Waziri Makamba afafanua kuhusu mkanganyiko matumizi mifuko ya plastiki

vifungashio Plastiki,mifuko  plastiki,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba,


Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amesema hakuna mtu atakayekamatwa kwa kukutwa na vifungashio vya vyakula mfano wa karanga, Ubuyu, kwani kinachokatazwa ni kutumia vifungashio hivyo kubebea bidhaa nyingine.
Kauli hiyo ameitoa siku moja baada ya kusambaa habari kuwa Serikali imepiga marufuku matumizi ya vifungashio vinavyohifadhia vyakula kama ubuyu, karanga, ice cream na bidhaa nyingine kama hizo ambapo waziri Makamba amesema kuwa taarifa hiyo sio kweli.
Katika mtandao wa kijamii wa Twitter waziri Makamba ameutumia kuwajibu watanzania mbalimbali waliokuwa wakihoji na kutaka ufafanuzi wa suala hilo.
“Vifungashio vya bidhaa za vyakula (karanga, ubuyu, etc) havijazuiwa. Kinachozuiwa ni vi-plastic hivi transparent ambavyo huwa vinafungia karanga, ubuyu etc visitumike kuendea sokoni/dukani kubebea bidhaa. Hakuna mtu atakamatwa kwa kuuza karanga kwenye kifungashio cha plastiki” Ameeleza waziri Makamba katika mtandao huo.
Vile vile, Makamba ameeleza kuwa zipo bidhaa ambazo lazima zifungwe kwenye mifuko ya Plastiki ili kulinda ubora wa bidhaa hizo kama magodoro, peremende na biskuti hivyo bidhaa kama hizo zitaendelea kuwa kwenye mfumo huo wa kufungwa kwenye vifungashio vya Plastiki.

Comments

Popular Posts