VIDEO: Lugola amkomalia Lugumi, ampa miezi minne

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Dar es Salaam.  Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amesema mmiliki wa kampuni ya Lugumi, Said Lugumi amepewa miezi minne kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole kwenye baadhi ya vituo vya polisi nchini.
Lugola ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 31, 2018 baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Lugumi, akiwa sambamba na watendaji wengine wa wizara hiyo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za wizara hiyo jijini hapa, Lugumi aliambatana na mwanasheria wake, Onesmo Mpinzile.
“Nilimuita Lugumi ofisini kwangu na amekuja leo asubuhi, amekuwa muungwana na nimepata fursa ya kujadiliana naye kuhusu kukamilisha mfumo huu unaolenga kudhibiti uhalifu,” amesema Lugola akieleza kuwa Lugumi ameomba kupewa miezi minne kukamilisha kazi hiyo.
Julai 21, 2018 Lugola alimpa siku 10 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro kumfikisha Lugumi ofisini kwake.
Siku hiyo, Lugola alisema kampuni ya Lugumi ilipewa zabuni ya kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole kwenye baadhi ya vituo vya polisi baina yake na jeshi la polisi, lakini hakukamilisha kazi hiyo.
Kampuni ya Lugumi iliingia mkataba wa Sh37bilioni za Jeshi la Polisi kufunga mashine za kieletroniki za kuchukua alama za vidole katika vituo vya jeshi hilo, lakini ilibainika kutotimiza masharti baada ya kufunga mashine 14 kati ya 106, licha ya kulipwa asilimia 90 ya fedha, kwa mujibu wa mkataba.

Comments