TAMISEMI: Hatujazuia uhamisho wa walimu,Tumeshatoa uhamisho wa walimu 15,000 hadi sasa,
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhandisi Musa Iyombe, amesema taarifa zinazosambaa kuwa wizara hiyo imepiga marufuku uhamisho wa walimu hazina ukweli wowote na ni za upotoshaji.
Badala yake alisema, kilichofanyika ni kusitishwa kwa suala hilo kupisha tathmini ya kuangalia upatikanaji wa walimu katika maeneo ya pembezoni kutokana na walimu wengi kuonekana kuhama kutoka maeneo hayo kuja mjini.
Hayo aliyasema jana ofisini kwake, katika mahojiano na Jamvi la Habari kufuatia taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Tamisemi wamepiga marufuku walimu kuhama.
Mhandisi Iyombe alisema, hadi sasa tayari wametoa vibali vya uamisho wa walimu 15,000, lakini wamegundua walimu wengi wanatoka maeneo ya pembezoni kwenda maeneo ya mijini na hivyo umeleta athari kubwa.
“Si kama tumepiga marufuku uhamisho bali tumesimamisha kwa muda tufanye tathmini kuona nini kinasababisha walimu wengi kuhama na namna ya kukabiliana na uhaba uliojitokeza maeneo ya pembezoni na baada ya tathmini uhamisho utakuwepo kama kawaida,” alisema.
Alibainisha, katika kukabiliana na changamoto hiyo waliomba kibali cha kuajiri walimu 5,000 lakini walipata kibali cha kuajiri walimu 3,000 na kwa kwamba wamefanya tena maombi ya kupatiwa walimu 2,000.
Katika hatua nyingine alizungumzia taarifa za kuwepo malalamiko ya baadhi ya walimu waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi kuwa wamepoteza baadhi maslahi yao na kusema taarifa hizo zina upotoshaji ndani yake.
Alisema, si kweli kwamba kupelekwa shule za msingi kumepoteza maslahi ya walimu hao kwani wameendelea kulipwa mishahara yao na maslahi mengine kama awali bila kupunguzwa.
Aliongeza kuwa awali kulikuwa na malalamiko kuwa kuhamishwa huko kunaongeza umbali wa makazi ya walimu na ilipo shule hivyo wizara kuelekeza walimu wahamishiwe shule zilizopo karibu.
“Hata hivyo walilalamika tena kwamba ni karibu mno basi tukasema wahamishiwe umbali uziozidi maili 6,” alisema Iyombe.
Aisha, lengo la kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu ya msingi kwa wanafunzi kufundishwa na walimu wazuri.
“Hatutaki wanafunzi wafundishwe na watu wasio na weledi hivyo kufanya hivi ni kuhakikisha kuwa elimu wanayopatiwa ni ya uhakika,” alisema Iyombe.
Wakati huohuo ametoa rai kwa wadau wa maendeleo kufuata utaratibu mpya wa kuchangia maendeleo ya elimu nchini kwa kusaidia kuboresha miundombinu badala ya kuiachia serikali pekee.
Alisema awali ilizoeleka kuwa washirika wa maendeleo ya elimu wanachangia katika utoaji wa mafunzo na semina huku wakidai kuwa suala la miundombinu ni la serikali.
“Wapo ambao wameanza kutuelewa na wanachangia ujenzi na upatikanaji wa miondombinu ya elimu badala ya kujikita tu katika utoaji wa mafunzo, tunaomba wengine nao wajaribu kuona umuhimu wa kuchangia kwenye miundombinu,” alisisitiza.
Alisema wameendelea kushirikiana na washirika na wananchi katika ujenzi wa miundombinu hasa baada ya kuongezeka kwa idadi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi baada ya serikali kuanza kutoa elimu bila malipo.
Application ya CCM NEWS Uweze Pata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi


Comments
Post a Comment