Soma hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20


HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO

YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20

I.    UTANGULIZI
1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kukubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2019/20. Hii ni bajeti ya nne ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 26 cha Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015.

2.    Mheshimiwa Spika, hotuba hii inaambatana na vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2019 ambavyo ni sehemu ya bajeti hii.
3.    Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumuinulia Mungu moyo wangu wote kwa shukrani, kwa kuwa amenijalia mema mengi katika maisha yangu na katika utumishi wangu kwa Taifa. Ninamshukuru kwa kuendelea kuijalia nchi yetu amani na umoja na kutupatia safu ya juu ya uongozi wa Taifa hili unaomtanguliza Mungu katika kuwatumikia Watanzania wote na kujielekeza kutatua kero za wanyonge.
4.    Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo kwa Mwenyezi Mungu, naomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa uongozi wake shupavu na wa mfano katika bara la Afrika hususan katika kufanya maamuzi magumu yenye maslahi mapana kwa Taifa. Katika kipindi cha uongozi wake: amesimamia kwa ujasiri uvunaji adili wa rasilimali za Taifa; ameongoza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi bila
kigugumizi; amedhibiti biashara haramu ya madawa ya kulevya; ameimarisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma; na ameendelea kusikiliza na kushughulikia malalamiko na kero za makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo wajasiriamali wadogo (wamachinga na mama/baba lishe), wafanyabiashara wadogo wa madini, wakulima na wafugaji, na wafanyabiashara wa kati na wakubwa kutoka katika wilaya zote nchini. Vile vile, ameendelea kudumisha amani na usalama katika nchi. Aidha, amethubutu kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo ili kujenga Tanzania mpya. Nitaeleza hapo baadaye mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii nchini. Kwa sasa itoshe tu niseme kuwa yalihitajika maamuzi magumu kutoka kwa kiongozi jasiri kuelekeza utekelezaji wa mageuzi makubwa na miradi ya kielelezo ambayo yameleta maendeleo makubwa na ya kuvutia katika miaka hii mitatu na nusu tu! Watanzania tunayo kila sababu ya kujivunia kumpata kiongozi shupavu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenye uthubutu na uzalendo wa hali ya juu.

5.    Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, ninapenda kumshukuru kipekee Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya Waziri wa Fedha na Mipango na hivyo kuniwezesha kuandaa na kusoma hotuba ya bajeti kuu ya Serikali hivi sasa kwa mara ya nne mfululizo. Kwa unyenyekevu, ninasema asante sana Mheshimiwa Rais kwa heshima hii kubwa uliyonipatia mimi na wananchi wenzangu wa wilaya ya Buhigwe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Ninayasema haya nikitambua kwamba wapo Watanzania wengi wenye sifa za kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Mimi ni nani basi hata nikateuliwa na kukabidhiwa majukumu haya makubwa? Kama alivyonijibu yeye mwenyewe siku aliponiteua, kazi hii nimepewa kwa neema tu kutoka kwa Mungu. Hivyo, napenda niwaahidi tena Watanzania kuwa nitaendelea kuifanya kazi hii ya Mungu kwa uadilifu.
6.    Mheshimiwa Spika, naamini Watanzania watakubaliana nami kuwa nguzo ya uongozi thabiti ni wasaidizi imara na wanaojituma. Hivyo, kwa namna ya pekee, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa busara na bidii katika kazi zake za kumsaidia Rais

kuongoza Taifa letu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa hekima, hali ambayo imewaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo yanayoonekana katika kipindi cha uongozi wake. Kadhalika, napenda kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mbunge wa jimbo la Ruangwa, kwa uongozi hodari ndani ya Serikali na hapa Bungeni pamoja na kumsaidia Rais kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Vile vile kwa namna ya pekee sana nimpongeze Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu wa  CCM kwa utendaji wake uliotukuka na kusimamia misingi ya Chama Cha Mapinduzi ya kupigania usawa wa binadamu na haki za wanyonge.
7.    Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia wakuu wa mihimili mingine ya dola kwa usimamizi na uongozi shupavu, hususan wewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa kuongoza vema mhimili wa Bunge. Hakuna shaka hata kidogo na kila mtu sasa anajua kwamba Bunge hili ni chombo chenye nguvu sana chini ya Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Naibu Spika Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb). Aidha, ninampongeza sana Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamisi Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa uongozi makini wa mhimili wa Mahakama.
8.    Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma, kwa kutekeleza kazi zake kwa weledi mkubwa.
9.    Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na kuwashukuru kwa dhati wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama, makamanda na askari wote (wanaovaa na wasiovaa sare za majeshi) kwa utumishi wao makini na uzalendo wa hali ya juu. Kipekee naomba niwatambue Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Nyakoro Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Faustine Martin Kasike; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter

Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Francis Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman Msuya; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Rogers William Siang’a; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye. Hakika, Watanzania tunatembea kifua mbele na kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila wasiwasi kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko macho na imara kuliko chuma! Tunawaomba muendelee kutimiza wajibu wenu wa kulinda mipaka na amani ya nchi yetu kwa wivu na moyo wa kizalendo na hivyo kuzidi kuimarisha mazingira ya kuwasha moto wa maendeleo na ustawi wa Taifa letu na wananchi wake.
10.    Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninamshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Profesa Adelardus Lubango Kilangi kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2019. Napenda pia nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, na Makamu wake Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kwa umakini wao katika kuongoza shughuli za Kamati hii muhimu sana. Chini ya uongozi wao, Kamati ya Bajeti imetupatia maoni mengi na ushauri wa kujenga ambao umeisadia sana Serikali katika kuboresha mapendekezo ya bajeti hii.
11.    Mheshimiwa Spika, kwa kipindi chote ambacho nimekuwa kwenye nafasi hii, napenda nishuhudie kwa Bunge hili na Taifa kwa ujumla kwamba, Kamati hii ya Bajeti imetoa mchango mkubwa sana katika kuboresha sera za uchumi na bajeti kuliko Watanzania wengi wanavyofahamu. Kusema kweli wanastahili kutambulika kipekee. Kama kuna nishani au tuzo ya Spika kwa Kamati ya Bunge inayojitanabaisha kwa utumishi uliotukuka, basi kama itakupendeza Mheshimiwa Spika, napendekeza iwe Kamati ya kwanza kutunukiwa heshima hiyo. Aidha, ninawapongeza Wenyeviti, Makamu wenyeviti na wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa michango yao waliyoitoa kupitia vikao

vya kamati za kisekta katika kuboresha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali na Serikali kwa ujumla kwa mwaka 2019/20. Maboresho hayo yalilenga kuwapatia Watanzania maendeleo hususan uboreshaji wa huduma za kijamii na miundombinu.
12.    Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2019/20 imeandaliwa kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwainua wananchi wanyonge kiuchumi na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini. Dhima kuu kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bado itaendelea kuwa “kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Bajeti hii inaendelea kufungamanisha juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda na uendelezaji wa sekta ya kilimo inayoajiri wananchi wengi na hasa waishio vijijini huku msisitizo ukiwa katika kuhamasisha tija na uzalishaji, kujenga miundombinu ya kiuchumi, kutafuta masoko, kupunguza kero kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wawekezaji na kuimarisha huduma za jamii.
13.    Mheshimiwa Spika, leo asubuhi niliwasilisha Hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20 ambapo nilieleza kwa kina mwenendo wa viashiria mbalimbali vya uchumi katika mwaka 2018. Aidha, katika hotuba hiyo, nilifafanua juu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19 na kuainisha maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2019/20. Hivyo, katika hotuba hii, nitajielekeza kutoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, kuwasilisha maboresho ya mfumo na viwango vya kodi na tozo mbalimbali, pamoja na mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20, ambayo yanatoa picha ya namna gani Serikali inakusudia kuendelea kukuza uchumi, kuboresha kilimo, miundombinu, huduma na kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuboresha ustawi wa Watanzania.

II.    TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19

Mwenendo wa Mapato
14.    Mheshimiwa Spika, Katika bajeti ya mwaka 2018/19, Serikali ilitarajia kupata jumla ya shilingi trilioni 32.48 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Mchanganuo wa mapato yaliyopatikana hadi Aprili 2019 ikilinganishwa na lengo la kipindi hicho ni kama ifuatavyo:
(i)    Mapato ya kodi yalifikia shilingi trilioni 12.9, sawa na asilimia 87.4 ya lengo;
(ii)    Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi trilioni 2.04, sawa na asilimia 122 ya lengo. Mapato yasiyo ya kodi yalivuka lengo kutokana na kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye taasisi za Serikali kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Serikali wa Ukusanyaji wa Mapato (Government electronic Payment Gateway –GePG);
(iii)    Mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo;
(iv)    Misaada na Mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia shilingi trilioni 1.70 sawa na asilimia 86 ya lengo;
(v)    Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 3.3, sawa na asilimia 57.4 ya lengo; na
(vi)    Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje ilifikia shilingi bilioni 692.3.
15.    Mheshimiwa Spika, kutofikiwa kwa malengo ya mapato ya kodi kulitokana na sababu mbalimbali, zikiwemo; ugumu wa kutoza kodi sekta isiyo rasmi; kuendelea kuwepo kwa upotevu wa mapato kunakosababishwa na tatizo la magendo hususan kupitia bandari bubu kwenye mwambao mrefu wa Bahari ya Hindi; na mwamko mdogo wa
wananchi kudai risiti za kielektroniki wanapofanya manunuzi au baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutotoa risiti wanapofanya mauzo.
16.    Mheshimiwa Spika, kutopatikana kwa mikopo ya ndani kama ilivyotarajiwa kumetokana na kupungua kwa washiriki katika soko la fedha la ndani hususan mifuko ya hifadhi ya jamii iliyokuwa kwenye zoezi la kuunganishwa. Kwa upande wa mikopo ya nje ya kibiashara, upungufu uliojitokeza ulitokana na hali ya masoko ya fedha kimataifa kubana zaidi (tighter global financial conditions) hususan kuimarika kwa dola ya Marekani, na riba kubwa za mikopo. Hali hii pia ilipelekea majadiliano na taasisi za fedha za Kimataifa kuchukua muda mrefu ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata mikopo hiyo kwa gharama zinazohimilika.
17.    Mheshimiwa Spika, mwenendo wa upokeaji wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya Washirika wa Maendeleo kutotimiza ahadi zao kama walivyoahidi kwenye bajeti kinyume na misingi ya makubaliano kama ilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania (Development Coperation Framework – DCF).
Mwenendo wa Matumizi
18.    Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2018/19 iliyoidhinishwa na Bunge ilikuwa shilingi trilioni 32.48 ambapo shilingi trilioni 20.47 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.01 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Aprili 2019, Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 22.19 zikijumuisha shilingi bilioni 529.25 kutoka kwenye makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 16.75 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 6.28 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma, shilingi trilioni 2.49 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi trilioni 7.98 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
19.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2019 Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 5.44 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 4.89 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 547.38 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki hakijumuishi baadhi ya fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi (D-Funds) ambazo hazikupita kwenye mfumo wa malipo wa Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu za kiuhasibu zitakapokamilika mwishoni mwa mwaka wa fedha.
20.    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mamlaka za Serikali za Mtaa hadi kufikia Aprili 2019 jumla ya shilingi bilioni 529.25 ambazo zinatokana na makusanyo yao ya ndani zimetumika. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 211.7 zimetumika kugharamia miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 317.55 zimetumika kugharamia matumizi ya kawaida.
21.    Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo ya kimkakati ambayo yamepatiwa fedha katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019 ni pamoja na:
(i)    Kulipa mishahara ya watumishi kila mwezi kwa wakati ambapo hadi Aprili 2019 jumla ya shilingi trilioni 6.3 zimelipwa;
(ii)    Kuendelea kulipa madeni ya Serikali kwa mujibu wa mikataba ambapo jumla ya shilingi trilioni 5.7 zilitumika, ikijumuisha shilingi trilioni 2.8 kwa ajili ya kulipa mtaji wa deni la ndani kwa utaratibu wa “rollover”.
(iii)    Kugharamia uendeshaji wa ofisi ambapo jumla ya shilingi trilioni
2.2 zimelipwa;
(iv)    Mradi wa kufua umeme utokanao na nguvu za maji katika Mto Rufiji ambapo kiasi cha shilingi bilioni 723.6 kimetolewa;
(v)    Kugharamia elimu msingi bila ada na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ambapo zimetolewa shilingi bilioni 616.9;
(vi)    Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jumla ya shilingi bilioni 269.3 zimetolewa;

