Lowassa apongeza kauli ya maaskofu
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amewapongeza maaskofu kwa kuunga mkono mambo aliyosema wamekuwa wakiyapigania.
Lowassa ametoa pongezi hizo leo Februari 11,2018 akimnadi mgombea ubunge jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu katika Kata ya Kijitonyama.
“Leo kwenye magazeti wameandika kwamba Baraza la Maaskofu wamezungumzia mambo ambayo tumekuwa tunayasema kila siku, kuhusu kuzuia uhuru wa kuzungumza na suala la maadili. Ninawashukuru sana maaskofu, ninawapongeza sana kwa kuunga mkono ambayo tumekuwa tunayasema,” amesema Lowassa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.
Lowassa akimnadi Mwalimu alisema anamfahamu kwamba ni kijana shupavu na mchapa kazi ambaye akipewa kura wananchi wa Kinondoni watapata maendeleo.
“Kinondoni msilale mpaka kieleweke. Mchagueni Salum Mwalimu akawaletee maendeleo,” amesema.
Mwalimu akiomba kura amesema Kinondoni ni watu ambao wanajitambua.
“Kinondoni ni watu mnaojitambua, ni watu ambao mlijitoa mwaka 2015, wengine waliachika. Ninawapenda sana, ninajua nina deni kubwa la kuwalipa,” amesema.
Mwalimu amesema, “Ninapozungumza najua ninazungumza na wajanja ambao hawadanganyiki. Tangu juzi, wenzangu wameleta fedha hapa Kijitonyama kwa ajili ya kununua shahada.”
Amesema waliposikia anagombea ubunge walipata hofu kubwa, vikao vikawa haviishi wakitafakari itakuwaje nikienda bungeni.
Comments
Post a Comment