Siku 27 za mapambano Kinondoni, Siha
Siku 27 za kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni na Siha zinatarajiwa kuwa ‘vita’ baina ya vyama vitatu vikubwa vya siasa; CCM, Chadema na CUF.
Wakati CCM ikitamba kuibuka na ushindi katika majimbo hayo kwa madai kuwa Serikali yake imetekeleza yale iliyoahidi, Chadema imesema haitakubali kuchezewa kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa kata 43 wa Novemba 26 mwaka jana.
Changamoto zilizoibuka katika uchaguzi huo wa madiwani zilisababisha vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi kususia uchaguzi mdogo wa ubunge wa Longido, Songea Mjini na Singida Kaskazini uliofanyika Januari 13, uamuzi ambao uliungwa mkono na vyama vingine vya Chaumma na ACT- Wazalendo.
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema jana kwamba chama hicho tawala kitashinda katika chaguzi hizo huku akitaja sababu mbili; “Tunashughulikia shida za wananchi na tunafanya siasa za maendeleo.”
Alisema CCM imejipanga kushinda na itafanya hivyo kwa sababu ni chama kinachoeleweka zaidi kwa wananchi.
Chadema kwa upande wake, imeshapanga safu mbili kila moja ikiwa na vigogo 15 zitakazoweka kambi katika majimbo hayo.
Ile ya Kinondoni itaongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na ile ya Siha itakuwa chini ya mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.
Vita ya kuwania Jimbo la Kinondoni itashuhudia naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu atakavyopambana na mgombea wa CCM, Maulid Mtulia ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF kabla ya kuhamia chama hicho Desemba 2, mwaka jana hivyo kupoteza sifa ya kuwa mbunge.
Lakini pia kutakuwa na mpambano mkali kati ya Chadema na mgombea wa CUF, Rajabu Salim Juma anayeungwa mkono na chama hicho unaoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba.
Tayari Jumaa ameilalamikia Chadema kwa uamuzi wake wa kumsimamisha Mwalimu kwa madai kuwa unavunja nguvu ya upinzani kuibuka na ushindi.
Mshikemshike mwingine katika uchaguzi huo utakuwa baina ya CUF upande wa Lipumba ambaye anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kama mwenyekiti halali wa chama hicho, dhidi ya CUF upande unaomuunga mkono katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambao unamuunga mkono mgombea wa Chadema kwa mwavuli wa Ukawa.
Katika jimbo la Siha nako vita itakuwa kali kati ya mgombea wa Chadema, Elvis Mosi na wa CCM, Dk Godwin Mollel ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema tangu 2015 mpaka Desemba 14 mwaka jana alipojivua uanachama na kuhamia CCM.
Pamoja na uchaguzi huo kuwa katika majimbo mawili, Kinondoni ndiko kunakotarajiwa kuwa moto na Mtulia anaonekana kuwa na kibarua kigumu zaidi kwani anaingia katika uchaguzi huo akikabiliwa na upinzani kutoka makundi mawili ambayo yote yalimuunga mkono na kushirikiana mpaka alipotangazwa mshindi kwa kumbwaga aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan.
Kibarua cha kwanza ni CUF upande wa Maalim Seif ambao kwa kiasi kikubwa walipigania ushindi wake sambamba na kumpitisha kwa mwamvuli wa Ukawa.
Mvutano ulioibuka katika chama hicho baada ya Profesa Lipumba kurejea kwenye uongozi mwaka 2016, ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipoutangazia umma kwamba amejiuzulu uliibua makundi mawili ndani ya chama hicho, ambayo yatachuana vikali katika uchaguzi huo moja likiwa upande wa Chadema.
Pia, uwepo wa Juma, mgombea huyo wa CUF ambaye mwaka 2015 alikuwa meneja wa kampeni wa Mtulia, kunaweza kumpa wakati mgumu mgombea huyo wa CCM.
Pia, CCM iliyokuwa ikimpinga Mtulia mwaka 2015 akiwa CUF na kikashindwa, sasa itakuwa na mtihani wa kwenda kumnadi kwa wananchi walewale ili ipewe dhamana ya kulirejesha jimbo hilo ambalo ililipoteza.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mbowe alisema, “Kitawaka, hatutakubali kuchezewa kama ule uchaguzi wa kata 43, tunataka haki itendeke la sivyo hakitaeleweka.”
Alipoulizwa watatumia njia gani kushinda, Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema, “Hatuwezi kuweka silaha zote hadharani, lakini niseme tu kwamba hatutakubali kuchezewa.”
Mwalimu
Mara baada ya kukamilisha mchakato wa fomu, Mwalimu aliwashukuru wanachama wa Chadema kwa kumsindikiza kuzirejesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)na kusema hiyo ni safari yake muhimu ya kugombea jimbo.
“Nashukuru fomu imepokewa na haina makosa na nilikuwa nauliza kila kipengele na maelezo na wahusika walitujibu ipo sahihi,” alisema Mwalimu jana.
Kuhusu kuanza kampeni Mwalimu alisema anasubiri mchakato wa mapingamizi uliotarajiwa kuanza jana jioni hadi kesho saa 10 jioni kabla ya kutangaza siku ya kuanza kampeni.
“Nawaomba watu wavumilie mchakato huu uishe, lakini kesho saa 10 nitawatangazia. Nawapenda wakazi wa Kinondoni maana jana nilipigiwa simu zaidi ya 100 za kunipongeza baada ya kuchukua fomu,” alisema.
Mwalimu alisisitiza kuwa hakubahatisha kuingia katika uchaguzi huo.
Mtulia
Wakati Mwalimu akisema anasubiri mapingamizi kutangaza siku ya kuanza kampeni, Mtulia alisema kesho anatarajia kuanza kampeni huku akisisitiza kufanya kampeni za kistaarabu na kuwataka wapinzani wake nao kufanya hivyo.
“Nakishukuru chama kwa kuniteua, pia nashukuru wanachama wa CCM kwa kupokea uamuzi wa Kamati Kuu baada ya kuniteua. Kesho natarajia kuanza kampeni zangu.” Alisema CCM itafanya kampeni za kistaarabu na Kinondoni ndiyo Dar es Salaam hivyo lazima wawafundishe watu wa maeneo mengi namna kampeni za kistaarabu zinavyofanyika.
Kazi imeanza
Mara baada ya kurejesha fomu zake katika ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jana, Juma alianza kutoa shutuma kwa Chadema akisema kitendo ilichokifanya cha kusimamisha mgombea ni kutaka kuzigawa kura.
“Chadema wanakuja kupoteza nguvu na kuja kugawa kura za wapinzani. CUF ililipata jimbo la Kinondoni kukiwa na ushirikiano wa Ukawa na siyo mtu mmoja. Chama kilichoshirikiana katika mchakato huo bado kipo na kimemsimamisha mgombea, iweje leo Chadema wamesimamisha mgombea na wao tena?” alihoji Juma. Hata hivyo, Juma aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutovunjika moyo na hamahama ya viongozi hatua ambayo alisema imelenga kudhoofisha upinzani na kuwataka wasirudi nyuma.
Wengine waliorudisha fomu ni mgombea wa chama cha Demokrasia Makini, Juma Mboya ambaye alisema ataanza kampeni zake kesho katika Uwanja wa Biafra.
“Nina uhakika tutashinda na nina imani vijana wenzangu wataniunga mkono katika mchakato huu ambao chama kimeniamini na kunipa nafasi,” alisema Mboya
Comments
Post a Comment