Rais Magufuli amtega RC Chalamila, atuma salamu kwa ma-RC wengine

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais John Magufuli kumsifia mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa utendaji kazi mzuri, leo Jumamosi Aprili 27, 2019, amempa kipimo kitakachomuwezesha mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya kuendelea na kazi hiyo.
Rais Magufuli amempa jaribu RC Chalamila la kuanzisha soko la dhahabu wilayani Chunya ndani ya siku saba akisema hili litakuwa jaribu kubwa kuendelea kuwepo katika nafasi hiyo.
Rais Magufuli ametoa mtego huo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Sabasaba wilayani Chunya mkoani Mbeya ambao ulikuwa unarushwa moja kwa moja (Live) na vyombo mbalimbali vya habari.
Amesema kuwa alishatoa maagizo kuwa kila mkoa ambao kuna uchimbaji wa madini ufungue kituo cha kuuzia dhahabu hivyo inashangaza kuona bado mikoa yote haijaanzisha isipokua mkoa wa Geita.
“Nilipokutana na viongozi wa madini pamoja na viongozi wa mikoa yote ya Tanzania Bara nilitoa maelekezo kwamba wakafungue masoko ya madini, tangu nimefika hapa (Chunya) sijaliona soko hilo,” amesema.
“Sasa nakuagiza mkuu wa mkoa (Albert Chalamila) pamoja na wizara hii (Wizara ya Madini), nataka soko la dhahabu hapa Chunya lianze, hakuna sababu ya soko hilo kutoanzishwa hapa Chunya,’’ amesema.
“Ninataka ndani ya siku saba hili soko liwe limeshafunguliwa hapa,’’ amesisitiza Rais Magufuli.
Amesema kuwa haoni sababu ya mikoa mingine kushindwa kufungua masoko hayo wakati mkoa wa Geita walishafungua.
“Kama mkuu wa mkoa wa Geita amefungua, sioni sababu kwa nini wakuu wa mikoa wengine ambako madini mbalimbali yanazalishwa wamekaa kimya, wanasubiri nini? Amehoji Rais Magufuli na kuongeza:
“Nimeshatoa maelekezo ni kutimiza, sasa mkuu wa mkoa jana nimeshakusifia lakini kwenye soko, hili litakuwa jaribu lako kubwa sana kwa shetani, mheshimiwa mkuu wa mkoa nakueleza hili sifurahi,” amemuambia RC Chalamila.
Pia, amewataka wakuu wa mikoa wengine ambao kwenye maeneo yao kuna uzalisjhaji wa madini wafungue vituo hivyo.
‘’Najua kuna wakuu wa mikoa wengine wananisikiliza, hawataki kufanya kazi, kama mkuu mkoa wa Geita ameweza wakuu wa mikoa mingine mnasubiri nini? Amehoji
“Na hili agizo si kwa mkuu wa mkoa tu wa Mbeya, wa Katavi ajiandae, wa Rukwa, Singida, Arusha ajiandae hivyo hivyo, siwezi kuwa na wakuu wa mikoa ambao natoa maagizo hawatekelezi, kwangu hapana,” amesisitiza Rais Magufuli kwa wakuu wa mikoa ambao maeneo yao yanachimbwa madini.
Jana akiwa kwenye mkutano wa hadhara mjini Mbeya, Rais Magufuli alimsifia mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akibainisha kuwa hakumchagua kwa kubahatisha.

Comments
Post a Comment