Ngome ya Lowassa Monduli yatikiswa



Dar/Arusha. Unaweza kushangaa hatua ya aliyekuwa mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga kutangaza usiku kurejea CCM, lakini unaweza kushangaa zaidi pale unapobaini mbunge huyo alikuwa mtu wa karibu na mrithi wa Edward Lowassa katika jimbo hilo.
Lowassa aliyewahi kuwa waziri mkuu, aliliongoza Jimbo la Monduli kwa miaka 20, kuanzia mwaka 1995 hadi 2015 akiwa CCM na kumwachia Kalanga kuwaongoza wana Monduli huku yeye akiwa na ndoto ya kuwania urais.
Kalanga alijiunga na Chadema mwaka 2015 sawa na Lowassa mwaka huo, Julai 28 ambapo waziri mkuu huyo wa zamani alipitishwa na chama hicho kuwania urais akiungwa mkono na Ukawa huku Kalanga akipata baraka za Lowassa kuwania ubunge wa Monduli.
Ingawa wengi waliamini kuwa chaguo namba moja la Lowassa kurithi Jimbo la Monduli lilikuwa Namelok Sokoine, lakini mtoto huyo wa waziri mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine aliamua kubaki CCM ambako aliteuliwa kuwa mbunge wa viti maalumu.
Uamuzi wa Kalanga aliyewatumikia wana Monduli kwa miaka zaidi ya miwili umewashtua wengi akiwamo Lowassa mwenyewe hasa ikizingatiwa nguvu na ushawishi alioutumia kuhakikisha anayeliongoza jimbo hilo anakuwa na baraka zake.
Kalanga anaungana na wabunge wengine watatu wa upinzani waliohamia CCM na mmoja kati yao, Mwita Waitara (Chadema) akichukua uamuzi huo Jumamosi iliyopita ya Julai 28.
Wengine ni Dk Godwin Mollel (Siha-Chadema) na Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) waliotimkia CCM na kupitishwa tena na chama hicho tawala kuwania ubunge katika majimbo yaleyale na kushinda.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alizungumzia uamuzi huo wa wabunge kuhama akisema, “Wanahama kwa sababu wanaona walipata ubunge kwa upepo tu na wanaona ili kuendelea kuwa salama njia pekee ni kujikomba CCM.”
Alisema wameangalia mazingira na kubaini, “Ule upepo wa mwaka 2015 unaweza usiwepo, ili kujihakikishia ubunge mwaka 2020 na kwa kuwa CCM inawapokea, wanaona bora waende huko.”
Akigusia ushawishi wa Lowassa, Dk Mbunda alisema mazingira ya mwaka 2015 si ya sasa akisema, “Kwa sasa hakuna kufanya siasa, Lowassa hapati muda wa kufanya mikutano jambo linalomfanya kuwa kimya, ameamua kuwaacha kila aliyekuwa akimwamini atumie akili zake.”
Alisema ukimya huo wa Lowassa umewafanya wafuasi wake wasijue kipi cha kufanya au kinachoendelea. “Na wanajikuta kama hivyo wanaondoka, kujihakikishia usalama mwaka 2020.”
Ameumiza wana Monduli
Jana asubuhi, Mwananchi lilimtafuta Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kupata mtazamo wake juu ya uamuzi wa Kalanga na kwa ufupi alisema hajapata taarifa.
“Nikipata taarifa za kutosha ndio nitazungumza,” alisema.
Baadaye jioni, taarifa iliyotolewa na ofisi yake ilimkariri akisema, “Kwa sababu zozote atakazokuwa amezitoa mbunge wangu wa Monduli ni haki yake kikatiba.
“Najua wana Monduli wote nikiwemo mimi uamuzi huo umetuhuzunisha na kutuumiza.”
Lowassa alisema, “Lakini nawaomba msife moyo hata dakika moja zaidi, kitendo hicho kizidi kutupa nguvu, ari, hamasa na mori zaidi ya kuendeleza mapambano ya kuitafuta demokrasia na mabadiliko ya kweli.
“Hakuna jipya katika hili, ni kawaida kwa wanasiasa duniani kuhama vyama vyao na kubadilishana vijiti. Monduli imetupa heshima kwenye harakati za mabadiliko, naomba msife moyo.”
Kisha, mwanasiasa huyo nguli nchini alisema, “Moto ule tuliouwasha 2015 hauwezi hata mara moja kuzimwa na mbinu hizi. Wataondoka kina Kalanga wengi tu lakini kasi ya moto ule jinsi ilivyo hivi sasa ndani ya mioyo ya Watanzania ni ya ‘moto wa kiangazi’.”
Chadema yamshangaa Kalanga
Chama chake alichokaa miaka miwili na ushee, Chadema, kimeshangazwa na uamuzi wa Kalanga kutangaza kurejea CCM usiku wa manane wakati waliompigia kura wakiwa wamelala.
Kalanga akiwa pamoja na katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitangaza kuhamia CCM kati ya saa 5:57 na 6:30 usiku wa kuamkia jana katika mazungumzo aliyoyaitisha Polepole na kuyarusha moja kwa moja kupitia kurasa zake za Facebook na Twitter.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema, “Tumeshangazwa na Kalanga kuondoka usiku watu wakiwa wamelala hata wa jimbo lake, haya ni mambo ya ajabu.
“Hivi kama alikuwa na nia njema ya kuondoka kwa nini hakuondoka jana (juzi) mchana au angesubiri kukuche na atangaze kuhama tena mbele ya waandishi, lakini kwa kuwa hana nia njema ameondoka usiku.”
