Serikali Kuendelea Kusimamia Maadili ya Askari Polisi



Serikali imesema haitakua tayari kuona Jeshi la Polisi linachafuliwa na baadhi ya Askari Polisi wasiofuta maadili huku ikisisitiza haitosita kumchukulia hatua askari atakaebanika kukiuka maadili

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akifunga mafunzo kwa Vikundi vya Ulinzi Shirikishi Visiwani Zanzibar ambapo jumla wa walinzi 681 walihitimu mafunzo hayo

Akizungumza na wahitimu pamoja na askari katika hafla hiyo Naibu Waziri Masauni alisema Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na askari polisi waadilifu huku akiweka wazi kuwepo kwa askari wasio waadilifu

“Jeshi letu la Polisi lina miiko yake katika utendaji wa kazi zake,lakini wapo askari wachache wanaovujisha taarifa kwa wahalifu, wanasaidia wahalifu kutenda makosa sambamba na kupokea rushwa,hali hiyo haikubaliki na atakebainika hatutosita kumchukukia hatua kwa mujibu wa taratibu za jeshi,” alisema Masauni

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Saleh Mohamed Saleh, aliwataka wananchi kufichua wahalifu wanaowafahamu katika makazi yao ili matendo ya uhalifu yaweze kupungua

“Polisi Jamii ni dhana pana,tunawategemea wananchi mtusaidie kufichua wahalifu katika maeneo mnayoishi maana uhalifu ukifanyika nyie ndio mnaathirika hivyo basi ni bora mkawa mabalozi wazuri katika maeneo yenu kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi,” alisema Kamishna Saleh

Katika mafunzo hayo jumla ya Walinzi Shirikishi 681 walihitimu ambapo walipitishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukamataji salama,namna ya kuendesha doria,jinsi ya kumfikisha mtuhumiwa kituo cha polisi na elimu jinsi ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto.


                    KWA HABARI ZA MICHEZO PAKUA APP YETU YA MICHEZO SASA

Comments

Popular Posts