DC amuweka ndani mwenyekiti wa kijiji anayedaiwa kutafuna mamilioni ya fidia
Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ameagiza kukamatwa mara moja, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ewor Ndeke, Kata ya Kimokokua, Moses Lesikar Leng’ese Ole Nasuaku kwa tuhuma za kula fedha za wanakijiji kiasi cha Sh69 milioni zilizotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kupisha mradi wa umeme.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna alisema jana kuwa wanamshikilia mtuhumiwa huyo na uchunguzi bado unaendelea.
Mwaisumbe alisema mwenyekiti huyo pia amepewa siku saba kurejesha fedha hizo wakati hatua nyingine za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa.
Akizungumza na Nasi jana jijini Arusha, Mwaisumbe alisema amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho wakimtuhumu mwenyekiti wao kujipatia fedha za mradi huo wa Rea baada ya kudanganya kuwa maeneo yanayopitiwa na mradi huo ni mali yake wakati si kweli.
“Taarifa zinaonyesha huyu mwenyekiti alilipwa fedha hizo mara mbili akitumia majina tofauti, awali alilipwa Sh66 milioni kwa hekari saba ambazo ni mali yake halali na Sh69 milioni kwa hekari 10 huku akitumia majina ya Lesikar Leng’ese na Moses Leng’ese na kujipatia kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria,” alidai DC huyo.
Alisema wanakijiji saba waliohojiwa na polisi juu ya tuhuma za mwenyekiti huyo, watano walithibitisha maeneo hayo ni ya kijiji huku wawili wakisema ni mali ya mwenyekiti huyo na kwamba anayamiliki tangu mwaka 2013.
Hata hivyo, hatua ya upimaji maeneo ya mradi ilishapita tangu mwaka 2008.
“Hivyo nimeamuru akamatwe kwa kosa la kujipatia fedha kinyume cha sheria kama kosa lake litathibitishwa, atakuwa anaangukia kwenye uhujumu uchumi, nimempa siku saba arejeshe fedha hizo na baada ya hapo tutampeleka mahakamani,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Aliwataja wengine waliotumia mpango huo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia maeneo hayo ya kijiji ambao wanatafutwa kuwa Elia Shapashina Kool, Luca Sambeke Ole Mboloso, mwenyekiti wa Kitongoji cha Maatiani aliyetambulika kwa jina moja la Kerimboti, Sindiyo Leakui na Nengolo Sadaka wote wakazi wa Kijiji cha Ewor Ndeke.
“Fedha hizo zilizopaswa kuwekwa kwenye akaunti ya kijiji, lakini mwenyekiti huyo na wenzake walitumia akaunti binafsi kujinufaisha” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa kijiji hicho, Mbayo Olotito alisema, “hatuishii hapa, kilio hiki tumejipanga kukipeleka kwa mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ili kushinikiza huyu bwana achukuliwe hatua zaidi za kisheria yeye na wenzake walioshiriki kuhujumu maeneo ya kijiji na kujinufaisha wenyewe.”
Licha ya tukio hilo, REA imeendelea kuwalipa fidia wananchi katika wilaya hiyo.

Comments
Post a Comment