(vii)    Ununuzi    na    uendeshaji    wa    ndege    mpya    ambapo    zimetolewa shilingi bilioni 238.8;na
(viii)    Kuendeleza    ujenzi    wa    meli    mpya    katika    maziwa    makuu, zimetolewa shilingi bilioni 27.6.
Ulipaji wa Malimbikizo ya Madai
22.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakiki na kulipa madeni ya wazabuni, makandarasi na watumishi ambapo hadi Mei 2019 kiasi cha shilingi bilioni 598.4 kimelipwa kati ya bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 600.0 kwa mwaka 2018/19. Kati ya kiasi kilicholipwa shilingi bilioni 300.5 ni kwa ajili ya wakandarasi, shilingi bilioni 232.9 ni kwa ajili ya watoa huduma, na shilingi bilioni 65.0 ni kwa ajili ya watumishi. Aidha, Serikali imelipa malimbikizo ya kimshahara ya watumishi 790 waliostaafu kabla hawajalipwa, ambapo hadi Aprili, 2019 jumla shilingi bilioni 3.10 zililipwa.
23.    Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa na kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kupunguza ulimbikizaji wa madai ikiwa ni pamoja na kuhimiza uzingatiaji wa Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015; Sheria ya Ununuzi wa Umma SURA 410; Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali.

24.    Mheshimiwa Spika, napenda nisisitize kuwa japokuwa rasilimali fedha zinazopatikana hazitoshi kugharamia mahitaji yote ya kawaida na miradi ya maendeleo, hakuna shaka kwamba kupitia jitihada tunazofanya hivi sasa, tunapanda mbegu leo ambazo zimeanza na zitaendelea kuzaa matokeo mazuri ya Tanzania ya uchumi wa kati.

Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika Kutekeleza Ilani ya CCM 2015

25.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa dhati ahadi zake kama zilivyobainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano

2016/17-2020/21 na vipaumbele vilivyobainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge la 11 mnamo tarehe 20/11/2015.

26.    Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bajeti hii ni ya nne, niruhusu tujikumbushe kwa uchache maeneo ambayo Mheshimiwa Rais aliyawekea mkazo mkubwa mwanzoni mwa utawala wake. Maeneo hayo ni pamoja na: kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati; kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya Serikali; kuendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja, viwanja vya ndege, reli mpya, bandari na umeme; ujenzi wa viwanda; kuongeza kasi ya kuzalisha ajira na kupunguza umaskini; kuhakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu; kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi; kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za maji, afya na elimu (ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo katika viwango vya ubora wa elimu na stadi za kazi); mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; kuboresha mazingira ya uwekezaji; Kuendeleza utalii; kushughulikia migogoro ya ardhi; kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma; na kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi.
27.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mafanikio mengi yamepatikana katika maeneo niliyoyataja hapo juu, ikiashiria kwamba Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 inatekelezwa ipasavyo.
28.    Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na:
(i)    Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge,  ambapo hadi Aprili 2019 ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 48.9 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422), ujenzi umefikia asilimia 7.12. Mradi huu utakapokamilika utaboresha usafiri nchini na kuwezesha usafirishaji wa mizigo (mazao, mifugo, madini, mazao ya misitu) na abiria kwenda na kutoka nchi jirani zisizo na
bahari (Uganda, Rwanda, Burundi, DRC) na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha biashara na huduma (trade and logistics hub) katika nchi za maziwa makuu. Aidha, mradi huu utapunguza uharibifu wa barabara unaotokana na usafirishaji wa mizigo mizito kwa malori, utapunguza msongamano wa shehena ya mizigo katika bandari ya Dar es Salaam na kutoa fursa za ajira;
(ii)    Ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambapo hadi Aprili 2019 jumla ya ndege sita mpya zimenunuliwa na kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga nchini (Dar es Salaam, Mwanza, Bukoba, Kigoma, Tabora, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songea, Mtwara, Arusha, Mpanda) na kimataifa (Hahaya – Comoro, Lusaka, Harare, Entebbe, Bujumbura). Aidha, ndege nyingine mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Bombadier Q400 zinatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka 2019. Hivi karibuni, ATCL inatarajiwa kuanza safari kwenda Mumbai (India), Johannesburg (Afrika Kusini) na Guangzhou (China). Kuimarishwa kwa usafiri wa anga kutasaidia sana kukuza biashara na sekta ya utalii nchini;
(iii)    Ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) na miundombinu yake katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka umekamilika;
(iv)    Ujenzi wa barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami, ikiwemo daraja la juu la Mfugale katika makutano ya TAZARA; ujenzi wa barabara ya juu yenye ngazi tatu (ubungo interchange) katika makutano ya Ubungo; barabara ya njia nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi Kibaha (km 19); daraja la Magufuli katika mto Kilombero; na kuanza ujenzi wa daraja jipya la Selander jijini Dar es Salaam ikijumuisha barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2;
(v)    Ujenzi wa meli mpya za kubeba mizigo na abiria kwenye Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa;

(vi)    Kukamilika kwa upanuzi wa gati namba moja, kuanza ujenzi wa gati namba mbili, na kuendelea na ujenzi wa sakafu ngumu katika gati la kupakua na kupakia magari katika bandari ya Dar es Salaam. Upanuzi huu utawezesha meli kubwa kuingia na kutoka bandarini kwa ajili ya kushusha na kupakia mizigo;
(vii)    Ujenzi wa mradi wa kihistoria wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika Mto Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 ambapo ujenzi wa miundombinu wezeshi imekamilika na mkandarasi wa kutekeleza ujenzi huo ameshapatikana. Mradi huu utaiwezesha nchi yetu kuwa na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ambao ni wa lazima katika jitihada na dhamira yetu kama Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda. Mradi huu pia utafungua fursa za utalii, uvuvi na kilimo cha umwagiliaji; na
(viii)    Kuendelea na utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini (REA) ambapo hadi Mei 2019, jumla ya vijiji 7,127 vimeunganishiwa umeme.
29.    Mheshimiwa Spika, yapo pia mafaniko makubwa yaliyopatikana katika kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za jamii kwa kipindi cha Awamu ya Tano ambayo ni pamoja na;
(i)    Kuendelea na utekelezaji wa ahadi ya kugharamia elimu msingi (kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne) bila ada na kuongezeka kwa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
(ii)    Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vyuo vikuu ikiwemo kukamilika na kuzinduliwa kwa maktaba ya kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
(iii)    Kuboreshwa kwa huduma za afya katika hospitali za rufaa, mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini. Aidha, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na huduma za kibingwa umeimarika. Vile vile, idadi ya wagonjwa waliokuwa wanapelekwa kutibiwa nje imepungua na hivyo kuokoa fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya matibabu nje ya nchi; na
(iv)    Kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za maji safi mijini na vijijini ambapo katika Jiji la Dar es Salaam umefikia asilimia 85, katika mikoa mingine asilimia 80, miji midogo asilimia 64 na vijijini asilimia 64.8.
30.    Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ni:
(i)    Kutengamaa kwa viashiria vya uchumi jumla ikiwemo ukuaji wa Pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2016 – 2018), kukua kwa sekta ya kilimo kwa wastani wa asilimia 5.3, mfumuko wa bei wa tarakimu moja ya kiwango cha wastani wa asilimia 4.7 katika kipindi hicho, utulivu wa thamani ya shilingi, na kupungua kwa kiwango cha umaskini kutoka asilimia 28.2 hadi asilimia 26.4.
(ii)    Serikali kuhamia makao makuu ya nchi, Dodoma na kuendeleza eneo la Mji wa Serikali kwa kujenga majengo 23 ya ofisi za wizara zote na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na miundombinu yake (umeme, maji, barabara).
(iii)    Kudhibiti utoroshaji na uuzaji wa madini nje ili kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017, ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la migodi ya Tanzanite Mirerani na kuanzisha masoko ya madini;
(iv)    Kuanza utekelezaji wa Mkakati wa Kuharakisha Maendeleo ya viwanda Nchini (Fast Tracking Industrialization Strategy). Aidha, sekta binafsi pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii zimewekeza kwenye miradi ya viwanda ambapo mifuko hiyo inaendeleza miradi 7 kati ya miradi 25;
(v)    Mifumo ya kielektroniki ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato imeimarishwa;
(vi)    Usimamizi wa fedha za Serikali umeimarishwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina;

