Maporomoko ya rundo la takataka yaua watu 17 Msumbiji
Takriban watu 17 wakiwemo watoto wamepoteza maisha mjini Maputo nchini Msumbiji na wengine wengi kujeruhiwa baada ya rundo la takataka kuporomoka, maafisa wameeleza.
Takataka hizo zilizorundikwa mpaka urefu wa futi 49 kwenda juu, liliporomoka baada ya mvua zilizonyesha siku ya Jumatatu.
Eneo hilo la kutupa taka linajulikana kuwa makazi ya wakazi masikini wa mji huo, ambao waliweka makazi katika eneo lenye takataka hizo.
Nyumba tano zilibomolewa na maporomoko hayo.Vikosi vya uokoaji vinawatafuta walionusurika na tukio hilo.
Msemaji wa kikosi cha huduma za dharura, Leonilde Pelembe,amesema huenda kuna waathirika zaidi walionasa kwenye takataka hizo.
Wilaya ya Hulene mjini Maputo ni moja kati ya sehemu duni mjini Maputo.Watu wengi wakiwemo watoto, hawana namna isipokuwa kuweka makazi yao kwenye takataka hizo au pembezoni mwa jalala.
Jalala hilo haliwapatii tu chakula, bali vitu ambavyo huviuza, Mwandishi wa BBC Jose Tembe ameeleza.
Mamlaka zimesema awali ziliwataka wakazi wa eneo hilo kuondoka kwa kuwa makazi yao yalijengwa kinyume cha sheria, Shirika la habari la Reuters limeripoti.
Mkazi mmoja ambaye kijana wake alijeruhiwa na maporomoko hayo, Maria Huo,amesema ''Ninaishi eneo hili kwa kuwa sina pa kwenda, Serikali ingeniambia wapi pa kwenda kuishi ningekwenda''.
Mji wa Maputo ulipatwa na mvua kubwa tangu siku ya Jumapili, mvua ambayo iliharibu nyumba na barabara kufurika.
Comments
Post a Comment