Mbowe ,Mashinji washindwa kufika polisi leo

Chadema kimetoa sababu za viongozi wake wakuu watatu akiwamo Freeman Mbowe zilizowafanya wasiitikie wito wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Mbowe pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho-Zanzibar, Salum Mwalimu ni kati ya viongozi saba wa Chadema waliopaswa kufika Kituo Kikuu cha Polisi leo Februari 20  lakini hawakufika.
Akizungumza leo Februari 20, 2018 na Mwananchi, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema wakati wanapokea barua ya wito wa polisi kwa viongozi hao kufika kituoni wengine walikuwa wametawanyika.
“Mfano, Salum Mwalimu jana alitangulia Mafinga (Iringa) kwa ajili ya kuongoza mazishi ya kiongozi wetu Daniel John hivyo kwa wito tulipokea asingeweza kufika sawa na Mwenyekiti (Mbowe) alikuwa nje ya Dar es Salaam,” amesema Mrema na kuongeza,
“Katibu Mkuu (Dk Mashinji) wakati tunapokea wito yeye alikuwa safarini kwenda Marekani kikazi na alisafiri saa 10 jioni akipita ‘airport’ ya Dar es Salaam, kwa hiyo kama wangetoa taarifa mapema wangeweza wao wenye kumdaka pale pale ‘airport.”
Mrema amesema viongozi hao watakaporejea kabla ya Jumanne ya Februari 27, 2018 wanayotakiwa kuripoti na viongozi wengine watakwenda kuitikia wito huo.
Viongozi walioripoti leo kituoni hapo na kuachiwa kwa dhamana ni, Naibu Katibu Mkuu- Bara, John Mnyika, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee, Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Ester Matiko ambaye ni Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake Bawacha.

Comments

Popular Posts