Maofisa 50 waswekwa mbaroni kwa ufisadi



Nairobi, Kenya. Jeshi la Polisi limewakamata na kuwaweka ndani maofisa wa ngazi ya juu zaidi ya 50 na watendaji wakuu baada ya wananchi kuonyesha hasira kutokana na madai ya wizi wa zaidi ya dola za Marekani 100 milioni katika mashirika ya serikali.
Baada ya zaidi ya wiki ya kusoma habari nyingi katika kurasa za mbele za magazeti ya Kenya na mitandao ya jamii, ofisi ya mwendesha mashtaka ya umma ilitangaza Jumatatu kwamba mashtaka yatafunguliwa kwa watuhumiwa wote ambao majina yao yatakuwa katika mafaili yaliyoandaliwa na idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mkuu wa Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) Richard Ndubai, viongozi waandamizi na wanachama wanne wa familia moja, wanaohusika katika biashara ya ufisadi.
Watuhumiwa hao kwanza walipelekwa kwenye vituo vya polisi vya Muthaiga, Gigiri na Makao makuu kisha wakapelekwa makao makuu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kiambu Road, Nairobi.
Rais Uhuru Kenyatta, ambaye aliahidi kupambana na ufisadi alipochaguliwa kwa mara ya kwanza 2013, haraka alichukua hatua za kupunguza hasira za umma. “Hatutawavumilia watu wasiowaaminifu. Watu waliokabidhiwa majukumu lazima wawe tayari kutumikia badala ya kutumikiwa,” alisema Jumatatu
Wakosoaji wake wanasema, Kenyatta ambaye alishinda kiutata muhula wa pili mwaka jana amekuwa mlegevu kuwafuatilia viongozi wa juu. Hakuna viongozi wowote wa ngazi ya juu ambao wamechukuliwa hatua tangu alipoingia madarakani.
Kashfa ya ufisadi imezingira katika Shirika la Taifa la Huduma ya Vijana (NYS), taasisi ya kijeshi ambayo inawafundisha vijana na kuwapeleka kwenye miradi inayoanzia ujenzi hadi udhibiti wa usalama barabarani. Mradi huo umekuwa kipaumbele katika mpango wa Kenyatta kukubali ukosefu wa ajira wa vijana.
Mkurugenzi mkuu wa mashtaka amesema anafanyia uchunguzi ankara mbalimbali za malipo yanayofikia shilingi za Kenya 8 bilioni (pauni 59 milioni). Uchunguzi wa awali unaonyesha malipo ya ankara nyingi yamezidishwa.
Vyombo vya habari vya Kenya vimeonyesha kwamba NYS lilitumia dola 10 milioni kulipia nyama kwa mwaka mmoja ikiwa na maana kwamba kila kuruta alikuwa anakula kilo 66 za nyama kwa siku.
Ankara nyingine, vyombo vya habari vimeandika tairi moja ilinunuliwa kwa dola 1 milioni.

Comments

Popular Posts