Serikali yakaza msimamo kodi taulo za kike
Dodoma. Serikali imepigilia msumari wa mwisho kuhusu taulo za kike (sodo) kuwa ni jambo gumu kuondoa kodi katika bidhaa hiyo.
Naibu waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji akizungumza jana bungeni jijini Dodoma alisema kama kodi zitaondolewa kwenye bidhaa hiyo, bado haiwezi kusaidia kitu zaidi ya kupunguza mapato ya Serikali tu.
Naibu waziri huyo alikuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda aliyeuliza ni lini Serikali itasimamia kwa ukamilifu suala la bei za taulo za kike ili zishuke (bei) na kusaidia afya ya wanawake hasa wenye umri wa usichana.
Kijaji alisema hatua ya kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo za kike ililenga kupunguza sehemu ya gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo na ilitegemea kushusha bei ya bidhaa hiyo.
Alisema bei ya bidhaa hiyo katika soko inaamuliwa na nguvu ya soko lenyewe na gharama nyingine za uzalishaji na uendeshaji wa gharama za malighafi, mishahara, uwekezaji, mifumo ya uzalishaji na ubora wa bidhaa.
“Mambo haya yalipelekwa kisiasa zaidi kuliko uhalisia, tukiondoa kodi haisaidii kitu zaidi ya kupunguza mapato ya Serikali, lakini mtazamo wetu kwa sasa ni kutoa bidhaa hiyo bure,” alisema Kijaji.
Wakati naibu waziri huyo akisema hayo bungeni, nje ya Bunge Mwananchi lilizungumza na mbunge wa viti maalumu (Chadema), Upendo Peneza ambaye amekuwa akipigania kuhusu jambo hilo bungeni mara kwa mara. Alisema suala la kodi kuondolewa ni jambo jema.
Alisema tatizo lipo kwa Serikali kuwasimamia wafanyabiashara hasa kwa kutaka wafanyabiashara wakubwa kuwa na bei elekezi.
“Ingawa kiwango kilichopunguzwa na Vat ni kidogo, suala la Serikali kugawa pedi bure shuleni bado ni la muhimu. Serikali inaweza kuzitaka tu halmashauri kusimamia utoaji wa pedi hizo bure, itafanikiwa,” alisema Peneza.
“Ingawa kiwango kilichopunguzwa na Vat ni kidogo, suala la Serikali kugawa pedi bure shuleni bado ni la muhimu. Serikali inaweza kuzitaka tu halmashauri kusimamia utoaji wa pedi hizo bure, itafanikiwa,” alisema Peneza.
Suala hilo limeshika kasi huku jana ikiwa ni siku ya hedhi duniani ambayo waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliitumia kuzungumzia suala la gharama kubwa za taulo hizo na akaahidi kuwa anajipanga kumwandikia barua waziri wa Viwanda ili kujua tatizo liko wapi.
Comments
Post a Comment