(vii)    Kuimarishwa kwa taasisi za umma na zile ambazo Serikali ina hisa. Serikali imeendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu zaidi utendaji katika mashirika ya umma ili kuhakikisha kuwa michango na gawio stahiki inatolewa kwa Serikali. Katika kuimarisha mashirika ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa, Serikali imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na mashirika mengi ambayo yalikuwa hayatoi gawio na michango stahiki kwa Serikali kuanza kufanya hivyo. Mwaka 2015/16 kulikuwa na mashirika 13 tu yaliyotoa gawio kwa Serikali kiasi cha shilingi bilioni 119.2 na sasa yameongezeka kufikia mashirika 28 ambayo hadi Mei 2019 yalikuwa yametoa gawio la jumla ya shilingi bilioni 497.5.
(viii)    Serikali imefanya majadiliano yenye maslahi kwa Taifa na baadhi ya makampuni ikiwemo kampuni ya “Airtel Tanzania” ambayo yameleta mafanikio yafuatayo: Umiliki wa hisa za Serikali kuongezeka kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 bila kuzilipia, Mwenyekiti wa Bodi na Afisa Mkuu wa Ufundi (Chief Technical Officer) kuteuliwa na Serikali, Kampuni kuilipa Serikali shilingi bilioni moja kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitano ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3 kimeshalipwa kwa kipindi cha mwezi Aprili, Mei na Juni 2019, Kupatikana kwa kiasi cha dola za Marekani milioni moja kutoka kwa Mwenyekiti wa “Bharti Airtel” kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility) ambazo zimeelekezwa kujenga hospitali mpya ya kisasa Dodoma, Kufutwa kwa madeni na madai ya “Bharti Airtel” kwa Airtel (T) kiasi cha shilingi bilioni 937 (Dola milioni 407.38), na Serikali kupata gawio maalum kutoka mapato ghafi ya Airtel Tanzania kwa mwaka 2019; na
(ix)    Mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambapo ripoti ya uwazi ya kimataifa (Transparency International) ya mwaka 2018 imeonesha Tanzania imeshika nafasi ya 16 kwa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ikilinganishwa na nafasi ya 27 mwaka 2015.
31.    Mheshimiwa Spika, kwa matokeo haya niliyoeleza, ni wazi kabisa kuwa Taifa letu linakwenda mbele chini ya Serikali hii ya tano ya CCM na liko katika mwelekeo sahihi (moving forward in the right direction). Serikali ya CCM chini ya Jemadari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inawashukuru sana wananchi wote wa Tanzania waliotimiza wajibu wao wa msingi kwa kulipa kodi ipasavyo na hivyo kuwezesha Taifa kupata mafanikio hayo makubwa sana katika kipindi kifupi. Wananchi wamejitoa na kuonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kushiriki kwenye ujenzi wa Tanzania mpya. Mafanikio haya pia ni matunda  mazuri ya kutunza nidhamu katika usimamizi wa uchumi, udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato na matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma. Bajeti hii ninayowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu itaendelea kutekeleza malengo ya Serikali kama yalivyoanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17-2020/21.
III.    SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2019/20 Shabaha za Uchumi Jumla
32.    Mheshimiwa Spika, Shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2019/20 ni kama ifuatavyo:-
(i)    Pato la Taifa kukua kwa asilimia 7.1 mwaka 2019 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.0 mwaka 2018;
(ii)    Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3.0 hadi 4.5 katika kipindi cha muda wa kati;
(iii)    Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 14.3 mwaka 2018/19;
(iv)    Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.1 mwaka 2018/19;
(v)    Matumizi ya Serikali kufikia asilimia 22.7 ya Pato la Taifa    mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 21.6 mwaka 2018/19; na
(vi)    Nakisi ya bajeti inakadiriwa kufikia asilimia 2.3 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 2.0 mwaka 2018/19.
Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
33.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali imekusudia kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuiwezesha kugharamia shughuli za Serikali ikiwemo miradi mikubwa ya miundombinu na huduma za jamii. Katika kufanikisha azma hii, Serikali itatekeleza sera zifuatazo:
(i)    Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogo na za kati ili kupanua wigo wa kodi na mapato mengine ya Serikali;
(ii)    Kurekebisha viwango vya kodi kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje;
(iii)    Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi;
(iv)    Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato, pamoja na kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu kwa mlipakodi;
(v)    Kuimarisha makusanyo yasiyo ya kodi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA;
(vi)    Kuendelea kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na wakala, taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na
(vii)    Kuiongezea Mamlaka ya Mapato ya Tanzania uwezo hususan watumishi, vitendea kazi bora na mafunzo ili kutambua na kudhibiti mbinu za ukwepaji kodi.
34.    Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya makadirio ya mapato ya ndani, Serikali imeandaa mikakati mahsusi ya kiutawala itakayotekelezwa katika kipindi cha muda wa kati. Mikakati hiyo inajumuisha:
(i)    Kuongeza ufanisi katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi za ndani kwa kutekeleza Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya
Ndani    (Integrated    Domestic    Revenue    Admistrative    System- IDRAS);
(ii)    Kupanua wigo wa kodi kupitia utambuzi na usajili wa walipakodi wapya pamoja na kuendelea na zoezi la urasimishaji wa sekta isiyo rasmi;
(iii)    Kuwekeza kwenye maeneo ambayo Serikali inaweza kupata mapato zaidi hususan katika uvuvi wa bahari kuu kwa kujenga bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli za uvuvi;
(iv)    Kuimarisha uwezo wa ufuatiliaji na udhibiti wa uhamishaji wa faida unaofanywa na kampuni za kimataifa;
(v)    Kuimarisha usimamizi wa misamaha ya kodi kwa kuhakikisha inaelekezwa kwenye miradi inayokusudiwa;
(vi)    Kuhakikisha kuwa maduhuli yote yanapitia katika Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato; na
(vii)    Kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika taasisi za Serikali ili kuhakikisha kuwa michango stahiki ya taasisi za umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali inawasilishwa kwa wakati.
35.    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa misaada na mikopo nafuu kutoka nje, Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali itaendeleza mazungumzo na Washirika wa Maendeleo ili kila upande uzingatie misingi na kanuni za ushirikiano wa maendeleo pamoja na kuendeleza majadiliano ya kimkakati (Strategic Dialogue) na kumaliza tofauti za kisera au kimtazamo pindi inapojitokeza, pasipo kuathiri utoaji wa fedha za utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.
36.    Mheshimiwa Spika, kuhusu mikopo ya kibiashara ya ndani na nje, Serikali itaimarisha uhamasishaji wa wadau katika soko la ndani kwa lengo la kuimarisha ushiriki wao katika minada ya dhamana za Serikali. Aidha, jitihada zinafanyika ili kuvutia wawekezaji mbalimbali kutoka nje
ya nchi wenye nia ya kuikopesha Serikali ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa uchumi wa Taifa letu.
Sera za Matumizi
37.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya matumizi hususan katika miradi ya maendeleo. Lengo kuu ni kuwa na matumizi bora ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya fedha. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia kuongezeka kwa malimbikizo ya madai kwa Serikali. Pia, Serikali itaendelea kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yenye kuchochea ukuaji wa uchumi.
Maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2019/20
38.    Mheshimiwa Spika, katika Hotuba niliyoiwasilisha asubuhi kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20, niliainisha vipaumbele kwa mwaka 2019/20 ambavyo vitatekelezwa kwa kuzingatia umuhimu wa pekee wa kulinda mazingira nchini (environmental sustainability). Bajeti hii inalenga kutekeleza vipaumbele hivyo kama ifuatavyo:
(i)    Viwanda na kilimo: Katika kuendeleza azma ya kujenga uchumi wa viwanda, katika mwaka 2019/20 Serikali itajikita kuvutia uwekezaji zaidi kwenye viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini kama vile mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na ziada kwa ajili ya kuuza nje, pamoja na kuongeza fursa za ajira. Vile vile kama wote tunavyofahamu, sekta ya kilimo (mazao,  uvuvi, mifugo na misitu) ni muhimu sana kwa uendelezaji wa viwanda Tanzania kwa kuwa sehemu kubwa ya malighafi za viwanda zinatokana na kilimo. Katika kuimarisha sekta hii, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) hususan kuhakikisha upatikanaji wa
mbegu bora, pembejeo, huduma za ugani, masoko, miundombinu wezeshi na tafiti, ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha zaidi kwenye maeneo wezeshi kwa kilimo na kutoa nafuu za kikodi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha bodi za mazao, kuboresha na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya mazao ili kuviwezesha kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye shughuli mbalimbali za kilimo na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya mazao.
(ii)    Ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu: Licha ya kutilia mkazo kuongeza ukuaji wa sekta kuu za uchumi zinazotegemewa na kuajiri Watanzania wengi, bajeti ya 2019/20 itaelekezwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu na ujuzi, chakula na lishe bora na huduma za maji safi na salama. Aidha, kupitia bajeti hii, msukumo utawekwa katika kuongeza ubora wa nguvukazi ili iendane na mahitaji ya soko la ajira
(iii)   Uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji: Bajeti hii imeweka msisitizo mkubwa katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan reli, bandari, nishati, barabara, madaraja, na viwanja vya  ndege. Aidha, Serikali itaendelea kupitia na kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. Napenda niwahakikishie wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itaanza kutekeleza kwa nguvu zaidi mpangokazi wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint for the Regulatory Reforms to improve the Business Environment) ili mazingira ya biashara nchini yawe rafiki zaidi na yenye gharama nafuu.
(iv)    Ufuatiliaji na tathmini Bajeti hii pia inakusudia kuimarisha zaidi ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo  katika ngazi zote. Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi wa
ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti lakini wakati huo huo  kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa kodi unafanyika bila kuathiri biashara. Napenda kuwasisitiza tena watumishi wa TRA kwamba hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe kodi au malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA.
IV.    MABORESHO    YA    MFUMO    WA    KODI,    ADA    NA    TOZO MBALIMBALI
39.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika (stable and predictable). Vilevile yanalenga pamoja na mambo mengine, kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo, viwanda, kukuza ajira, na kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kuanza kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta baadhi ya tozo na ada, kupunguza na kuondoa muingiliano katika kutoza tozo hizo. Marekebisho yanayopendekezwa yanahusu Sheria zifuatazo:-
(a)    Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
(b)    Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
(c)    Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
(d)    Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;
(e)    Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168;
(f)    Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
(g)    Sheria ya Bajeti, SURA 439;

