Wiki ngumu kwa mawaziri wa Elimu na Maji bungeni


Dodoma. Bunge linaendelea na vikao vyake jijini Dodoma leo likiingia katika wiki ya nne lakini macho ni Alhamisi ijayo wakati Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa atakapowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo.

Leo, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako anasoma mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo ambayo yatajadiliwa kwa siku mbili.
Bajeti ya Wizara ya Maji ambayo itajadiliwa kwa siku tatu, ndiyo inayotarajiwa kuwa na mjadala mpana kutokana na wabunge wengi kujiandikisha kuchangia.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, alisema kuna ‘mchwa’ wametamalaki katika miradi mingi ya maji na sasa anamsubiri Rais John Magufuli jimboni kwake amfikishie kilio chake.
Alisema haoni mtu wa kumaliza changamoto ya kuhujumu miradi hiyo kuanzia kwenye tenda za ujenzi hadi katika utekelezaji akidai kuwa watu wamekuwa wakiiba fedha mchana kweupe.
Keisy alisema kuna mchwa katika halmashauri nyingi kwa sababu ‘mashimo’ ya kutumbukiza fedha za miradi ya maji yamekuwa makubwa kupita kiasi.
Waziri Mbarawa hana shaka
Alipoulizwa kuhusu wingi wa wabunge kujiandikisha kuchangia wakati wa mjadala wa wizara yake, Profesa Mbarawa alisema hana taarifa kuwa wabunge wameikamia hotuba yake lakini anachojua kila kitu kiko vizuri.
Alisema ana imani kuwa bajeti ya wizara yake itapita salama na hatarajii kama kutakuwa na ugumu kwenye kupitishwa.
“Kwa sasa niko kwenye ziara Mbeya, lakini mambo mengi wasubiri hotuba yangu itakuja na majibu yote au nisubiri nikifika Dodoma nipigie,” alisema.
Katika michango yao tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, wabunge wamekuwa wakihoji juu ya mkwamo wa miradi ya maji na Rais John Magufuli katika ziara zake alizozifanya hivi karibuni, amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ya kukosa maji safi na salama katika maeneo mengi.
Akiwa mkoani Njombe mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa maji ajitathimini.

Comments