Halmashauri ya jiji la Dodoma Yaandaa Viwanja 161,069
Halmashauri ya jiji la Dodoma imeandaa michoro 245 yenye viwanja 161,069 kwa kipindi cha mwezi Mei, 2017 hadi Januari 2019,.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa idara ya Ardhi, Mipango Miji, na Maliasili Joseph Mafuru alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za sekta ya Ardhi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na nusu ya mwaka 2018/2019 kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika ukumbi wa halmashauri ya jiji la Dodoma jana.
Mafuru alisema kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwezi Mei 2017 hadi Januari, 2019, Halmashauri hiyo katika utekelezaji wa mipango kina iliandaa michoro 245.
“Michoro hiyo ina jumla ya viwanja 161,069, ambapo upangaji huu unajumuisha michoro ya maeneo mapya, maeneo ya urasimishaji, na upangaji uliotekelezwa na Halmashauri” alisema Mafuru.
Ongezeko hilo ni kubwa ikilinganishwa na michoro 148 yenye viwanja 69,353 wakati wa miaka 44 ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1973 hadi mwezi Mei, 2017, aliongeza.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angelina Mabula alifanya ziara ya kikazi ya siku moja katika halmashauri ya jiji la Dodoma kukagua utekelezaji wa shughuli za sekta ya Ardhi na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Comments
Post a Comment