(h)    Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali;
(i)    Kuanza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali;na
(j)    Hatua za Kisera na Kiutawala katika Kuboresha ukusanyaji wa mapato.
(a)    Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
40.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:-
(i)    Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye makasha yenye majokofu (HS Code 8418.69.90) yanayotumika kwenye Kilimo cha Kisasa cha mboga mboga (horticulture) kwa wakulima watakaoingiza makasha hayo kutoka nje ya nchi kwa matumizi ya kilimo. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika uzalishaji na kuhamasisha kilimo cha kisasa cha mboga mboga nchini;
(ii)    Kufanya marekebisho kwenye Kifungu cha 68(3)(d) ili kisihusishe uuzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje ya nchi. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wauzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje ya nchi kuendelea kufanya biashara hiyo kwa kadri ya kibali kitakavyotolewa na Serikali;
(iii)    Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifaa vya kukaushia nafaka (Grain Drying Equipment HS Code 8419.31.00). Msamaha huu unatarajiwa kutoa unafuu kwenye gharama za kukausha nafaka kwa ajili ya kuzihifadhi. Aidha hatua hii itachochea ukuaji wa kilimo cha mazao ya nafaka;
(iv)    Kupunguza kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kutoka asilimia kumi na nane (18) hadi asilimia sifuri (0) kwenye huduma ya umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania Zanzibar ili kuwapunguzia gharama za maisha wananchi wa Tanzania Zanzibar. Serikali iliridhia na kuelekeza kuwa umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania Visiwani utozwe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri;
(v)    Kutoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa vilainishi vya ndege vinavyoingizwa nchini na waendeshaji wa ndani, Shirika la ndege la Taifa, au mashirika ya ndege yanayotambulika katika Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga (Bilateral Air Services Agreements) kwa Kufanya marekebisho ya Sehemu ya Pili ya Jedwali la Misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani katika kipengele cha 11. Hatua hii itawezesha nchi yetu kusaini Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo ilishindikana kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo;
(vi)    Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye tiketi za ndege, vipeperushi, kalenda, shajara, karatasi zenye nembo na sare za wafanyakazi zilizowekwa nembo ya Shirika husika la ndege, kwa kufanya marekebisho ya Sehemu ya Pili ya Jedwali la Misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kuongeza kipengele kipya kinachotoa msamaha pale vinapoingizwa nchini na mashirika ya ndege yanayotambulika katika Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga. Hatua hii itawezesha nchi yetu kusaini Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo ilishindikana kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo; na
(vii)    Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani uliokuwa unatolewa kwenye taulo za Kike (HS Code 9619.00.10) kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha wafanyabiashara. Aidha, wakati Serikali ilipoweka msamaha huu ilitarajia kwamba wazalishaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi.
Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,646.7
(b)    Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
41.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
(i)    Kupunguza kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax) kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia mwaka 2019/20 hadi mwaka 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike. Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano (Performance Agreement) na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali. Vile vile hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wake ndani ya nchi;
(ii)    Kusamehe Kodi ya Zuio inayotozwa kwenye gharama zinazoambatana na mikopo (mfano ada za bima, gharama ya usimamizi, na uandaaji wa mkopo, na ada nyingine zinazoendana na gharama za mkopo) kwa mikopo inayotolewa na Benki, Taasisi za Fedha za nje na wahisani mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha Serikali kupata mikopo kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi. Aidha, msamaha huu utaiwezesha Serikali kutekeleza miradi yake kwa wakati;
(iii)    Kutoa msamaha wa kutengeneza hesabu ambazo zinatakiwa kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya ukokotoaji wa Kodi ya Mapato kutoka kiwango cha sasa cha shilingi milioni ishirini (20,000,000/=) hadi shilingi milioni mia moja (100,000,000/=). Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa mlipa kodi ya kutafuta mtaalam (Certified Public Acountant) kwa ajili ya kutengeneza hesabu. Aidha, hatua hii inalenga pia kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza mapato ya Serikali; na
(iv)    Kusamehe kodi kwenye mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne (4,000,000/=) kwa wenye vitambulisho vya wajasiriamali na kupunguza kiwango cha chini cha kodi kutoka shilingi laki moja na
nusu (150,000/=) kwa mwaka hadi shilingi laki moja (100,000/=) kwa mwaka kama ilivyofafanuliwa kwenye Jedwali Na. 1 na Na. 2. Lengo la hatua hii ni kupunguza mzigo wa kodi kwa walipakodi wadogo pamoja na kuoanisha viwango vya kodi na kiwango cha chini kinachotakiwa kwa mfanyabiashara kutumia mashine ya kodi ya kielektroniki (EFD) ambacho kwa sasa ni shilingi milioni kumi na nne (14,000,000/=). Aidha, hatua hii inalenga pia katika kusisitiza matumizi ya mashine za kielektroniki (Electronic Fiscal Device- EFD) ili kuwezesha ukokotoaji wa kodi ulio sahihi na kuongeza ulipaji kodi wa hiari.
(c)    Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
42.    Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa (specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Kwa msingi huo wa sheria, napendekeza kutokufanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli. Aidha, hatua hii inazingatia kiwango kidogo cha mfumuko wa bei nchini na azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda, na hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye Sekta ya Viwanda, kuvilinda na hatimaye kukuza ajira na mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa. Hata hivyo, napendekeza kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa kwa bidhaa chache tu kama ifuatavyo:-
(i)    Kupunguza Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana na usindikaji wa matunda (kama ndizi, mabibo, rozela/choya, nyanya, nk) yanayozalishwa hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni punguzo la shilingi 139 kwa lita. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari na pia kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vidogo vidogo vya aina hii. Aidha, bei ya mvinyo huu kwa lita inafanana na bei ya vinywaji baridi;
(ii)    Kutoza Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele za bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinazotambuliwa kwa HS Code 67.03; 67.04 na 05.01. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali;
(iii)    Kusamehe Ushuru wa Bidhaa kwenye vilainishi vya ndege (lubricants) vinavyoingizwa nchini na Shirika la ndege la Taifa au mashirika ya ndege yanayotambulika katika mikataba ya Kimataifa ya huduma za anga. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha nchi yetu kusaini mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo ilishindikana kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo; na
(iv)    Kutoza Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 10 kwenye bidhaa za mabomba na vifaa vya plastiki vinavyotumika kwenye ujenzi wa miradi ya ujenzi wa miundo mbinu ya maji kwa kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo na kutosheleza mahitaji hapa nchini. Hatua hii inahusisha bidhaa za mabomba na plastiki zinazotambuliwa katika HS Code 39.17. Lengo la kuanzisha Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa hizo ni kulinda viwanda na kuongeza fursa za kazi, ajira na mapato ya Serikali.
Hatua za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,955.50.
(d)    Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438
43.    Mheshimiwa Spika; napendekeza kuongeza muda wa ziada wa miezi sita (6) hadi Disemba 2019 kwa walipa Kodi waliokubaliwa kulipa kodi wanazodaiwa kwa utaratibu maalum wa kusamehe malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu (Tax Amnesty on Interest and Penalties) kwa asilimia 100 kwa kufanya marekebisho ya Kifungu cha 70 (2) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 . Hatua hii inapendekezwa kutokana na muitikio mzuri wa walipakodi wakati msamaha huo ulipotolewa mwezi Julai 2018 ambapo dhamira ya Serikali ilikuwa ni kutoa ahueni kwa walipakodi waliokuwa na malimbikizo makubwa yanayoathiri biashara zao.
Hatua hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi inatarajiwa
kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 367,000.

(e)    Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168

44.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kama ifuatavyo:-
(i)    Kuongeza muda wa Leseni za udereva kutoka miaka mitatu (3) ya sasa hadi miaka mitano (5);

(ii)    Kuongeza tozo ya Leseni ya udereva kutoka shilingi elfu arobaini (40,000) kwenda shilingi elfu sabini (70,000); na
(iii)    Kuongeza ada ya kadi ya usajili wa magari kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi elfu hamsini (50,000/=); pikipiki za matairi matatu kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi elfu thelathini (30,000/=) na pikipiki kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi elfu ishirini (20,000/=).

Lengo la mapendekezo haya ni kupunguza gharama za kuchapisha leseni kwa kipindi cha miaka mitatu kwani leseni hizo zinaweza kudumu zaidi ya miaka mitano. Aidha, marekebisho haya pia yanalenga katika kuoanisha gharama za uchapishaji wa leseni na kipindi cha leseni husika.

Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 18,147.0

(f)    Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004
45.    Mheshimiwa Spika, kikao cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya  ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget consultations of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 3 Mei, 2019 mjini Arusha, kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa Mwaka wa Fedha 2019/20. Mapendekezo hayo yanalenga katika kuendeleza viwanda, kukuza ajira na kuboresha maisha ya wananchi katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
46.    Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mawaziri wa Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika mwaka 2018/19.
(i)    Mapendekezo ya hatua mpya za viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo:-
(a)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwenye malighafi ya kutengeneza taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotengenezwa hapa nchini kwa mwaka mmoja. Aidha, Watakaonufaika na punguzo hili ni viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa Tanzania na utaratibu utakaotumika katika kuagiza malighafi hizo ni ule wa kuwapa unafuu wa Ushuru wa Forodha “Duty Remission”. Aidha, Serikali itaendelea kutoza ushuru wa Forodha wa asilimia 25 kwa taulo za watoto (Baby Diapers) za kutoka nje ya nchi. Hatua hii inatarajiwa kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji, ajira na mapato ya Serikali. Aidha ni matarajio ya Serikali kuwa viwanda vinavyonufaika na msamaha huu wa Ushuru wa Forodha vitazalisha bidhaa hizi muhimu kwa afya ya watoto na kuziuza kwa bei nafuu ili watanzania wengi waweze kuzinunua. Malighafi zitakazohusika katika msamaha  huu ni zile zinazotumbulika katika HS Code 3506.91.00; PE Film HS Code 3926.90.90; Super Aborbent Polymer HS Code 3906.90.00; Wet Strength Paper HS Code 4803.00.00; Non Wovens HS Code 5603.11.00; Polyethylene Laminated Non Wovens HS Code 5903.90.00; Spandex HS Code 5402.44.00; na Dust Free Paper Hs Code 4803.00.00;

(b)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito. Hatua hii itawanufaisha wanaofanya shughuli hizo na utaratibu wa “Duty Remission” ndio utatumika katika kuagiza vifaa hivyo. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa gharama na kuhamasisha ukataji na usafishaji wa madini hayo hapa nchini na hivyo kuongeza thamani yake kabla ya kuuzwa. Aidha, hatua hii itaongeza mapato ya Serikali

na ajira. Vifaa vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS Codes 3606.90.00; 6804.10.00; 6813.20.00;
7018.90.00;    7020.00.99;    8202.20.00;    8202.99.00;
8203.20.00; 8205.10.00; 8423.89.90;    8513.10.90; na
9002.19.00;

(c)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye makaratasi (HS Code 4805.11.00 na 4805.19.00) yanayotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya mboga mboga kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika ambapo viwanda vinavyotengeneza vifungashio hivyo tu ndivyo vitakavyonufaika. Lengo la kuondoa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi hizo ni kupunguza gharama ya utengenezaji wa vifungashio ili kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa nje, kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa vifungashio vya aina hii na hatimaye kuhamasisha uuzaji nje wa mboga mboga kwa ajili ya kupata fedha za kigeni;

(d)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya mbegu vinavyotumiwa na wazalishaji wa mbegu hapa nchini. vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes 3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00; 7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00; 6304.91.90; 7607.19.90. Lengo la hatua hii ni kuongeza ubora wa mbegu na pia kuzipa unafuu wa gharama Taasisi zinazozalisha mbegu hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;

(e)    Kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwa utaratibu wa “Duty Remmission” kwenye malighafi (Alluminium Alloys)

zenye HS Code 7606.92.00 zinazotumika katika kutengeneza sufuria (Alluminium pots). Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu hapa nchini, kulinda viwanda vya ndani ili viweze kuongeza uzalishaji wa kutosheleza mahitaji na kuongeza ajira;

(f)    Ili kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa kahawa hapa nchini pamoja na kuongeza mapato ya Serikali napendekeza kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye kahawa inayoagizwa nje ya nchi (HS Code 09.01);
(g)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 125 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja  kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala ya asilimia 10 pekee. Bidhaa hizo ni “Flat -rolled products of iron or Non-alloy steel na Flat –rolled products of other alloy steel.” Bidhaa hizi hutambulika katika HS Codes 7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00; 7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00; 7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la kuweka viwango hivyo vya Ushuru wa Forodha ni kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo na kulinda viwanda vya hapa nchini na ajira;
(h)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala ya asilimia 25 pekee. Ushuru huo unahusu bidhaa zinazotambulika katika HS Code 7212.30.00; 7212.40.00 na 7212.50,00. Hatua hii ina lengo la kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa
hizo    zinapoingizwa    kutoka    nje    (under-invoicing    and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;
(i)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika katika HS Code 7212.60.00 badala ya kutoza ushuru wa asilimia
10 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;

(j)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 pekee. Hatua hii inahusu bidhaa zinazotambulika katika HS codes 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00 na 7210.90.00. Lengo la hatua hiyo ni kuwalinda wazalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini kutokana na ushindani wa nje;

(k)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 badala ya kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye nondo kwa mwaka mmoja. (Reinforment bars and hallow profile). Hatua hii inahusu bidhaa
zinazotambulika    katika    Hs    codes    7213.10.00;
7213.20.00;    7213.99.00;    7214.10.00;    7214.20.00;
7214.30.00;    7214.90.00;    7214.99.00;    7215.10.00;
7215.50.00;    7215.90.00;    7225.90.00;    7225.92.00;
7225.99.00; 7306.30.00; 7306.50.00; 7306.61.00;
7306.69.00; na 7306.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini na kuongeza ajira;

(l)    Kwa kuwa mbogamboga zinalimwa kwa wingi hapa nchini, napendekeza kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mboga mboga (horticultural products)
zinazotambulika    kwenye    HS    codes    0603.11.00;
0603.12.00;    0603.13.00;    0603.14.00;    0603.19.00;
0604.20.00;    0604.90.00;    0701.90.00;    0702.00.00;
0703.10.00;    0703.20.00;    0706.10.00;    0710.10.00;
0710.21.00;    0710.22.00;    0710.30.00;    0714.10.00;
0714.20.00;    0804.30.00;    0804.40.00;    0804.50.00;
0805.10.00;    0805.40.00;    0805.50.00;    0806.10.00;
0807.11.00;    0807.20.00;    0808.10.00;    0808.20.00.
Aidha, hatua hii itaongeza mapato ya serikali; na
(m)    Kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za fito za plastiki zijulikanazo kama PVC Profiles HS Code 3916.10.00; 3916.20.00; 3916.90.00 ambazo hutumika kwa ajili ya kutengenezea fremu za milango, madirisha
n.k. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali.
(ii)    Mapendekezo ya kuendelea na utekelezaji wa viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo;-
(a)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazotambulika kwenye HS codes 4804.11.00; 4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00 na 4804.41.00. Karatasi hizi ni zile zinazozalishwa na kiwanda cha Mufindi;
(b)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye ngano inayotambulika kwa HS Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90. Hatua hii imezingatia kwamba uzalishaji wa ngano katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hautoshelezi mahitaji, na bidhaa hii ni muhimu katika kutengeneza vyakula mbalimbali. Lengo la Serikali ni kuwezesha Viwanda na walaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa ngano waweze kupata vyakula husika kwa bei nafuu na tulivu. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utaendelea kutumika katika kuagiza ngano hiyo ambapo Viwanda vinavyotumia ngano ya aina hii katika uzalishaji ndivyo vinavyohusika katika kutumia kiwango hicho nafuu cha Ushuru wa Forodha. Kutokana na mahitaji makubwa ya ngano katika Jumuia ya Afrika Mashariki na SADC, wakati umefika sasa kwa wananchi kuchangamkia fursa ya Kulima ngano katika maeneo mbalimbali nchini yanayofaa kwa kilimo cha ngano ikiwemo eneo la shamba la Basuto;
(c)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Electronic Fiscal Device) zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00;
(d)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates” (ABL) HS Code 3920.10.90 ambayo hutumika kama malighafi ya kutengeneza dawa ya meno kwenye viwanda vya ndani;
(e)    Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwa utaratibu wa “Duty Remission” kwenye bidhaa ya kutengeneza sabuni
ijulikanayo    kama    RBD    Palm    Stearin    (HS    Code 1511.90.40);
(f)    Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety matches) vnavyotambuliwa kwenye HS code 3605.00.00 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa;
(g)    Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma za misumari zinazotambulika katika HS code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins, corrugated nails, staples other than those of heading 83.05);
(h)    Kutoza ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo (HS code 1601.00.00);
(i)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye chingamu (chewing gum) zinazotambulika katika HS code 1704.10.00;
(j)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye  peremende (HS code 1704.90.00);
(k)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye chokoleti (chocolates) HS code
18.06 kwa mwaka mmoja;
(l)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye biskuti (HS code 1905) kwa mwaka mmoja;
(m)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauces) zinazotambulika katika HS code 2103.20.00;
(n)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye maji (mineral water) yanayotambulika katika HS code 2201.10.00;
(o)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyama (meat and edible meat offal in chapter 2) kwa mwaka mmoja;
(p)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 kwenye mafuta Ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, nazi, karanga, mahindi n.k) kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya kula hapa nchini. Nchi yetu ina fursa kubwa ya kukuza uzalishaji wa bidhaa hiyo. Hivyo, kuna umuhimu wa kuchochea na kuhamashisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na uchakataji wa mafuta ghafi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa hapa nchini. Lengo la hatua hii ni kuongeza ajira mashambani, viwandani na pia kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi. Mafuta ghafi hayo yanatambulika kwenye HS code 1507.10.00; 1508.10.00; 1511.10.00; 1512.11.00; 1513.11.00; 1514.11.00; 1514.91.00; 1515.11.00; 1515.21.00; 1515.30.00;
(q)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (semi- refined, refined/double refined oil) mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, karanga, nazi, mahindi n.k. Ongezeko la Ushuru wa Forodha linatarajiwa kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta hapa nchini na kuongeza ajira viwandani na mashambani. Aidha ongezeko la Ushuru wa Forodha linahusu mafuta yote ya kula yaliyochakatwa yanayoingizwa nchini na
yanayotambulika    kwenye    HS    codes    1507.90.00;
1508.90.00;    1509.90.00;    1510.00.00;    1511.90.10;
1511.90.30;    1511.90.90;    1512.19.00;    1512.29.00;
1513.19.00;    1513.29.00;    1514.19.00;    1514.99.00;
1515.19.00; 1515.20.00; 1515.50.00; 1515.90.00;
(r)    Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye “Gypsum Powder” HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja;
(s)    Kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 100 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji hapa nchini. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha sukari, ajira na mapato ya Serikali;
(t)    Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 kwenye mitumba inayoingia kutoka nje (badala ya asilimia 35 au dola za marekani 0.40 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi kikubwa);
(u)    Kusamehe Ushuru wa Forodha kwenye malighafi,  vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza nguo na viatu vya ngozi. Aidha, Mawaziri wa Fedha wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki wameridhia orodha iliyooanishwa (harmonized list) ya malighafi na vipuri ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kuziwezesha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ziweze kufanya biashara kwa bidhaa za nguo na viatu vya ngozi vitakavyozalishwa ndani ya Jumuiya; na
(v)    Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kutoza Ushuru wa Mauzo nje (Export Levy) wa asilimia
10 kwenye ngozi iliyosindikwa kwa kiwango cha kati (wet blue). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi, kuongeza thamani, na kuongeza ajira katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
47.    Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
(i) Kufanya marekebisho katika kipengele cha 1 (a) Sehemu B  ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CMA, 2004) ili kuingiza vilainishi kwa ajili matengenezo ya ndege (Lubricants for Aircraft), sare (uniforms), kalenda, shajara na peni kwenye orodha inayopata msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye huduma za ndege. Lengo la kutoa msamaha huo ni kuiwezesha nchi yetu kusaini mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo haikuweza kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo.

Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 31,074.0
(g)    Sheria ya Bajeti, SURA 339
48.    Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha utekelezaji wa Miradi Mikubwa yenye manufaa kwa Taifa kama vile Ujenzi wa Miundombinu, Ununuzi
wa Ndege, Mabehewa au Vichwa vya Treni, Miradi ya Umeme n.k, inapendekezwa kurekebisha Kanuni ya 23 ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za mwaka 2015, ili kumpa Mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuongeza muda wa matumizi ya fedha za mwaka wa fedha uliomalizika hususan zinazohusu Miradi ya Maendeleo. Hivi sasa Kanuni hii imeweka ukomo wa miezi mitatu (3) wa kutumia fedha za mwaka wa fedha uliomalizika, ambapo baada ya muda huu wa miezi mitatu (3) kuisha, fedha hizo hupaswa kurejeshwa Mfuko Mkuu wa Serikali. Utaratibu huu wa sasa  wa kurejesha fedha za miradi, Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kumalizika kwa muda wa miezi mitatu (3) unaathiri utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kutokana na kutokuwepo kwa fedha za kulipia Hati za Madai hadi hapo mgao mpya wa fedha utakapotolewa kwenye bajeti ya mwaka mpya wa fedha.
(h)    Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali.
49.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
(i)    Kuanza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa biashara (Blueprint) kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali.
50.    Mheshimiwa Spika, kufuatia matokeo ya mkutano wa Mh. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini uliofanyika ikulu, Dar es salaam, tarehe 7 Juni, 2019, Serikali inapendekeza kufuta au kupunguza ada na tozo hamsini na nne (54) zinazotozwa na Wizara, Idara na taasisi zinazojitegemea ili Kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Hatua hizi ni sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara

(Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Aidha, hatua hii imelenga kuondoa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji baina ya Wizara, Taasisi na Mamlaka za Udhibiti. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 na Matangazo ya Serikali (Government Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-
I.    Mamlaka ya Dawa (TFDA)
(a)    Kufuta tozo za Kushikilia usajili wa dawa za chanjo (Vaccines and Biologicals) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150); dawa za mitishamba (Herbal medicines) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150); vifaa tiba (medical devices) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia moja (100); vitendanishi (diagnostics) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia mbili hamsini (250); chakula kinachotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia moja (100); vipukusi (antiseptics and diagnostics) vinavyotozwa kwa kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=); na tozo za bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi (retention fees for domestic products);

(b)    Kufuta tozo za Kudurufu cheti cha usajili wa vitendanishi inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia moja (100);

(c)    Kufuta tozo za ukaguzi wa maduka mapya ya kuuzia vyakula inayotozwa kwa kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000);

(d)    Kufuta tozo za usajili wa maduka ya reja reja ya dawa za mifugo kati ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) hadi shilingi laki moja (100,000/=);

(e)    kufuta tozo ya ukaguzi wa viwanda vya samaki nchini iliyokuwa inatozwa kwa kiwango cha kati ya shilingi laki

mbili    (200,000/=)    hadi    shilingi    laki    mbili    na    elfu hamsini (250,000/=);
(f)    Kufuta tozo ya ukaguzi wa maduka mapya ya samaki ya shilingi elfu hamsini (50,000/=); na
(g)    Kufuta tozo ya leseni ya mwaka ya biashara ya samaki kati ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) hadi shilingi laki tatu (300,000/=).
Lengo la hatua hizi ni kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na  uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa sheria kwa hiari na kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za TFDA (customer base).
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 2,500.0
II.    Shirika la Viwango Tanzania
Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Shirika la Viwango Tanzania kwa:-
(a)    Kufuta tozo ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) ya maombi ya alama ya ubora (TBS mark);
(b)    Kufuta tozo ya nembo ya ubora (TBS mark guarantee) ya asilimia kumi na tano (15) ya tozo ya gharama za mwanzo za ukaguzi wa ubora (transport costs and overhead fees);
(c)    Kufuta tozo ya dhamana ya cheti cha kutumia nembo ya ubora (TBS mark licence). Tozo hii hutozwa kwa kiwango cha asilimia hamsini (50) ya gharama za usafirishaji na upimaji wa Sampuli kutoka sokoni na viwandani;
(d)    Kufuta tozo ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) ya ununuzi wa fomu ya maombi ya bidhaa zinazotoka nje kwa bidhaa zote;
(e)    Kufuta tozo ya gharama za ugenzi (calibration of equipment based on industrial metrology). Tozo hii hutozwa kulingana na umbali wa sehemu (Kwa mfano Dar es salaam - chini ya umbali wa kilometa 5 kutoka TBS ni shilling elfu kumi (10,000/=); umbali wa kati ya kilometa 5 hadi 7 kutoka TBS ni shilingi elfu hamsini (50,000/=); na umbali wa zaidi ya kilometa 7 kutoka TBS ni shilingi laki moja (100,000/=); na
(f)    Kufuta tozo ya asilimia 0.2 ya gharama ya mzigo na usafirishaji ya udhibiti wa vipodozi, vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kondomu, mabomba ya sindano (syringes), glavu (gloves), pamba (cotton wool) na bendeji (bandage).
Lengo la hatua hii ni kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara na wazalishaji, kupunguza gharama katika uendeshaji wa vifaa vya viwandani na kupunguza tozo za kero.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 2,687.4
Aidha, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwenye eneo la usimamizi wa viwango ambao unajumuisha ubora na usalama wa chakula na vipondozi ili Shirika la Viwango Tanzania (TBS) liendelee kusimamia eneo la chakula na vipodozi kwa ujumla kama ilivyo kuwa tangu mwaka 1975. Hivyo basi, Shirika la Viwango litachukua jukumu la kuunganisha utaratibu wa usajili wa majengo (premises registration), Usajili wa bidhaa (product registration), udhibiti wa bidhaa (certification) na udhibiti wa bidhaa kutoka nje (import inspection) kwa ujumla. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) itaendelea kusimamia madawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi ili kuongeza ufanisi katika eneo hili.
III.    Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani, Sura 182 kwa kufuta tozo zifuatazo:-
(a)    Kufuta tozo ya huduma ya kusitisha kibali cha awali na kutoa kibali kipya inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani hamsini (50);
(b)    Kufuta tozo ya huduma ya kubadilisha taarifa za kibali inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani hamsini (50);
(c)    Kufuta tozo ya usajili wa kampuni ya Wakala wa Forodha (Clearing Agent) inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia tano (500) kila kipindi cha usajili;
(d)    Kufuta tozo ya huduma ya kubadilisha taarifa za usajili inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia moja (100) kila kipindi cha usajili;

(e)    Kufuta tozo ya huduma ya ukaguzi wa dharura inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia tatu (300) kwa kila ukaguzi;
(f)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili (maintenance fee) kwa viwanda vya magodoro inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kila mwaka;
(g)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa viwanda  vya rangi inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;
(h)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa viwanda  vya nguo inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;

(i)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa viwanda  vya ngozi inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;

(j)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa viwanda  vya plastiki inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;

(k)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa viwanda vinginevyo vikubwa inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;

(l)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa viwanda vidogo vidogo inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia mbili hamsini (250) kwa mwaka;

(m)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa wasambazaji wakubwa inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka; na

(n)    Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa wasambazaji wa kati inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia tano (500) kwa mwaka.

Aidha, napendekeza pia kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani Sura 182, ili kurekebisha viwango vya tozo kama ifuatavyo:-

(a)    Kutoza tozo ya shilingi elfu arobaini (40,000/=) ya usajili wa kemikali kwa kila kemikali kwa kipindi cha usajili badala ya Dola za Kimarekani ishirini (20);

(b)    Kutoza tozo ya shilingi laki mbili (200,000/=) kwa wafanyabiashara wakubwa na shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa wajasiriamali wadogo kwa kila cheti cha usajili (Certificate holder registration);

(c)    Kutoza tozo ya shilingi laki mbili (200,000/=) badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100) kwa wafanya biashara wakubwa na shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa wafanyabiashara wadogo kwa Usajili wa eneo la kuhifadhia kemikali (Premises registration);

(d)    Kutoza tozo ya shilingi laki tatu (300,000/=) kwa siku kwa kila mtu ya kuchambua kemikali chakavu badala ya Dola za Kimarekani mia tatu (300);

(e)    Kutoza tozo ya shilingi laki mbili (200,000/=) ya kuainisha na kuidhinisha njia ya kuteketeza kemikali badala ya Dola za Kimarekani mia tano (500);

(f)    Kutoza tozo ya shilingi laki tatu (300,000/=) kwa kila siku kwa kila mtu ya kusimamia kupakia, kusafirisha, kushusha na kuteketeza kemikali chakavu badala ya Dola za Kimarekani mia tatu (300);

(g)    Kutoza tozo ya shilingi laki tatu (300,000/=) ya ukaguzi wa maghala na sehemu za kuhifadhia kemikali badala ya Dola za Kimarekani mia mbili (200);

(h)    Kutoza tozo ya shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000/=) kwa kila siku kwa kila mtu kwa tathmini ya njia za Usafirishaji na ukaguzi wa dharura (Transportation Routes assessment and emergency inspection) badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100);

(i)    Kutoza tozo ya shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000/=) kwa siku kwa kila mtu kwa kusindikiza kemikali hatarishi badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100); na

(j)    Usafirishaji wa kemikali hatarishi na kemikali zingine ndani    na    nje    ya    nchi    utatozwa    tozo    kama zilivyoainishwa kwenye Jedwali Na. 3 hapa chini:- Jedwali Na 3.

Aidha, ili kutimiza matakwa ya sheria ya kutumia fedha za kitanzania, tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa dola za kimarekani zitatozwa kwa fedha za Kitanzania isipokuwa kwa shehena za kemikali zinazoenda nje ya nchi (On-transit). Lengo la hatua hizi ni kupunguza wingi na ukubwa wa tozo ili kuweka mazingira bora ya biashara nchini. Aidha, mizigo ya kemikali inayopitishwa katika bandari ya Dar es salaam itaongezeka na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.

Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 450.0
IV.    Wizara ya Mifugo na Uvuvi- Sekta ya Mifugo
Napendekeza kufuta tozo mbalimbali kwenye Sekta ya mifugo kama ifuatavyo:-

(a)    Kufuta tozo ya shilingi 5,000 ya vibali vya vyombo vya kusafirisha maziwa chini ya lita 51;

(b)    Kufuta tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa vituo vya kukusanyia maziwa lita 201 kwa siku;

(c)    Kufuta tozo ya shilingi 5,000 ya usajili wa wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 kwa siku;

(d)    Kufuta    tozo    ya    shilingi    500,000    ya    usajili    wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa;

(e)    Kufuta tozo ya shilingi 15,000 ya usajili wa wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama;

(f)    Kufuta tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa wafugaji wa kati wa mifugo ya nyama;

(g)    Kufuta tozo ya shilingi 75,000 ya usajili wa wafugaji wakubwa wa mifugo ya nyama;

(h)    Kufuta tozo ya shilingi 20,000 ya usajili wa wasimamizi wa minada ya awali;

(i)    Kufuta tozo ya shilingi 30,000 ya usajili wa wasimamizi wa minada ya upili na mipakani;

(j)    Kufuta tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa minada ya upili na mipakani;

(k)    Kufuta    tozo    ya    shilingi    30,000    ya    usajili    wa wafanyabiashara wa minada ya awali;

(l)    Kufuta    tozo    ya    shilingi    60,000    ya    usajili    wa wafanyabiashara wa minada ya upili na mipakani;

(m)    Kufuta tozo ya shilingi 100,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa nyama na bidhaa zake nje ya nchi;

(n)    Kufuta tozo ya shilingi 1,000 ya kibali cha kusafirisha kuku nchini (vifaranga 100 kwa siku moja); na

(o)    Kufuta tozo ya shilingi 200 ya kibali cha kusafirisha kuku mkubwa nchini.

Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha takribani shilingi milioni 16,689.8
V.    Wizara ya Maliasili na Utalii
Napendekeza kufuta ada ya Leseni ya kufanya biashara ya Utalii inayohusisha uwindaji wa kitaalamu (professional hunting) iliyokuwa inatozwa kwa dola za kimarekani mia mbili (USD 200) kwa raia wa Tanzania na dola za kimarekani elfu moja (USD 1000) kwa raia wa kigeni. Lengo la hatua hii ni kupunguza tozo zinazotozwa katika sekta ya utalii, na kuvutia watalii. Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha takribani Dola za Kimarekani elfu themanini (USD 80,000).

VI.    Wizara ya Maji
Napendekeza kufuta ada ya matumizi ya maji kwa watumiaji wenye visima nyumbani ambayo ilikuwa inatozwa kuanzia shilingi laki moja (100,000/=) na kuendelea kulingana na matumizi ya maji. Lengo la kufuta tozo hiyo ni kupunguza gharama kwa wananchi wanaochimba visima vya maji kwa matumizi binafsi nyumbani na kuwezesha upatikanaji wa maji hayo kwa gharama nafuu. Hata hivyo, ili kudhibiti uchimbaji holela wa visima, itabidi visima hivyo viendelee kusajiliwa na Bodi za Maji za Mabonde.

Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 1,961

Aidha, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (BLUEPRINT). Lengo ni kuendelea kuweka mazingira bora ya kuvutia uwekezaji, katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Hatua hii inatoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha biashara mpya zitakazo ongeza ajira na kukuza uchumi. Kwa kuzingatia kuwa, Serikali imewekeza katika kuboresha mazingira ya udhibiti wa mazingira ya biashara, kupitia mpango wa BLUEPRINT, hivyo basi, ni matarajio na wito wa Serikali kwamba wawekezaji wa ndani na nje, watachangamkia fursa hii kwa kuanzisha na kuendeleza uwekezaji mpya ili kukuza faida za biashara na kuweza kulipa kodi stahiki kwa hiari na kuongeza mapato ya Serikali.

(j)    Hatua    za    Kisera    na    Kiutawala    katika    Kuboresha ukusanyaji wa mapato

51.    Mheshimiwa Spika, napendekeza kuweka utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini ambapo wananchi wa kawaida wataruhusiwa kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia Wakala wa Forodha (Clearing and Forwarding Agents). Hata hivyo, utaratibu huu hautahusisha mizigo inayopitishwa hapa nchini kwenda nje ya nchi (Transit Cargo). Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania itaandaa utaratibu wenye kueleweka kwa urahisi ili kuwawezesha Wananchi kugomboa mizigo yao kwa gharama nafuu zaidi na bila kuchelewa.

52.    Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza kuchukua hatua mbalimbali za Kisera na Utawala kwa lengo la kuimarisha na kurahisisha ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-

(i)    Ili kuondoa malalamiko ya wafanyabiashara dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeamua kuanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko na taarifa za kodi (Office of Tax Ombudsman) ambacho kitaratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, kitengo hiki kitahusisha kupokea na kupitia malalamiko ya taarifa za Kodi zitakazotolewa na walipakodi au watu wenye nia njema. Baadhi ya majukumu ya Kitengo hiki ni kama yafuatayo:-


(a)    Kupokea malalamiko ya rushwa dhidi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;

(b)    Kupokea malalamiko ya ukadiriaji wa Kodi na uthamanishaji wa bidhaa usio wa haki wala uhalisia dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;
(c)    Kupokea malalamiko ya matumizi ya nguvu katika ukusanyaji kodi dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;

(d)    Kupokea malalamiko ya ufungaji wa biashara bila kufuata sheria na taratibu dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania; na

(e)    Kupokea malalamiko pamoja na kero nyingine zinazofanana na hayo dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
(ii)    Ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kodi za ndani, serikali inakamilisha manunuzi ya mfumo unganishi wa kielektroniki (Intergrated Domestic Revenue Adminstration System- IDRAS) katika kukusanya kodi na mapato yasiyo ya kodi ili kuleta uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Pia mfumo huu utarahisisha ulipaji wa kodi na kupunguza rushwa miongoni mwa watumishi wasio waaminifu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;
(iii)    Kuendelea kusimamia matumizi ya mfumo wa kukusanyia kodi wa kielektroniki (Electronic Fiscal Device Management System) ambao umefanyiwa maboresho makubwa na kuanza kazi tangu tarehe 1 June, 2019, ili kudhibiti na kubaini udanganyifu unaofanywa katika matumizi ya mfumo huo. Aidha, hatua hii itadhibiti uvujaji wa mapato katika urejeshaji wa kodi ( Tax refund), utoaji wa risiti bandia, n.k;
(iv)    Kutokana na wimbi la vijana wengi kujihusisha na michezo ya kubahatisha na kusahau majukumu ya ujenzi wa taifa, Serikali ikishirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imebuni na kutengeneza mfumo maalum ambao utatumika kudhibiti uchezaji

wa michezo hii (Responsible Gaming). Pia, Mfumo huu utatumika kudhibiti udanganyifu ambao unafanywa na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha ili Serikali ipate mapato yake halali;
(v)    Kutokana na malalamiko ya walipa kodi kuhusu ukadiriaji wa kodi na uthaminishaji wa bidhaa usio na haki wala uhalisia, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanzisha dawati la kushughulikia mapingamizi ya makadirio ya kodi ambapo pingamizi za uthamanishaji na utambuzi litashughulikiwa ndani ya masaa ishirini na nne (24); na
(vi)    Kutoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita (6) kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). Hatua hii inatofautiana na hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN anaanza kufanyiwa tathmini (tax assessment) ya mapato yake ya biashara na kutakiwa kulipa kodi. Hatua hii itawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wapya kupata muda wa kujiandaa na mahitaji yanayotakiwa katika shughuli wanazofanya na kuondoa usumbufu au dhana ya woga wakati wa kuanzisha biashara. Mfano kuna mahitaji ya Leseni ya biashara na vibali vingine muhimu.

(k)    Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.

53.    Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2019, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.

V.    SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2019/20

54.    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2019/20, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 33.11 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 23.05, sawa na asilimia
69.6 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 19.10 sawa na asilimia 12.9 ya Pato la Taifa. Mapato yasiyo ya kodi kwa mwaka 2019/20 yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 3.18 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Shilingi bilioni 765.5.

55.    Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni
4.96 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 3.46 ni  kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Shilingi bilioni 1.50 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.32 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.

56.    Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 2.78 ambayo ni asilimia 8 ya bajeti. Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo shilingi trilioni 2.31; Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 199.5; na Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) shilingi bilioni 272.8.

57.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 33.11 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 20.86 zimetengwa kwa  ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.0 ya bajeti, ikijumuisha Shilingi trilioni 9.72 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na shilingi trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara. Aidha, shilingi trilioni 3.58 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (Other Charges-OC) ikijumuisha shilingi bilioni
460.5  kwa  ajili  ya  matumizi  yatokanayo  na  vyanzo  vya  ndani  vya

Halmashauri. Aidha, kwa mwaka 2019/20, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

58.    Mheshimiwa Spika, matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 12.25, sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote, ambapo kiasi cha Shilingi trilioni 9.74 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.51 ni fedha za nje. Kati ya fedha za maendeleo zilizotengwa, shilingi trilioni 2.48 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge; shilingi trilioni 1.44 ni kwa ajili ya mradi wa kufua umeme Mto Rufiji; shilingi bilioni 788.8 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na REA; shilingi bilioni 450 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na shilingi bilioni 288.5 kwa ajili ya elimu msingi bila ada. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme.

59.    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2019/20 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali A.

VI.    HITIMISHO
60.    Mheshimiwa Spika, bajeti ni nyenzo ya kufikia matarajio ya wananchi wetu. Hivyo, katika kuandaa bajeti hii, Serikali iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo, Kamati ya Bunge ya Bajeti, wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi, wananchi wa kawaida, na wataalam wa kodi hususan wale walioshiriki vikao vya kazi vya kikosi kazi cha maboresho ya kodi (Task Force and Think Tank) kujadili na kushauri juu ya mapendekezo ya maboresho ya kodi na tozo mbalimbali. Baadhi ya wadau walituletea maoni na ushauri kwa maandishi au barua pepe. Nakiri kuwa walitupatia mrejesho ambao umesaidia kuboresha será na vipaumbele vya nchi yetu kwa mwaka 2019/20 na siku zijazo. Napenda kwa niaba ya Serikali kuwashukuru sana kwa michango hiyo mizuri ambayo tumejitahidi kuizingatia. Ni matarajio ya Serikali kwamba wadau hao wataendelea kufanya hivyo katika mchakato wa bajeti zitakazofuata.