Mrema alisema walipopata tetesi za Kalanga kuchukua uamuzi wa kurudi CCM, walimuuliza na aliwathibitishia kuwa harejei katika chama hicho tawala.
“Hadi jana (juzi) saa nne usiku katika makundi, (Kalanga) alikuwa anasema harudi CCM. Inawezekana huo muda ndio alifika bei na kushinikizwa atangaze usiku huohuo wakihofia anaweza kubadili msimamo,” alidai Mrema.
Alichosema Kalanga
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Kalanga alisema amechukua uamuzi wa kuhamia CCM ili kulinda masilahi ya wananchi waliompigia kura.
Alisema mbunge ni mwakilishi wa wananchi na kwamba, kuna wakati msimamo wa chama hukinzana na juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi.
“Msimamo wa chama kwenye uwajibikaji wa pamoja lazima uheshimu kutokukubaliana na Serikali kwenye mambo fulani, lakini wakati mwingine uamuzi huo unakuathiri wewe (mbunge) na wananchi wako kwa sababu una mkataba na wananchi wako,” alisema. Kalanga alisema ni vyema afuate matakwa ya wananchi waliomchagua kuliko kupingana na viongozi wa Chadema katika vikao vya chama hicho, jambo ambalo lingemfanya aonekane msaliti.
“Ningeweza kuonekana mnafiki wakati lengo langu lilikuwa kutimiza ahadi nilizozitoa wakati wa kampeni,” alisema.
Kuhusu changamoto za kufanya siasa nchini kwa sasa, alisema jambo hilo linazungumzika na muafaka unaweza kupatikana.
Alisema wanaodai wabunge na madiwani wa Chadema wanakimbilia CCM kutokana na hofu ya kushindwa na wagombea wa chama tawala 2020 hawapo sahihi.
Alijitolea mfano yeye jinsi alivyoibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, licha ya kukabiliwa na ushindani mkubwa.
Alipoulizwa kama uamuzi wake huo umetokana na ushawishi wa Lowassa, Kalanga alisema uamuzi aliouchukua hakushawishiwa na mtu yeyote.
“Wanaosema nimenunuliwa siwezi kuwazuia kuhisi hivyo. Nataka niwaambie kuwa nina mshahara na marupurupu yangu, nimeona nikiwa mbunge bila kushirikiana na Serikali siwezi kuwatumikia vyema,” alisema.
Kauli ya Polepole
Mwananchi lilimtafuta Polepole kuhusu hamahama inayoendelea na kujua kwa nini mazungumzo yake na Kalanga yalifanyika usiku na si asubuhi au mchana.
Alisema mkutano huo ulifanyika usiku kwa kuwa ndio muda pekee uliopatikana kutokana na kutingwa na shughuli nyingi.
“Unajua jana (juzi) nilikuwa Tarime (Mara), nikaenda Mwanza pale nilikuwa na kikao, kisha nikaenda Dar es Salaam ambako nilikuwa na shughuli. Baadaye nilikwenda Kilimanjaro na Arusha. Nilifanya mkutano jana (juzi) usiku kwa kuwa ndio muda niliokuwa nao,” alisema Polepole.
“Ingawa ilikuwa usiku, lakini mazungumzo yale yamefuatiliwa na watu wengi kwelikweli na wengi walipiga simu hadi kutoka nje ya nchi.”
Kisha, Polepole alisema, “Kuna wabunge ambao tumeweka msimamo kama chama kwamba hatuwezi kuwapokea hata wakitaka. Huwezi kuwa na mbunge yeye kazi yake ni kuota ndoto tu.”
Akijibu swali aliloulizwa kuwa fedha zinazotumika kurudia uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini haoni ni bora zingepelekwa katika maeneo mengine kama afya au kuongezea mikopo ya wanafunzi, alisema, “Pesa ya maji ipo, pesa ya kujenga barabara ipo, pesa ya kujenga reli ya kisasa ipo, pesa ya kununua ndege ipo, pesa ya kujenga shule ipo na pesa ya kuimarisha demokrasia ipo.”
Kuhusu iwapo Kalanga na Mwita watagombea tena wakati ukifika, alisema wanachokifanya kwa sasa wanachama hao wapya ni kukamilisha taratibu za uanachama na baada ya hapo kwa mujibu wa katiba ya CCM, ibara ya 4 inasema “binadamu wote ni sawa”.
Mtei atoa neno
Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei alipoulizwa maoni yake kuhusu sakata hilo, alisema viongozi wakiwamo wabunge wanaotaka kuondoka ndani ya chama hicho waondoke mapema.
Alisema baadhi yao wamechanganyikiwa na wana mpango wa kukivuruga chama. “They are confused (wamechanganyikiwa) wana mpango wa kuvuruga, wale wanaotaka kuondoka waondoke,” alisema.
Mtei aliyeanzisha chama hicho mwaka 1995 alisema hatua ya viongozi hao kuondoka ndani ya Chadema kwa madai wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli hazina mashiko.
“Sikubaliani nao na sababu ya kwamba wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli.”
Alisema katika uchaguzi wa 2020 kuna mambo makubwa yataibuka ambayo hakutaka kuyaweka hadharani huku akisisitiza kuwa mkakati wao ni kuhakikisha nchi inakuwa na demokrasia ya kweli.
Imeandaliwa na Ibrahim Yamola (Dar), Filbert Rweyemamu na Moses Mashalla (Arusha)

Comments