WASTAAFU 10,000 WA PSSSF WALIOKUWA WANADAI WALIPWA BILIONI 880
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) umefanya malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 880 kwa wastaafu elfu 10,000 ambao walikuwa wanadai malimbikizo ya pensheni ya mkupuo na ya kila mwezi, Meneja Kiongozi wa Mfuko huo Bi. Eunice Chiume amesema.
Amesema malipo hayo yamefanyika katika kipindi cha mpito kilichotolewa na serikali kuanzia Agosti 2018 hadi Februari 2019 hii ikiwa ni chini ya mwaka mmoja tangu Mfuko huo uanze kutekeleza majukumu yake Agosti 1, 2018 baada ya serikali kuunganisha Mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii, ambayo ni PSPF, LAPF, PPF na GEPF.
“Ili kuhakikisha PSSSF inatoa huduma bora na za haraka, imefungua ofisi mikoa yote Tanzania bara na Visiwani na tunatoa wito sasa, kwa wale wastaafu takriban elfu 10,500 ambao bado taarifa zao hazijahakikiwa wafike kwenye ofisi zilizo karibu nao ili kukamilisha zoezi hilo muhimu linalofanyika kila mwaka.” Alisema Meneja huyo kiongozi wakati akizungumza na waendesha bloggers na waendesha mitandao ya kijamii kwenye ofisi za PSSSF, barabara ya Ohio jijini Dar es Salaam Juni 13, 2019.
Alisema uhakiki wa wastaafu sio kitu kipya ingawa mwaka huu zoezi hilo lilionekana kama ni geni.
“Lengo la uhakiki ni kuupa Mfuko fursa ya kufanya malipo kwa wakati, usahihi na kwa mtu anayepaswa kulipwa kwani taarifa zinaweza kubadilika ikiwa ni pamoja na zile za kibenki huenda muhusika akahama kutoka benki moja kwenda nyingine, mabadiliko ya wategemezi lakini haka kifo pia.” Alifafanua Bi. Chiume.
Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF), Bi. Eunice Chiume (katikati), akisikilzia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mmoja wa bloggers katika kikao baina ya meneja huyo na wamiliki na waendeshaji wa blogu hapa nchini. Kikao hicho kilicholenga kujenga mahusiano na kuutambulisha Mfuko huo Mpya kwa wamiliki hao wa mitandao ya kijamii kilifanyika ofisi za PSSSF jengo la Jubilee Tower jijini Dar es Salaam Juni 13, 2019.
Comments
Post a Comment