UCHOKOZI WA EDO : Ni vichaa tu ndio wanaweza kupinga maendeleo




Majuzi alisimama Mheshimiwa Sugu pale Mbeya na kumsifia Namba Moja. Ilipendeza sana. Akamwambia wazi kwamba anafanya kazi nzuri lakini kuna maeneo ambayo hawaridhiki na inabidi wayaseme hadharani. Alipoendelea kuongea zaidi akaondolewa kwa nguvu. Mheshimiwa akaamuru arudi kumalizia.

Huwa nawaza. Anayepinga hisia za Namba Moja si anaweza kuwa na kichaa? Ndio. Namba Moja anataka maendeleo. Anataka barabara za juu. Ana ndege zetu. Anataka treni ya umeme. Anataka madini yasiibiwe. Anataka nchi ikusanye kodi.
Hivi mwanadamu mwenye akili timamu anaweza kupinga? Sidhani. Yote haya huwa yanatumiwa na watu wa vyama vyote. Dini zote. Rangi zote. Kupinga ni wendawazimu. Tatizo linalojitokeza ni dogo tu. Tunafikaje tunakotaka kwenda? Hapa yanaibuka mawazo tofauti.
Namba Moja akisema anataka kutumia njia hii, mtu mwingine atashauri tutumie njia ile. Hii ndio akili nzuri katika kuendesha nchi. Ukimfuatilia Namba Moja siku hizi utaona jinsi alivyobadili mawazo yake kuhusu baadhi ya mambo. Amebadili mitazamo yake kuhusu masuala ya kodi na mengi mengiyo.
Wakati biashara zinafungwa watu walipiga kofi. Wakati Namba Moja anawaelekeza watu wake wa kodi wawe makini na biashara ziendelee watu bado walipiga kofi. Unajiuliza, watu wa namna hii wanamsaidia Namba Moja kweli?
Tatizo letu ni kupiga kofi katika kila kitu au kuponda kila kitu. Tuachane na unafiki huu. Hatumsaidii Namba Moja. Muda si mrefu Namba Moja atawabaini watu wanaomhujumu. Ni wale wale wanaojifanya washauri wake, halafu hawa wanaojaribu kumwambia kitu tofauti atabaini kwamba hawana nia njema.
Jaribu kujiuliza pale mjengoni Dodoma. Waliopiga kofi wakati mikataba ya madini ikipitishwa katika awamu iliyopita ndio hao hao waliopiga kofi wakati Namba Moja anabadilisha kibao na kulaumu kuhusu mikataba mibovu ya madini.
Kabla mambo mengi hayajaharibika tunahitaji kubadilishana mawazo. Tunahitaji kufikiria njia tofauti. Sio dhambi. Sioni mtu anayeweza kupinga uwepo wa mambo mengi mazuri anayofikiria Namba Moja. Tatizo kuna watu wanataka kupongeza kila kitu, na kuna watu wanataka kupinga kila kitu. Makundi yote haya mawili yanasahau kwamba tukikwama tunakwama sote.

Comments