani kupitia China ikihisiwa kuwa ni kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa kilele kati ya Trump na Kim Jong-un. Ofisa huyo ni Kim Yong-chol, ambaye inadaiwa ana mafungamano ya karibu na Kim.

Comments

Popular Posts