Sugu aenda rumande hadi Ijumaa


Mbeya. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imeamuru mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) na katibu wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga kwenda mahabusu hadi Ijumaa itakapotoa uamuzi kuhusu dhamana yao.
Wawili hao walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo jana asubuhi kabla ya wakili wa Serikali, Joseph Pande kuwasomea mashtaka ya matumizi ya lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Pande alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Desemba 30 mwaka jana katika Uwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini hapa.
Uamuzi wa hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite kuwapeleka mahabusu watuhumiwa hao ulitokana na Pande kuiomba Mahakama kutowapatia dhamana kwa sababu za kiusalama, hoja ambayo ilipingwa na wakili wa washtakiwa, Sabina Yongo.
Akisoma mashtaka ya watuhumiwa hao, Pande alisema, “Sugu alitamka ‘hayo ndio mambo ambayo Magufuli angefanya kama anataka kupendwa… hawezi kupendwa kwa kumshuti Lissu, (Tundu-Mbunge Singida Mashariki), huwezi kupendwa kwa kumtupa Lema (Godbless-mbunge Arusha Mjini) miezi minne gerezani.”
Mwendesha mashtaka huyo aliendelea,”Pia Sugu alisema ‘huwezi kupendwa kwa kumkataza Sugu asiongee hivi, asiongee hili au lile, huwezi kupendwa kwa kuteka watu, umemteka Roma, unamteka Ben Saanane mtoto wa watu hadi leo hatujui alipo.”
Kuhusu Masonga, Pande alisema akiwa na Sugu alitamka kuwa Rais Magufuli amebadili namna ya kutawala na kwamba anaamini njia pekee ni kuwafanya watu wasizungumze.
Washtakiwa hao walikana kutenda kosa hilo na Pande alieleza kuwa upande wa Jamhuri umekamilisha upelelezi na kuiomba mahakama kuendelea na taratibu za kusikiliza kesi hiyo itakavyoona inafaa.
Mabishano kuhusu dhamana
Wakili Yongo akisaidiana na Boniface Mwabukusi aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo na kuipangia siku nyingine kwa maelezo kuwa hakujiandaa kuomba wateja wake kupatiwa dhamana. Ombi hilo lilipingwa na Pande kwa maelezo kuwa kosa linalowakabili washtakiwa hao si tu chukizo kwa Rais Magufuli bali ni chukizo kwa Watanzania wote waliomchagua kiongozi mkuu huyo wa nchi, kutaka warejeshwe rumande kwa sababu ya usalama wao.
“Kwa nia njema kabisa tunaiomba mahakama yako tukufu isiwape dhamana washtakiwa hawa kwa sababu ya usalama wao,” alisema na kuongeza,
“Mashtaka yao ni matumizi ya lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli ambaye amechaguliwa na Watanzania wakiwamo watu wa Mbeya… hivyo si chukizo kwa Rais pekee bali hata kwa waliosikia.”

Comments

Popular Posts