61.    Mheshimiwa Spika, bajeti ya 2019/20 inahusu kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa jamii na hatimaye kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi. Hususan, bajeti hii imelenga:
(i)    Kuimarisha na kujenga miundombinu ya kisasa ili kuongeza uwezo wa Taifa katika uzalishaji viwandani hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini na kutoa huduma bora (afya, elimu na maji) kwa wananchi. Aidha, miundombinu hiyo itasaidia kuongeza biashara nchini, kikanda na kimataifa;
(ii)    Kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na uwekezaji kwa kushughulikia changamoto zilizobainishwa katika mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint);
(iii)    Kuimarisha kilimo (uzalishaji wenye tija na masoko ya mazao, ufugaji, uvuvi, na misitu) kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa sekta hii katika uchumi wa Taifa (chakula, ajira, kipato cha mwananchi, mchango katika fedha za kigeni na muunganiko wa sekta hii na maendeleo ya viwanda);

(iv)    Kudumisha amani na usalama katika Taifa; na Kujenga misingi ya Taifa kujitegemea kiuchumi
62.    Mheshimiwa Spika, safari ya kuijenga Tanzania mpya imeiva lakini haitakuwa rahisi hasa tukizingatia mabadiliko yanayoendelea  katika uchumi wa dunia, ushindani mkali wa kibiashara, mabadiliko ya haraka ya teknolojia na demografĂ­a na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, bahati nzuri ni kuwa, katika historia ya nchi yetu, Watanzania ni watu jasiri katika mapambano dhidi ya changamoto zinazojitokeza na kila wakati zilipojitokeza tulizishinda kwa kutumia ubunifu na nguvu ya umoja wa Watanzania.
63.    Mheshimiwa Spika, hivi sasa tuko imara zaidi chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Uchumi wetu unaendelea kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka 2018 ulikua kwa asilimia 7.0 na kiwango cha umaskini wa mahitaji  ya  msingi kinazidi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia
26.4 mwaka 2017/18. Naamini pasipo shaka yoyote kwamba kwa umoja wetu, uongozi makini, kufanya kazi kwa bidii na kwa kutumia rasilimali za nchi yetu vizuri, tutaijenga Tanzania mpya, ambayo itakuwa kitovu kikuu cha uchumi (Economic hub) katika ukanda wa Afrika Mashariki katika muda usiozidi miongo miwili ijayo.
64.    Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa hotuba hii, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo kwa misaada na mikopo nafuu wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini. Katika bajeti ya mwaka 2019/20, Washirika wa Maendeleo kwa pamoja wanatarajia kuchangia jumla ya shilingi trilioni 2.78. Naomba niwatambue kwa kuwataja mmoja mmoja: Nikianza na nchi za Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, Uingereza, na Uswisi. Aidha, zipo taasisi za kimataifa ambazo ni: Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia, Arab Bank for Economic Development in Afrika (BADEA), Global Fund, Kuwait Fund, Abu Dhabi Fund, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), OPEC Fund, Global Environmental Facility (GEF), Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mfuko wa kukinga Hatari ya

Kimazingira (GRMF), Climate Development Special Fund, African Legal Support Facility (ALSF), Dignity, Global Agriculture and Food Security Program (GAFSP),na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF, IFAD, UNDP, UNFPA, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), na United Nations Environment Programme (UNEP). Napenda pia kutambua uhusiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Ni matarajio yetu kuwa misaada ya kiufundi na fedha zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi kilichoahidiwa. Nasi kwa upande wa Serikali tunaahidi kutumia misaada hiyo kama ilivyokusudiwa.
65.    Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuwahimiza Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na taasisi za  kimataifa hapa nchini Tanzania waongeze nguvu kukuza biashara kati ya nchi zao na nchi yetu na kuhamasisha wenye mitaji toka nchi zao kuja kuwekeza hapa Tanzania. Tanzania ni salama kwa uwekezaji wenye faida kwao na kwetu. Aidha, wafanye jitihada zaidi kuhamasisha watalii kuja kujionea vivutio vya utalii, ambavyo ni fahari ya Tanzania.
66.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua na kuthamini michango yao katika maendeleo ya Taifa letu ili mradi isiambatane na masharti yanayohatarisha uhuru wa Tanzania (national sovereignity), au kwenda kinyume na mila na desturi zetu. Hata pale ambapo Serikali au mihimili mingine imefanya maamuzi ambayo hawakubaliani nayo, ni vema na haki washirika wetu wa maendeleo watupe muda wa kuyatafakari na kujadiliana nao kwa staha badala ya kuishinikiza Serikali ibadili uamuzi wake ndipo watoe fedha, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.
67.    Mheshimiwa Spika, kwa Watanzania wenzangu, napenda kuwasisitiza tuendelee kushikamana katika kuijenga Tanzania mpya. Tuwe wazalendo na tena tukae macho daima kulinda na kutetea maslahi ya Taifa letu. Tuongeze bidii kufanya kazi. Enzi za kutegemea wajomba hazipo tena na habari njema ni kuwa: “Tukiamua Tunaweza” na Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph  Magufuli imethibitisha ukweli huo.

68.    Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Serikali kupongeza mchango mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi wote ambao wamelipa kodi kwa mujibu wa sheria. Aidha, napenda kutambua mchango adhimu wa mashirika na taasisi ambazo Serikali ina hisa yaliyotoa gawio au asilimia 15 ya mapato ghafi kuingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inayataka mashirika yote ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa kuhakikisha kuwa wanatoa gawio au mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi na Msajili wa Hazina asimamie kikamilifu utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali.
69.    Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu, mwezi Oktoba mwaka huu wa 2019 tutafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Serikali kwa upande wake imejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo. Ninawasihi wananchi wote wenye sifa wajitokeze kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. Aidha, katika kuchagua viongozi wa ngazi hiyo, tafuteni Watanzania wenye sifa zifuatazo:
(i)    Awe mchapakazi mwenye kujitoa sadaka kuwatumikia watu, hasa wananchi wa kawaida;
(ii)    Awe mwepesi kuona, kusikiliza na kuguswa na shida za wananchi wake. Tena awe jasiri katika kupigania haki za wanyonge na awe na uwezo na ubunifu katika kutatua kero za wananchi hao;
(iii)    Awe mwadilifu, anayechukia na kupiga vita rushwa na ufisadi kwa matendo;
(iv)    Anayetambua fursa zilizopo katika eneo lake, kubuni mikakati ya kuwaendeleza wananchi anaowaongoza na kuwatia watu wake hamasa ya kuthubutu kutumia fursa hizo;
(v)    Awe mtetezi hodari wa kulinda mazingira na mpambanaji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi;
(vi)    Mwenye kutoabudu nyadhifa; anayetambua kuwa nafasi na vyeo tulivyopewa ni vya muda tu. Ni vya kupita! Thamani halisi ya kiongozi ni kufanya kazi kwa bidii na kuacha kumbukumbu nzuri kwa ustawi wa eneo analoliongoza na Taifa kwa ujumla;

(vii)    Awe kama mchezaji mzuri wa kiungo katika timu ya ushindi, anayetambua kwamba mkono mmoja hauwezi kupiga makofi ya shangwe;
(viii)    Awe mwenye kutambua kwamba kazi za kiongozi zina maana sana kwa kuwa zinamwezesha kubadilisha maisha ya maelfu ya Watanzania, hasa wanyonge, kuwa bora zaidi;
(ix)    Awe na uwezo wa kuwaeleza wananchi kinaganaga kuhusu Serikali yao inawapeleka wapi na wajibu wa kila mmoja ili waendelee kuiunga mkono; na
(x)    Awe anatoka ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni CCM!
Naomba nikiri kuwa, sifa hizi nilizozitaja nimeziazima kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ridhaa yake!
70.    Mheshimiwa Spika, nawaomba viongozi wote wa dini pamoja na waumini wote kila mmoja kwa imani yake, tuendelee kumwombea Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema, hekima, busara na kumwongoza kwa kila jambo alifanyalo kuliletea Taifa letu maendeleo.
71.    Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambao wamekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na maandalizi na uratibu wa bajeti hii ya Watanzania. Kipekee ninawashukuru Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye ni Mbunge mahiri wa Jimbo la Kondoa; Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bwana Doto M. James, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Bi. Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M. Kazungu na Bwana Adolf H. Ndunguru pamoja na watumishi wa ngazi zote wa Wizara ya Fedha na Mipango. Vile vile, ninamshukuru Profesa Florens D. Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Naibu Gavana Dkt. Yamungu Kayandabila, Dkt. Bernard Kibesse na Bwana Julian Raphael Banzi kwa kusimamia vema sekta nyeti ya fedha. Kwa nafasi ya kipekee, napenda nimpongeze Dkt. Edwin Mhede kwa kuteuliwa na Rais kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato

Tanzania (TRA). Ni matumaini yangu na ya Watanzania kuwa atakuwa chachu ya kujenga taswira mpya ya TRA itakayoongeza mapato ya Serikali bila manyanyaso kwa wafanya biashara.
72.    Mheshimiwa Spika, ninawashukuru viongozi na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao. Nawashukuru Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Taasisi na Wakala za Serikali zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wafanyakazi wake wote kwa kazi nzuri wanazofanya na kuendelea kunipa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi wa hali ya juu.
73.    Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia wananchi wenzangu wa Wilaya ya Buhigwe na mkoa wetu wa Kigoma ambao walinilea na kunifundisha kufanya kazi. Mwisho kabisa naishukuru familia yangu, hususan mke wangu mpenzi na rafiki yangu Mbonimpaye, watoto, wajukuu, ndugu, jamaa na marafiki zetu wote tuliopewa na Mungu. Asanteni kwa kuniombea msaada wa Mungu katika kazi hii, usiku na mchana. Nami ninasema kwa kila mmoja wao:

“Bwana akubarikie na kukulinda,
Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili, Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani”
Hesabu 6: 24-26.
Nimalizie kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa baraka zake na kuniwezesha kuwasilisha hotuba hii. Aidha, apende kuendelea kunijalia uwezo na unyenyekevu wa kulitumikia Taifa letu na wananchi wake kwa uadilifu. Asanteni sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa kunisikiliza.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA

74.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Comments

Popular Posts