Ajali ilivyokatisha uhai wa mwanahabari Sagati




Dar/Geita. Ofisa uhusiano wa Wizara ya Viwanda, Shadrack Sagati amefariki katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Katoro mkoani Geita.
Katika ajali hiyo iliyotokea juzi saa 8:00 mchana, watu wengine wanne walijeruhiwa akiwamo naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Ludovick Nduhiye. Taarifa iliyotolewa jana na kaimu mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano cha wizara hiyo, Edward Nkomola zilieleza kuwa wengine waliojeruhiwa ni Nickson Matembo (mchumi), Yusuph Mbwalwa (mkaguzi wa ndani) na dereva wa gari hilo, Lucas Wambura.
Akizungumzia mipango ya mazishi, waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage alisema: “Kinachofanyika sasa ni kuwasiliana na familia na baada ya hapo tutakuwa na la kusema kuhusu kinachoendelea.”
Hata hivyo, msemaji wa familia, Masau Bwire alisema mwili wa Sagati utawasili jijini Dar es Salaam Alhamisi na siku hiyo hiyo ndugu na jamaa watatoa heshima za mwisho, Ijumaa utasafarishwa kwenda mkoani Mara kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi kijiji cha Mwiruruma wilayani Bunda.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema ajali hiyo ilihusisha gari la wizara hiyo aina ya Toyota Land Cruiser chanzo kikiwa nidereva wa gari hilo kujaribu kumkwepa mtoto mwenye umri wa miaka saba aliyekatiza barabarani eneo la Mintoko lililopo kati ya Bwanga na Buseresere.

Comments