Magufuli aukumbuka wimbo wa ‘Wapo’ wa Ney
Rais John Magufuli ameukumbuka wimbo wa Ney wa Mitego wa ‘Wapo’ ambao ulifungiwa na baadaye kuagiza ufunguliwe.
Tukio hilo limetokea leo Aprili 7, alipokuwa akimaliza kuhutubia katika uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia mjini Arusha kitakachosaidia kutoa huduma kwa watalii na maofisa wa kibalozi.
Hafla hiyo imekwenda sambamba na uzinduzi wa nyumba 31 za polisi, ambapo wageni mbalimbali walihudhuria wakiwemo wakuu wa polisi wastaafu.
Hata hivyo, katika kutaka kuwataja mmoja mmoja waliohudhuria, Rais Magufuli alijikuta akitaja baadhi ya majina na kuongeza neno yupo na baadaye kusema kuwa angekuwa msanii angeimba ule wimbo wa ‘Wapo’, maneno yaliyosababisha umati uliohudhuria shughuli hiyo kushangalia.
Machi 26, mwaka jana wimbo huo wa Ney ulifungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), uliodaiwa kuwa ulimkashifu Rais.
Hata hivyo siku inayofuata, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kuufungulia, agizo ambalo alidai limetoka kwa Rais.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, Rais alifurahishwa na ‘Wapo’ huku akimshauri mwanamuziki huo kutaja majina ya watu wengine kwenye wimbo huo kama vile wakwepa kodi, wauza unga, wabwia unga na watu wengine wasiokuwa na maadili.
Mbali ya kufungiwa wimbo, pia Ney alijikuta akikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa mjini Morogoro ambapo nao waliamuriwa kumwachia huru.
Comments
Post a Comment