Mazungumzo ya Lugola, Lugumi yamalizika
Mmiliki wa kampuni ya Lugumi, Said Lugumi (kulia) akiwa na mwanasheria wake, Onesmo Mpinzile wakitoka katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es Salaam leo baada ya kufanya mazungumzo na waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola.
Dar es Salaam. Mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na mmiliki wa kampuni ya Lugumi, Said Lugumi yaliyofanyika katika ofisi wizara hiyo Jijini Dar es Salaam yamemaliza.
Julai 21, 2018 Lugola alimpa siku 10 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro kumfikisha Lugumi ofisini kwake ifikapo leo, saa 2 asubuhi.
Siku hiyo, Lugola alisema kampuni ya Lugumi ilipewa zabuni ya kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole kwenye baadhi ya vituo vya polisi baina yake na jeshi la polisi, lakini hakukamilisha kazi hiyo.
Leo Jumanne Julai 31, 2018 Lugumi ameitikia wito huo kwa kufika katika ofisi hizo zilizopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, akiambatana na mwanasheria wake, Onesmo Mpinzile.
MCL Digital iliyopiga kambi katika ofisi za wizara hiyo kuanzia asubuhi, ilimshuhudia Lugola akitoka katika chumba walichofanyia mazungumzo na Lugumi, akiwa ameambatana na maofisa wengine wa wizara hiyo, kuelekea katika jengo jingine.
Baada ya takribani dakika nne, Lugumi naye alitoa katika chumba hicho akiwa pamoja na Mpinzile ,
Kampuni ya Lugumi iliingia mkataba wa Sh37bilioni za Jeshi la Polisi kufunga mashine za kieletroniki za kuchukua alama za vidole katika vituo vya jeshi hilo, lakini ilibainika kutotimiza masharti baada ya kufunga mashine 14 kati ya 106, licha ya kulipwa asilimia 90 ya fedha, kwa mujibu wa mkataba.

Comments
Post a Comment